Wagombea urais CCM watoa zaidi ya Sh300 milioni kwenye harambee Zanzibar
Zanzibar. Hatimaye makada wa CCM wanaotajwa
kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano, juzi walipata nafasi ya
kutunishiana misuli baada ya kualikwa kuchangia mfuko wa maendeleo wa
mkoa mpya wa CCM wa Magharibi visiwani hapa.
Edward Lowassa, Mizengo Pinda, Bernard Membe,
Makongoro Nyerere, Mark Mwandosya na Steven Wasira walishiriki kwenye
hafla hiyo na kuchangia zaidi ya nusu ya fedha zilizokusanywa juzi kwa
ahadi, hundi na taslimu kwenye harambee hiyo iliyofanyika Hoteli ya
Zanzibar Beach Resort mjini hapa.
Hata hivyo, pamoja na cheche za makada hao
kuonekana visiwani hapa, Ni Waziri Mkuu Pinda aliyehudhuria harambee
hiyo iliyokusanya jumla ya Sh644.54 milioni na ambayo Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein alikuwa mgeni rasmi.
Waziri Pinda ndiye aliyetia fora kwenye hafla hiyo
baada ya yeye na marafiki zake kuchangia jumla ya Sh203 milioni, wakati
Lowassa, Membe, Wasira, Dk Shein, Mwandosya, Makongoro, Shamsi Vuai
Nahodha na Amina Salum Ali walichangia jumla ya Sh101.5 milioni.
Makada hao hawakukutana kwa bahati mbaya kwenye hafla hiyo.
“Tuliwapelekea mwaliko maalumu wote waliotangaza
nia ya kugombea urais,” alisema mratibu wa shughuli hiyo, Naibu Waziri
wa Afya Mahmoud Thabit Kombo kabla ya harambee kuanza.
Kombo alisema si vyema kwa wanachama wa CCM
kubaguana wakati viongozi wakuu wa nchi hawajambagua mtu kwa sababu ya
makundi ya wagombea uongozi.
“Wagombea wote 22 wanajua atapita mgombea mmoja
wao na wengi watakosa. Tujenge chama, sioni sababu ya watu kubaguana
wenyewe kwa wenyewe kwa sababu ya makundi ya wagombea (urais),” alisema
Kombo.
Akitoa neno la shukrani, Rais Dk Shein
aliwashukuru wote waliojitokeza kuchangia hafla hiyo na kuwataka
wanachama wa CCM kuendelea kujenga utamaduni wa kujitolea katika
uimarishaji wa shughuli za kichama, hasa wakati huu wa kuelekea Uchaguzi
Mkuu.
“Nilikuwa na uhakika wakati nilipotoa rai kwa
viongozi wa CCM tarehe 24 Aprili, 2013 kufanya harambee kuchangia
maendeleo ya chama hicho kuwa kazi hiyo itafanikiwa,” alisema Rais
Shein.
Kati ya fedha zilizokusanywa, Sh120.7 milioni
zilikuwa fedha taslimu, wakati ahadi zilikuwa Sh490.8 milioni na hundi
Sh33 milioni.
Katika hafla hiyo vitu mbalimbali vya asili pamoja
na picha za kumbukumbu za kitaifa, ikiwamo picha ya kuchora ya Rais Dk
Shein ambayo ilinunuliwa kwa Sh23 milioni.
Katika hafla hiyo, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye
aliwakilishwa na waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu wa SMZ, Machano
Othman Said, alikabidhi mchango wa Sh50 milioni, na kuibua shangwe na
nderemo mara baada ya kutajwa kwa mchango huo.
Akitoa salamu za Lowassa, Waziri Machano alieleza
kuwa mbunge huyo wa Monduli alikuwa safarini nje ya nchi, lakini
ameguswa na shughuli hiyo na kuamua kutoa kiwango hicho cha fedha ili
kusaidia mfuko wa maendeleo wa mkoa huo mpya.
“Mwenyewe hayupo lakini ameniagiza kuwa anachangia
Sh50 milioni, kwa ajili ya kutunisha mfuko huu maendeleo,” alisema
Waziri Machano huku akishangiliwa na umati wa wanachama wa CCM
waliojitokeza katika harambee hiyo.
Wakati waalikwa wakitafakari mchango huo, mratibu
wa shughuli hiyo, Mahmoud Thabit Kombo alitangaza mchango wa fedha
taslimu wa Sh10 milioni 10 kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Katika mnada wa picha, marafiki wa Waziri Pinda
walitangaza Sh10 milioni kwa ajili ya kununulia mojawapo ya picha
zilizokuwa zikinadiwa, kabla ya mwenyewe kuongeza Sh10 milioni na
marafiki hao kuongezea tena Sh3 milioni na kufanya thamani ya picha hiyo
kufikia milioni 23.
Aidha, marafiki hao wa Pinda, ambaye pia ni
miongoni mwa makada wa CCM waliotangaza nia ya kuwania urais wa Jamhuri
ya Muungano, pia walichangia zaidi ya Sh180 milioni na kufanya jumla ya
fedha zilizotoka kwa mtendaji huyo mkuu wa Serikali na marafiki zake
kufikia Sh203 milioni, akimpiku Lowassa.
Kiongozi mwingine anayetajwa kuwania nafasi hiyo
ya urais, Makongoro alichangia Sh10 milioni na kuahidi mchango wa Sh1
milioni kutoka kwa wabunge saba wa CCM waliopo Bunge la Afrika
Mashariki, ambako yeye ni mwenyekiti wa wabunge hao kati ya tisa kutoka
Tanzania.
Wasira, ambaye ni Waziri wa Kilimo na Ushirika,
alitoa mchango wa Sh5 milioni, sawa na Waziri Kiongozi wa zamani, Shamsi
Vuai Nahodha, na Kamishna wa AU katika Umoja wa Mataifa, Amina Salum
Ali.
Profesa Mwandosya, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais-Kazi Maalum, alichangia Sh1.5 milioni.
Katika hafla hiyo, Dk Ali Mohamed Shein alichangia
Sh15 milioni na mkewe, Mwanamwema Shein alichangia Sh5 milioni, Kampuni
ya Ujenzi ya Mecco (Sh20 milioni), Kampuni ya Simon Group (Sh30
milioni), na Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Asha Suleiman
Iddi (Sh2 milioni).
Hata hivyo, Mawaziri Benard Membe, Professa Mark
Mwandosya, Stephen Wassira, Edward Lowassa hawakuwepo katika harambee
hiyo ingawa walitoa michango hiyo baada ya kupewa barua za maombi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Pinda
alisema ari iliyoonyeshwa katika harambee hiyo inadhihirisha msemo wa
“kutoa ni moyo si utajiri”.Alisifu ari ya washiriki wa hafla hiyo na kueleza kuwa ilikuwa ya hali
ya juu na yeye binafsi ametiwa moyo sana na kitendo hicho cha wana CCM.
No comments:
Post a Comment