Thursday, 14 May 2015

Rais Nkurunziza ‘apinduliwa’ akiwa Dar


Mara tu baada ya taarifa hizo kuzagaa, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais Jakaya Kikwete alilaani mapinduzi hayo na kuitaka nchi hiyo kuahirisha uchaguzi hadi amani ya nchi hiyo itakapotengamaa.
 
Dar es Salaam. Hamkani si shwari tena Burundi baada ya kuwapo kwa jaribio kubwa la kuipindua Serikali ya Rais Pierre Nkurunziza muda mfupi baada ya kuwasili Dar es Salaam jana katika kikao cha kutafuta suluhu ya mgogoro wa nchi hiyo kuhusu dhamira yake ya kuwania urais kwa kipindi cha tatu.
Ofisa mmoja wa jeshi la nchi hiyo, Meja Jenerali Godefroid Niyombare alitangaza kuwa Jeshi la Burundi ‘limemtimua’ Rais Nkurunziza na kwamba limeunda Serikali ya mpito kuiongoza nchi hiyo.
Mara tu baada ya taarifa hizo kuzagaa, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais Jakaya Kikwete alilaani mapinduzi hayo na kuitaka nchi hiyo kuahirisha uchaguzi hadi amani ya nchi hiyo itakapotengamaa.
Vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa jana mchana vilitawaliwa na habari za kupinduliwa Rais Nkurunziza, lakini Ikulu ya nchi hiyo ilisema huo ulikuwa “utani” na kwamba jaribio hilo lilikuwa limegonga mwamba na Nkurunziza bado ni rais wa nchi hiyo.
Tangazo la mapinduzi
Akizungumza kwenye redio moja binafsi ya Bonesha FM, Jenerali Niyombare alisema: “Rais amekiuka Katiba na amekiuka mazungumzo ya amani ya Arusha.
“Kwa kuwa Rais Nkurunziza anajiamini na amepuuza jumuiya za kimataifa zilizomshauri kuheshimu katiba na mkataba wa amani wa Arusha, tumemuondoa katika wadhifa wake pamoja na serikali yake.
“Ni muhimu kwa ajili ya kulinda heshima ya nchi... Rais Pierre Nkurunziza ameondolewa madarakani,” alisema Jenerali Niyombare ambaye alitimuliwa kazi na rais huyo mapema Februari mwaka huu akiwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Usalama, Burundi.
Alisema atafanya kazi kwa kushirikiana na taasisi za dini na wanasiasa.
Habari zilizopatikana baadaye jana jioni, zilisema Jenerali Niyombare alitangaza kufungwa kwa mipaka ya nchi hiyo, barabara na viwanja vya ndege na hakuna mtu aliyeruhusiwa kuingia.
Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, lilisema kuwa hata waandishi wa habari wa kimataifa hawakuruhusiwa kuingia nchini humo.
Hata hivyo, jana jioni shirika hilo lilisema taarifa ambazo hazikuthibitishwa ni kuwa kiongozi huyo wa mapinduzi alikuwa amekamatwa na polisi wakati akikimbilia Ubalozi wa Marekani.
Rais Nkurunziza
Kiongozi huyo wa Burundi ambaye alikuwa katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam kwa ajili ya mkutano wa marais wa Afrika Mashariki hakufika Ikulu ulipokuwa unafanyika mkutano huo na baadaye jioni ilielezwa kuwa ameondoka kurudi Burundi. Hata hivyo, taarifa nyingine zilieleza kuwa alirejea nchini kwa kile kilichoelezwa kuwa hali ilikuwa mbaya nchini humo huku nyingine zikisema kwamba huenda alielekea Uganda kabla ya kurudi tena Dar es Salaam jioni.
Waandishi wa Mwananchi waliofika kwenye Hoteli ya Serena alikoelezwa kufikia walishuhudia ulinzi ukiwa umeimarishwa.
Radio zakatisha matangazo, ghasia mitaani
Katika mitaa mbalimbali ya Mji Mkuu wa Burundi, Bujumbura, redio zilikatisha matangazo huku vibanda vinavyopiga muziki ama vikiwa kimya au kupiga miziki kwa sauti ya chini.
Ghasia zilizuka katika mitaa mbalimbali ya Bujumbura baada ya kutangazwa mapinduzi hayo na watu 15 wameuawa na wengine 220 kujeruhiwa kwa mujibu wa Chama cha Msalaba Mwekundu.
Mashuhuda wa matukio hayo, walisema kuwa polisi wanaomtii Rais Nkurunziza waliwafyatulia risasi waandamanaji na kutumia maji ya kuwasha na mabomu ya machozi kuwatawanya watu hao waliokuwa wakielekea katikati ya jiji, hasa Ikulu ya Bujumbura.
Mapema jana asubuhi, makundi ya wanawake waliokuwa wanaipinga Serikali ya Nkurunziza walikuwa wakiandamana kwa amani kwenda katikati ya jiji la Bujumbura.
