Na. Tabu Mullah
Naibu Inspekta Jenerali wa
Polisi, Abdulrahman Kaniki amewataka askari polisi kote nchini kufanya
kazi kwa weledi ili kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano
inayoongozwa na rais Mhe.John Pombe Magufuli ambayo lengo lake ni
kuwatumikia wananchi.
Hayo aliyasema wakati alipokuwa
akifungua mafunzo ya siku tano kwa askari polisi watakaokuwa Wakitoa
huduma katika vituo vya kuhamishika (mobile police station)
vinavyotarajiwa kuanza Kazi katika mkoa wa kipolisi Kinondoni (mkoa wa
mfano) ikiwa ni utekelezaji wa Mpango wa kuboresha usalama wa raia na
mali zao nchini, mpango ambao unatekelezwa na Jeshi la Polisi kwa
ushirikiano na Ofisi ya Rais, Usimamizi na utekelezaji wa miradi (PDB).
Alisema katika kipindi hiki kila
askari anatakiwa kufanya kazi kwa kasi na kufuata maadili ili Kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora kwakuwa ndio lengo la
Jeshi la Polisi kuhakikisha wananchi wanahudumiwa vyema na kwa wakati
katika vituo vya Polisi kwakufuata taratibu na misingi ya kazi za
Polisi.
Aidha, aliwataka askari hao ambao
watakuwa wakitoa huduma katika vituo hivyo vya kuhamishika kuhakikisha
kuwa lengo la kuwepo kwa vituo hivyo linatimia kwa kutoa huduma bora na
ya haraka ili kujibu yale yote yaliyoainishwa katika mpango huo.
“Jambo kubwa lililoainishwa
katika maabara iliyoandaa mpango huu ni suala la kuchelewa kufika Katika
matukio ya kiuhalifu hivyo kwa kutumia raslimali zilizopo pamoja na
vituo hivi vya kuhamishika ni wazi kuwa sasa Tutajitahidi kufika katika Matukio mapema”Alisema Kaniki.
Kwa upande wake Mkuu wa kitengo
cha kusimamia mpango huo ndani ya Jeshi la Polisi, Naibu kamishna wa
Polisi DCP Goodluck Mongi alisema, lengo la mafunzo hayo ya siku tano
ni kuwapa Utayari askari katika kutekeleza majukumu yao ili kuleta
matokeo makubwa katika mkoa wa kipolisi Kinondoni ambao ni mkoa wa
majaribio wa mpango huo ndani ya Jeshi la Polisi.
Alisema mpango huo umeainisha
mambo mengi ikiwemo kuwepo kwa vituo vya kuhamishika ili kuweza
kuwafikia wananchi kwa haraka na vituo hivyo vitawekwa kwa awamu ili
kuhakikisha kila Anayehitaji huduma za Kipolisi hapati shida kwa kwenda
umbali mrefu kuzitafuta hali itakayopelekea kudhibiti na kuzuia uhalifu
wa aina zote.
No comments:
Post a Comment