JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemuapisha Balozi Mhandisi John
William Kijazi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi.
Hafla ya kuapishwa Balozi Kijazi
imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais Mheshimiwa
Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Wakuu wa
vyombo vya Ulinzi na Usalama, Makatibu wakuu na Naibu Katibu Wakuu.
Balozi Kijazi ambaye kabla ya
kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi alikuwa Balozi wa Tanzania nchini
India, anachukua nafasi ya Balozi Ombeni Sefue ambaye atapangiwa kazi
nyingine.
Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameagana na Mwakilishi
wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR)
anayemaliza muda wake Bi. Joyce Mends-Cole Ikulu Jijini Dar es salaam,
ambapo pamoja na mambo mengine amemshukuru kwa kazi kubwa ya kuhudumia
wakimbizi kwa kipindi chote alichokuwepo hapa nchini.
Kwa upande wake Bi. Joyce
Mends-Cole amempongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri inayofanywa na
Tanzania kuzisaidia nchi zenye matatizo, hususani migogoro ya kisiasa
ambayo husababisha watu wake kuwa wakimbizi.
Pia amepongeza kuteuliwa kwa Rais
Mstaafu wa awamu ya Tatu Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, kusaidia
usuluhishi wa mgogoro wa Burundi ambao umesababisha idadi kubwa ya
wakimbizi kukimbilia Tanzania.
Hata hivyo amesema idadi ya
wakimbizi wanaokimbilia Tanzania imepungua kutoka wakimbizi 3,000
waliokuwa wakiingia hapa nchini kwa wiki, wakati Mgogoro wa Burundi
ulipoanza hadi kufikia wakimbizi takribani 1,000 wanaingia hapa nchini
kwa wiki hivi sasa.
Aidha, Bi. Joyce Mends-Cole
amewashukuru watanzania kwa ushirikiano alioupata kwa kipindi cha miaka
mitatu aliyofanya kazi hapa nchini, na ameahidi kuwa Balozi wa
kuitangaza vyema Tanzania.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
07 Machi, 2016
No comments:
Post a Comment