Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Ni dhahiri kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kimeingiwa hofu inayokifanya kishindwe kutangaza mchakato na ratiba za
vikao vya uteuzi wa wagombea wake wakiwamo wa urais na ubunge katika
Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu,
Kufikiwa kwa hatua kama hiyo kwa vyama vikubwa vya upinzani nchini,
kunaifanya CCM ibaki njia panda, hali iliyo tofauti na nyakati kama
hizi katika kuelekea chaguzi zilizofanyika hususani zikihusisha vyama
vingi tangu kuanzia 1995.
Taarifa za uhakika zilizothibitishwa na vyanzo tofauti ndani ya CCM
(majina tunayahifadhi) zilieleza kuwa, hali ilivyo mwaka huu kwa chama
hicho inachangiwa na sababu tofauti, ikiwamo mkakati wa `kuwatosa’
wagombea wasiokubalika kwa baadhi ya viongozi na `kuwabeba’ wasiokuwa na
mvuto kwa wapiga kura.
“Hali hii inawafanya (viongozi) washindwe kutimiza wajibu wao
katika kutoa ratiba na kutangaza mchakato wenye kutoa taarifa na uhuru
kwa wanachama wake kuchukua fomu za uteuzi,” kilieleza chanzo chetu.
Tangu mwaka 1995, CCM imekuwa ikitangaza mchakato na ratiba za kura
za maoni na kuwapata wagombea kabla ya vyama vya upinzani, hali
iliyovifanya vyama vya upinzani kutoa fursa kwa baadhi ya walioshindwa
katika kura za maoni (za CCM) kugombea nafasi tofauti kupitia vyama
hivyo.
ADHABU KWA MAKADA
Wakati CCM ikiendelea kuwa kimya kuhusu mchakato na ratiba ya kura
za maoni kuwapata wagombea wake, hatma ya adhabu ya makada sita
waliokuwa wakichunguzwa kwa tuhuma za kufanya kampeni zenye mwelekeo wa
kukigawa chama, haijajulikana.
Makada hao walipewa adhabu ya kuchunguzwa mienendo yao kwa kipindi
cha mwaka mmoja. Kimahesabu, adhabu hizo zilipaswa kufikia ukomo wake
Februari 18, mwaka huu.
Waliokuwa kwenye orodha hiyo ni Bernard Membe (Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa), Edward Lowassa (Mbunge wa Monduli na
Waziri Mkuu wa Zamani), Frederick Sumaye (Waziri Mkuu mstaafu), William
Ngeleja (Mbunge wa Sengerema).
Makada wengine waliokumbwa na adhabu hiyo ni Steven Wasira (Waziri
wa Kilimo, Chakula na Ushirika) na January Makamba (Naibu Waziri wa
Sayansi na Teknolojia).
“Kwa chama kikongwe kama CCM kushindwa kusema kama adhabu ya miezi
12 imekwisha au la, ni ishara ya kutokuwapo uthubutu na dalili za hofu
inayokiangamiza chama hicho,” alieleza mmoja wa wachambuzi wa masuala ya
siasa.
Jitihada za NIPASHE kumpata Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana
na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye, kuzungumzia
hali hiyo hazikuzaa matunda jana kwani simu zao hazikuwa hewani.
Hata hivyo, Ofisa mmoja katika ofisi ndogo za chama hicho, Lumumba
jijini Dar es Salaam, alisema kuchelewa kwa mchakato na ratiba hiyo ni
sehemu ya utekelezaji wa mfumo wa utendaji kazi ndani ya CCM.
Ofisa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa vile si msemaji
rasmi wa CCM, alisema kimsingi mgombea urais kupitia CCM alipaswa
kufahamika jana na leo angetangazwa rasmi kwa umma.
Kwa mujibu wa ofisa huyo, CCM haijutii pale vyama vya upinzani
vinapotangaza ratiba na mchakato wa kura za maoni kabla yake (CCM).
“Kwa vile sisi tulikuwa na utaratibu wa kuanza kabla yao
(wapinzani) na sasa tupo katika utendaji wa kawaida, wao wanapotangaza
kabla yetu (CCM) linakuwa jambo jipya, lakini kila taasisi ina mfumo wa
utendaji kazi wake,“ alisema.
Ofisa huyo alisema CCM imefanya mageuzi makubwa katika mfumo wa uteuzi wa wagombea wake mwaka huu ikiwamo kwa nafasi ya urais.
Bila kutaka kuingia kwa undani, alisema mageuzi hayo yanayoweza kuwa na changamoto zake.
Tayari kumekuwa na mapendekezo kadhaa juu ya mfumo unaofaa wa kura ya maoni ndani ya CCM hasa kuhusu nafasi za ubunge.
Wakati wa Mkutano wa Bunge uliopita, wabunge wa CCM walijadili
pamoja na mambo mengine, mapandekezo mapya ya mfumo wa kura ya maoni wa
kuwa na wagombea watatu tu watakaopigiwa kura na mkutano mkuu wa jimbo
baada ya majina ya waombaji wote kuchujwa na chama ngazi husika.
Kadhalika, kulikuwa na pendekezo la kutaka wabunge ambao
wamethibitika kutekeleza ilani ya CCM kwa ufanisi unaotosheleza, wasiwe
na wapinzani ndani ya chama na wapitishwe kuwania tena nafasi hizo kama
bado wanataka kugombea.
Mikakati hii mipya inaelezwa kuwa inachukuliwa na CCM ili pamoja na
mambo mengine, kuzuia uwezekano wa kupoteza majimbo kwa sababu tu ya
watu kutoridhishwa na matokeo ya kura ya maoni, hali ambayo kwa miaka
mingi imesababisha walionyanganywa ushindi kuhamia upinzani na kushinda.
Pia inachukuliwa kama tiba ya kukabiliana na matumizi ya fedha (rushwa) katika uchaguzi huo.
Hata hivyo, kuna taarifa kwamba CCM inavuta pumzi kutoa ratiba
kamili ya uteuzi wa wagombea ili kuondoa kila uwezekano kwa wale
watakaoshindwa au kuwekewa mizengwe kwenye nafasi ya urais kukimbilia
upinzani.
No comments:
Post a Comment