Friday, 4 March 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa:Mtu akiharibu Kazi Asitarajie Uhamisho

mf4WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema watumishi wa umma wako huru kuhamia kokote wapendako lakini wahakikishe wanaenda huko wakiwa safi na kamwe mtu asiharibu kazi kazi akitarajia kuwa atahamishiwa sehemu nyingine.

“Serikali hii haina utumishi kwa mtu aliyeharibu kazi. Usije ukaharbu hapa Itilima ukadhani utaenda Bunda kuendelea na kazi. Serikali ya awamu hii haina nafasi na  watumishi wa aina hiyo,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa onyo hilo leo (Ijumaa, Machi 4, 2016) wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Itilima kwenye ukumbi wa Halmashauri ya wilaya hiyo ambao ameuzindua leo hii wilayani Itilima, mkoani Simiyu.

“Watumishi wenzangu huu ni wakati wa kubadilika na kuona mwelekeo wa Serikali hii ya awamu ya tano ukoje. Jukumu letu ni kuwatumikia Watanzania wote bila kujali itikadi zao, rangi wala dini zao,” alisisitiza.

Waziri Mkuu aliwahakikishia watumishi hao kwamba Serikali inatambua changamoto walizonazo kutokana na upya wa wilaya hiyo na mkoa huo na akawaahidi kuwa itaboresha mazingira yenu. “Msiwaadhibu wananchi kwa kisingizio cha mazingira magumu ya kazi zenu, tunajua mnayo madai ya nauli, posho za mafunzo, kupandishwa madaraja na malimbikizo ya likizo,” alisema huku akishangiliwa.
Alisema Serikali itayalipa madeni hayo japo haitamaliza yote kwa wakati mmoja ila ana uhakika wa kukamilisha walau kwa asilimia 80.

Mapema, akitoa taarifa ya wilaya hiyo, Mkuu wa wilaya hiyo, Bibi Georgina Bundala alisema wilaya hiyo iliyoanzishwa Machi 2012 na kupata Halmashauri Julai 2013 haina kituo cha polisi cha wilaya, haina gereza, Ofisi za TAKUKURU, mahakama ya wilaya wala benki.

Alisema wilaya hiyo haina hospitali ya wilaya ila akabainisha kuwa wamekwishatenga eneo la ekari 30 kwa ajili ya ujenzi huo. “Pia tumekwishapima viwanja 123 na eneo la kujenga  taasisi lenye ekari 143.8 limefanyiwa uthamini na fidia kukamilika,” alisema.

WANANCHI WAOMBWA KUTOA MAONI KUBORESHA SERA MPYA YA MAENDELEO YA UTAMADUNI.


mae1
:Kaimu Mkurugenzi Sanaa Bibi. Leah Kihimbi (kushoto) akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaamkuhusu uchangiaji wa maoni katika sera ya utamaduni inayofanyiwa mabadiliko. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Lugha Hajjat Shani KitogoPicha na: Genofeva Matemu – Maelezo
mae2
Mkurugenzi Msaidizi Lugha Hajjat Shani Kitogo (katikati) akiwaonyesha waandishi wa habari (hawapo pichani) Sera ya utamaduni ya mwaka 1997 ambayo inafanyiwa Mabadiliko Wakati wa Mkutano na waandishi wa habarileo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Sanaa Bibi. Leah Kihimbi na kulia ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Zawadi Msalla.

Tabu Mullah

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imetoa Wito kwa Wananchi na Wadau Mbalimbali Kuendelea kutoa Maoni na Mapendekezo ili yatumike kuboresha Rasimu ya Sera Mpya ya Maendeleo ya Utamaduni ya Mwaka 2016 itakayochukua Nafasi ya Sera ya Maendeleo ya Utamaduni ya mwaka 1997.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Msaidizi Lugha wa Idara ya Utamaduni Wa wizara hiyo Bi. Hajjat Shani Kitongo wakati akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu kuifanyia mabadiliko Sera ya Mwaka 1997 ili iweze kukidhi mahitaji na mabadiliko ya kijamii.

 Amesema maoni yatakayotolewa na wananchi yatajikita katika maeneo yanayothamini na kuenzi Maadili, Mila na Desturi, kuendeleza matumizi Sanifu na Fasaha ya Lugha ya Kiswahili kitaifa na kimataifa, kuwa na tafiti endelevu za Lugha za Asili kwa ajili ya kuzihifadhi na kuongeza misamiati ya Lugha ya Kiswahili.

Ameongeza kuwa Maboresho Hayo yanalenga kuwa na bidhaa na Miundombini Endelevu katika Tasnia ya Filamu na michezo ya kuigiza yenye Viwango vya Ubora vya kitaifa na kimataifa Vinavyozingatia Mila, Desturi na maadili ya Taifa, pamoja na kuwa na Uwekezaji endelevu na Mfumo Jumuishi wa Utaratibu wa kazi katika sekta ya utamaduni.

Bi. Kitongo amefafanua kuwa wananchi watatuma maoni yao kupitia barua pepe au kuleta maoni yao kwa Mkono moja kwa moja Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo au kutuma Maoni kupitia Barua pepe, christopher.mhongole@habari.go.tz pia kupitia tovuti ya wizara ya www.habari.go.tz.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara hiyo Mwanzala Kayoka Amesema kuwa lengo la kufanya mabadiliko hayo ni kuboresha Sera hiyo kulingana na wakati Haswa katika Matumizi salama na sahihi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Sekta ya Utamaduni. 

“Lengo ya kuleta mabadiliko katika Sera hii si kuunda Sera mpya bali ni kuiboresha kulingana na wakati na kuongenza yale yaliyopungua haswa katika mfumo wa TEHAMA hivyo hupelekea kuleta mfumo sahihi wa kuratibu masuala ya Utamaduni nchini” Ameongeza Mkurugenzi huyo.

Amesema kuwa ukusanyaji wa Maoni hayo umeanza  Machi 4, 2016 hadi Machi, 25 Mwaka huu, na kuwaomba wadau na wananchi wote kushiriki kikamilifu kutoa maoni yatakayosaidia uboreshaji wa Sera ya Maendeleo ya Utamaduni ya mwaka 2016.

No comments:

Post a Comment