Mkurugenzi
wa Baraza la Uwezeshaji la Taifa, Bengi Issa mwenye kilemba,
akizungumza kwenye kikao cha pamoja na Mbunge wa Mkuranga, Mheshimiwa
Abdallah Ulega kushoto kwake kwa ajili ya kuangalia namna ya
kushirikiana naye kuwasaidia na kuwawezesha wananchi wa Mkuranga. Mbunge Mkuranga asaka uwezeshwaji wa wananchi wake
Na Mwamvita Mtanda,
MBUNGE
wa Jimbo la Mkuranga, wilayani Mkuranga, mkoani Pwani, Abdallah Ulega,
jana amefanya kikao na Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji
Taifa (NEEC), Bengi Issa, kwa ajili ya kutafuta fursa ya
kuwawezesha wananchi wilayani humo.
Mbunge
wa Mkuranga, Mheshimiwa Abdallah Ulega, akizungumza jambo katika kikao
cha pamoja na Mkurugenzi wa Baraza la Uwezeshaji la Taifa (NEEC), Bengi
Issa, hayupo pichani.
Kikao
hicho pia kilihusisha Mkurugenzi wa Uwezeshaji, Afisa Maendeleo ya
Jamii Mkuranga, ambapo Pamoja na mambo mengine, kilijadili namna
ya kusaidia vikundi vilivyosajiliwa 285, vikundi vya vicoba 109,
ufugaji wa nyuki, vikundi vya wanawake, vijana na waendesha bodaboda.
Akizungumza
baada ya kikao hicho kumalizika, Ulega aliyewahi pia kuwa Mkuu wa
wilaya Kilwa, Alisema kwamba lengo ni kuona wanananchi wa Mkuranga
wanapiga hatua kutoka kwenye hali ya Ukata na kufikia kiwango kizuri,
sanjari na kufanikisha maendeleo kwa wananchi wote.
Alisema
kwamba kikao hicho kimemalizika kwa mafanikio ambapo ilishauriwa
kuwa vikundi vya kukopeshana (VICOBA) inabidi viwekwe chini ya
mwamvuli mmoja utakaoviwakilisha vyote.
“Hili litakapofanyika,
Benki ya Posta Tanzania ina utaratibu wa kutoa mikopo ya riba ndogo
kupitia Mwamvuli huo unaowakilisha vikundi vyote kwa pamoja, tukiamini
kuwa itasaidia kwa kiasi kikubwa kufanikisha ndoto zetu.
“Lengo
letu ni kuhakikisha kwamba tunaiweka Mkuranga katika kiwango
kizuri ukizingatia kwamba Wilaya hii ipo karibu na jiji la Dar es
Salaam, hivyo inaweza kukua kwa kasi kwa sababu mtu anaweza kuishi
Mkuranga na akafanya kazi au kuingia na kutoka kwa urahisi wilayani
kwetu,” alisema.
Aidha
imeshauriwa pia kuanzisha SACCOS ya wafugaji wa nyuki ili kurahisisha
upatikanaji wa mikopo Ya vifaa kwa ajili ya ufugaji wa kisasa wa nyuki,
ambapo wana vikundi wanatakiwa kuandaa mpango kazi wao utakaopelekwa
Benki ya Maendeleo kwa ajili ya mkopo, ikiwa na lengo la kuhifadhi
misitu na kuacha utafutaji wa kipato kwa njia ya kukata miti ili
kuzalisha mkaa.
Barabara Ya Kigoma-Nyakanazi Kukamilika Mwezi Mei
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiwasili
katika Kiwanja cha Ndege cha Kigoma tayari kuanza ziara ya ukaguzi wa
miundombinu katika mikoa ya ukanda wa magharibi.
Meneja
wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Kigoma, Eng. Narcis
Choma akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Profesa Makame Mbarawa (aliyevaa kofia) kuhusu ujenzi wa barabara ya
Kidahwe-Kasulu Km 50 inayojengwa na China Railway 50 Group.
