Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira.
Zaidi ya malori 50 yenye shehena za magunia ya
mahindi yaliyokuwa yakisafirishwa kwenda nchini Kenya, yamekwama kwa
zaidi ya siku tatu sasa katika mpaka wa Sirari na kusababisha
msongamano mkubwa katika barabara kuu.
Kitendo hicho kimelazimisha baadhi ya malori hayo kushusha shehena
za nafaka hizo na kuvushwa kimagendo kupitia njia za panya kwenda Kenya
na kuisababishia Serikali ya Tanzania kukosa mapato yake.
Hali hiyo imeelezwa kuwa inachangiwa na urasimu na migogoro ya
kiutendaji ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara eneo la Sirari,
kuwapo kwa mawakala wawili wanaotoza ushuru wa mazao na uwapo wa maofisa
wa kilimo katika kituo hicho kwa zaidi ya miaka 10.
Kutokana na hali hiyo, wafanyabiashara wa mikoa ya Kanda ya Ziwa na
wananchi wilayani Tarime, wamemuomba Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Steven Wasira (pichani), kuwaondoa maofisa kilimo waliohudumu
katika kituo hicho kwa zaidi ya miaka 10 kwa madai kwamba wanachangia
kuzorota kwa makusanyo ya mapato katika kituo hicho ambapo hufanya kazi
kwa mazoea.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika mji mdogo wa Sirari
juzi, baadhi ya wafanyabiashara wanaosafirisha nafaka walidai kuwa
malori hayo yenye shehena ya magunia ya mahindi yamekwama kuvuka mpaka
kwenda Kenya licha ya kuwa na leseni na vibali vya kusafirishia nafaka
hizo.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Gimonge Nyagwisi, alisema hali hiyo
inachangiwa na baadhi ya maofisa Idara ya Kilimo katika kituo cha
Forodha Sirari, kuhudumu hapo kwa zaidi ya miaka 15.
Mbali ya Nyagwisi, baadhi ya wafanyabiashara waliozungumza na
NIPASHE kuhusu suala hilo ni Nyamorea Ndera, Samwel Sabai, John Kisiri,
Mabula Makoye, Mushi Alex, Joyce John, Onyango Okelo, Thomas Andrew,
Mashimba Madoho, Matiko Lameck na Yakobo Masafa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Athuman
Akalama, alipotafutwa ofisini kwake na kwa njia ya simu, kuzungumzia
suala hilo, hakupatikana.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Beredia Balozi, alisema yeye
si msemaji na kueleza kwamba bosi wake amesafiri kikazi kwa takriban
mwezi mmoja sasa.
No comments:
Post a Comment