WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amewasimamisha kazi watumishi wawili wa Halmashauri ya Wilaya
ya Chato kwa tuhuma za ubadhirifu, rushwa na matumizi mabaya ya
madaraka.
Watumishi hao ni Mkuu wa
Idara ya Kilimo na Ushirika, Bw. Mwita Mirumbe Waryuba pamoja na Afisa
Maendeleo ya Jamii wa Wilaya, Bw. Dioniz Mutayoba.
Waziri Mkuu alitoa agizo
hilo jana usiku (Jumatano, Machi 16, 2016) alipokuwa akizungumza na Watumishi wa idara zote na taasisi zilizomo kwenye wilaya ya Chato
katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Mshikamano SACCOS wilayani
humo.
Afisa Kilimo na Ushirika
anadaiwa kuchangisha kiasi cha sh. milioni 20 kutoka kwa watumishi wa
Halmashauri hiyo kwa ajili ya kuanzisha SACCOS tangu mwaka 2013 lakini
hadi sasa SACCOS Haijaanzishwa na wala fedha hizo hazijarejeshwa. Fedha
hizo zinadaiwa kuliwa na watumishi watatu (majina yamehifadhiwa).
Aidha, Bw. Waryuba
anadaiwa kutumia lugha chafu na za vitisho kwa watumishi walio chini
yake ikiwa ni pamoja na kuomba na kupokea rushwa, na kunyanyasa na
kudhalilisha kijinsia baadhi ya watumishi wa kike.
Inadaiwa pia Bw. Waryuba
alikopa bila kufuata taratibu za mikopo wilayani Chato ambapo alikopa Sh. milioni 15 kutoka Mwambao SACCOS na sh. milioni 15 nyingine kutoka
Chato Teachers’ SACCOS tangu mwaka 2015 na tangu wakati huo
hajazirejesha hali ambayo imeleta manung’uniko kutoka kwa viongozi na
wananchama wa SACCOS husika.
“Malalamiko ya watumishi
na wananchi dhidi ya huyu bwana yamefikishwa kwa Kaimu Mkurugenzi
lakini hajachukua hatua kwa sababu ni rafiki yake,” alisema Waziri Mkuu.
Kaimu Mkurugenzi huyo ni Mhandisi Joel Baha ambaye hakuwepo ukumbini
hapo kwa sababu yuko kwenye ziara ya mafunzo huko Japan.
Kwa upande wake, Bw.
Mutayoba ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya hiyo anadaiwa
kuzembea kusimamia mradi wa kufyatua matofali ya gharama nafuu
(interlocking bricks) zilizogawiwa kwa vikundi vinne vya vijana wa
wilaya hiyo.
“Mwaka 2013 Shirika la
Nyumba la Taifa (NHC) lilitoa mashine nne za kufyatulia matofali ya bei Nafuu kwa ajili ya vikundi vinne vya vijana wilayani Chato. Mashine hizo
ziligawiwa kupitia kwa Afisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya, Bw. Dioniz
Mutayoba na kila kikundi kilipewa sh. 500,000 ili waanze kazi ya
kufyatua matofali na kuyauza kwa bei nafuu katika maeneo waliyopo lakini
hadi leo hakuna kitu kilichofanyika,” inasema sehemu ya taarifa
Afisa huyo anadaiwa
kugawa mashine mbili kwa kila kata katika kata za Muganza na Buseresere
lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika kwani vikundi hivyo havikuzalisha
kitu chochote tangu wakati huo.
Aidha, Bw. Mutayoba
anatuhumiwa kudai na kupokea rushwa kwa wanachama wa vikundi vya Ujasiriamali ili aweze kuvisaidia kupata mikopo. “Yaani watu wanakuja
kukopa sh. milioni mbili halafu unawadai kitu kidogo cha sh. 300,000.
Sasa mradi waliotaka kufanya wataweza kuukamilisha kweli?,” alihoji
Waziri Mkuu.
“Huyu bwana
amelalamikiwa lakini Mkurugenzi aliyepita lakini naye anadaiwa kumlinda
kwa sababu ni rafiki yake,” alisema Waziri Mkuu na kuibua minong’ono
ndani ya ukumbi huo. Aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chato, Bw.
Clement Berege hivi sasa amehamishiwa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba.
“Katika Serikali hii
tunataka tuwe na Halmashauri zilizo safi. Lakini pia Serikali hii ina
mkakati wa kuimarisha ushirika na tunataka kuinua kilimo. Kwa hiyo basi,
TAKUKURU na polisi wachunguzeni hawa watu wawili kwa maana ya Afisa
Ushirika na Afisa Maendeleo ya Jamii na nipewe taarifa uchunguzi
utakapokamilika,” alisema Waziri Mkuu.
Mapema, akizungumza na watumishi hao,
Waziri Mkuu ambaye amewasili mkoani Geita kwa ziara ya siku Mbili
akitokea mkoani Kagera, alitumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi hao
aliwakumbusha wajibu wao wa kuwahudumia Watanzania bila kujali hali zao
na akasisitiza kuwa Serikali haitamuonea mtumishi yeyote ambaye
anatimiza wajibu wake.
“Napenda kusisitiza kuwa
malengo ya Serikali ni kuimarisha utendaji wa watumishi lakini pia
Serikali hii haitamvumilia mtu mdanganyifu, mzembe, asiye mwadilifu na
mla rushwa. Ukiharibu kazi hapa Chato mwwisho wako ni hapa hapa tu.
Usitarajie kupelekwa Bunda au kwingine ili Ukaharibu na huko,”
aliongeza.
No comments:
Post a Comment