Wengine washangilia
Wakati polisi wakipambana na baadhi ya raia mitaani, maeneo mengine ya Burundi yalikuwa yakishangilia kuondolewa madarakani kwa Rais Nkurunziza.
Wakati wote wa vuguvugu hizo, wananchi walikuwa wakishangilia hatua hiyo ya jeshi kutwaa madaraka.
Baada ya kiongozi huyo wa jeshi kuzungumza kwenye redio moja binafsi kuwa utawala wa Nkurunziza umefikia kikomo, watu walilipuka kwa shangwe kupokea mamlaka hizo.
Lakini kabla ya matangazo hayo, waandamanaji walikuwa wametanda kwenye maeneo mbalimbali ya mji wa Bujumbura kutaka kujua nini kinaendelea baada ya Rais Nkurunziza kwenda Tanzania kwa mazungumzo ya suluhu ya mgogoro.
Marais EAC wapinga
Marais wa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki wamepinga mapinduzi hayo na kutoa maagizo mazito kwa Serikali ya Burundi yanayotakiwa kufanyiwa kazi ili kuhakikisha hali ya amani na usalama inarejea.
“Kutokana na hali ilivyo, uchaguzi Burundi hauwezi kufanyika, mkutano unaitaka mamlaka kuahirisha uchaguzi kwa kipindi kisichozidi muhula wa Serikali iliyopo madarakani,” alisema Rais Kikwete.
Alisema EAC itaendelea kukutana na pande zote zinazohusika na machafuko ili uchaguzi ufanyike kwa uhuru na amani.
“Jumuiya haitakubali iwapo machafuko haya yataendelea nchini Burundi. Mkutano mwingine utafanyika baada ya wiki mbili kufuatilia kinachoendelea.”
Rais Kikwete alisema walikubaliana kutuma mawaziri wa mambo ya nje wa Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda Mei 6, kwenda Burundi kufuatilia hali ya mambo ilivyo ikiwa pamoja na kufanya mazungumzo na Rais Nkurunziza.
Wengine waliohudhuria mkutano huo wa marais jana ni Makamu Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Georges Rebelo Chicoti, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Nkosazana-Dlamin Zuma na Katibu Mkuu wa EAC, Dk Richard Sezibera.
Maandamano mfululizo
Kupinduliwa kwa Rais Nkurunziza, kumekuja baada ya maandamano ya mfululizo ya wananchi wa Burundi wakipinga Rais Nkurunziza kuwania urais muhula wa tatu.
Wananchi waandamanaji walikaribia Ikulu ya nchi hiyo wakishinikiza kiongozi huyo aondoke madarakani, lakini polisi waliwatawanya kwa risasi.
Jenerali Niyombare
Hadi jana, ilikuwa haijafahamika ni kwa kiwango gani kiongozi huyo alikuwa anaungwa mkono na maofisa wa Serikali baada ya kuchukua uamuzi huo.
Awali, taarifa zilieleza kwamba Redio ya Taifa ya Burundi ilikuwa imezungukwa na Jeshi la Burundi, lakini baadaye ilielezwa kwamba ilikuwa hewani ikiendelea kutangaza vipindi vyake kama kawaida.
Jenerali Niyombare ni nani?
Alikuwa ofisa mkuu wa usalama wa zamani wa nchi hiyo na alikuwa akiheshimika katika jeshi la nchi hiyo.
Ofisa huyo pia aliwahi kuwa Balozi wa Burundi nchini Kenya na amekuwa akiheshimika katika masuala ya usalama jeshini.
Wakati mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyodumu kwa miaka 13 nchini humo na kumalizika mwaka 2006, Jenerali Niyombare alikuwa bega kwa bega katika mapigano hayo na kuunda Kundi la Waasi la CNDD-FDD baada ya Nkurunziza kuchaguliwa kuwa rais.
Baada ya kumalizika kwa vita hiyo, Jenerali Niyombare aliteuliwa kuwa naibu mkuu wa Jeshi la Burundi na baadaye ofisa mwandamizi wa Usalama wa nchi hiyo.
Ikulu Bujumbura
Wakati Jenerali Niyombare akitangaza mapinduzi hayo, Msemaji wa Ikulu ya Burundi, Willy Nyamitwe alikaririwa na BBC akisema kuwa aliyetangaza mapinduzi hayo amekimbilia msituni na sasa anasakwa ili afunguliwe mashtaka.
Alisema Rais Nkurunziza bado yuko madarakani pamoja na Serikali yake... “Jaribio la kumpindua Rais Nkurunziza limekwama na aliyehusika atachukuliwa hatua za kisheria.”
Mpaka tunakwenda mitamboni bado kulikuwa hakuna uhakika ni nani alikuwa anatawala nchi hiyo kutokana na pande zote mbili za waasi na Nkurunziza kutoa habari zinazotofautiana kuhusu mapinduzi hayo.

No comments:

Post a Comment