Ujenzi wa barabara ya Kidahwe-Kasulu Km 50 inayojengwa na Kampuni ya China Railway 50 Group ukiendelea.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (aliyevaa
kofia) akitoa maelekezo kwa wataalamu wa ujenzi wa kampuni ya China
Railway 50 Group baada ya kukagua mitambo yao ya kupima na kutafiti
udongo kabla ya kujenga barabara.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (aliyevaa
kofia) akitoa maelekezo kwa viongozi wa Wilaya ya Kasulu mara baaada ya
kukamatwa kwa vijana wawili (waliokaa chini) kutokana na wizi wa nyaya
za mkongo wa taifa, mkoani Kigoma.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (aliyevaa
koti la kaki) akiangalia athari za mmonyoko wa udongo zilizoathiri
mkongo wa taifa wa mawasiliano katika eneo la Kidahwe mkoani Kigoma.
..
Makandarasi wanaojenga barabara ya
Kidahwe-Kasulu Km 50 na Kibondo-Nyakanazi Km 50 wametakiwa kukamilisha
ujenzi huo mwezi Mei mwakani badala ya Novemba ili kuharakisha mkakati
wa Serikali wa kuufungua mkoa wa Kigoma kwa barabara za lami.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema hayo mara baada ya kukagua
ujenzi wa barabara hiyo uliyogawanywa sehemu mbili, Kidahwe-Kasulu
inayojengwa na China Railway 50 Group na Kibondo-Nyakanazi inayojengwa
na Nyanza Road Works.
Prof. Mbarawa amewataka
makandarasi hao kuongeza kasi ya ujenzi, vifaa na wafanyakazi wenye
sifa ili barabara hizo zikamilike kwa wakati na ubora unaotakiwa.
“Tutahakikisha ifikapo Juni mwaka
huu tutakuwa tumelipa madeni yote mnayoidai Serikali hivyo fanyeni kazi
kwa uhakika kwa kuwa katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano
tayari tumeshawalipa makandarasi zaidi ya shilingi bilioni 725”, amesema
Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amesisitiza kwamba
nia ya Serikali ni kuifungua mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa
kwa barabara za lami ili kufungua ukanda wa magharibi mwa nchi
kibiashara kutokana na ukanda huo kuwa sehemu muhimu ya nchi katika
uzalishaji na kiungo kikuu kwa nchi za Congo DRC, Burundi na Rwanda.
Katika hatua nyingine Waziri Prof.
Mbarawa amewataka wafanyakazi wa Shirika la Reli (TRL), kulinda
miundombinu ya reli na kujiepusha na vitendo vya hujuma ili kuliwezesha
shirika hilo kupata shehena kubwa ya mzigo kufuatia wadau mbalimbali
kuonesha nia ya kusafirisha mizigo kwa njia ya reli
“Serikali imewekeza vya kutosha
katika Shirika la Reli hivyo mfanye kazi kibiashara ili mpate mzigo
mkubwa wa kusafirisha”, amesisitiza Prof. Mbarawa
Akizungumza na viongozi wa mkoa wa
Kigoma na taasisi zilizo chini ya wizara yake Prof. Mbarawa amewataka
kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuzuia uvamizi na uhujumu wa
miundombinu ya barabara, reli, na mkongo wa taifa wa mawasiliano na wote Watakaokiuka agizo hilo wachukuliwe hatua za haraka na za kisheria.
Prof. Mbarawa ametoa wiki moja kwa
taasisi zilizo chini ya wizara yake kuhakiki wafanyakazi ili kubaini
kama kuna wafanyakazi hewa.
Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara
nchini (TANROADS), mkoa wa Kigoma, Eng. Narcis Choma amemhakikishia
Waziri Prof. Mbarawa kuwa mkoa wa Kigoma Umejipanga vizuri katika
kudhibiti uvamizi wa miundombinu ya barabara na wale Waliojenga ndani ya
mita 22 kwenye barabara kuu wataondolewa maramoja bila kulipwa fidia.
Prof. Mbarawa yuko katika ziara ya
kukagua miundombinu katika mikoa ya kanda ya Magharibi ikiwa ni
utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa uiboreshaji wa miundombinu Ya
kanda hiyo ili kuiwezesha kufanya biashara kiurahisi na mikoa mingine ya
Tanzania na nchi za Congo DRC, Rwanda na Burundi.
No comments:
Post a Comment