Saturday, 2 May 2015

Meli ‘ya Tanzania’yakutwa na tani 3 za cocaine Uingereza






Kiwango cha uzito wa shehena hiyo kimeweka rekodi nchini Tanzania
London, Uingereza. Kwa mara nyingine, Jina la nchi limeendelea kuchafuka baada ya Meli ya MV Hamal iliyosajiliwa Tanzania kukamatwa barani Ulaya ikiwa imebeba shehena ya dawa za kulevya aina ya cocaine yenye uzito wa tani tatu.
Kama dawa hizo haramu zingeuzwa mitaani nchini Uingereza, zingekuwa na thamani ya Sh1.5 trilioni, kiasi ambacho nchi wafadhili zinatarajiwa kuichangia Tanzania kwenye bajeti ya mwaka 2015/16.
Matukio mengine yaliyoichagua nchi ni la meli ya mizigo ya Gold Star iliyosajiliwa Tanzania ambayo ilikamatwa Septemba 2013, jirani na Kisiwa cha Sicilia katika Bahari ya Mediterranian nchini Italia wakati ikielekea Uturuki ikiwa na tani 30 za dawa za kulevya aina ya bangi zenye thamani ya Pauni 50 milioni za Uingereza (sawa na Sh125 bilioni). Tukio jingine ni lile la Watanzania wawili kukamatwa na dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 150 na thamani ya Sh6 bilioni kwenye Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo, Afrika Kusini.
Kiwango hicho cha dawa zilizokamatwa kimeweka rekodi ya ukubwa wa mzigo wa dawa hizo haramu nchini Uingereza. Awali shehena ya cocaine iliyokuwa kubwa ilikamatwa Septemba mwaka jana ikiwa na mzigo wenye thamani ya Sh450 bilioni.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uingereza, meli ya MV Hamal ilikamatwa kwenye Bahari ya Kaskazini na baada ya kupekuliwa kwenye bandari ya Arberdeen nchini Scotland, ilikutwa na shehena ya dawa za kulevya aina ya cocaine.
Meli hiyo yenye urefu wa mita 32 na uwezo wa kubeba tani 422, ilikamatwa na askari wa kikosi cha majini cha Royal Navy waliokuwa kwenye meli ya HMS Somerset pamoja na askari wa uhamiaji wa Border Force waliokuwa kwenye meli ya Valiant, karibu kilomita 160 mashariki mwa mji wa Aberdeen Alhamisi baada ya kupewa taarifa na kitengo cha makosa ya jinai, NCA.
Baadaye, meli hiyo ilipelekwa bandari ya Aberdeen, ambako maofisa wa Border Force wenye stadi maalumu ya upekuzi, waliipekua meli hiyo kwa kusaidiana na polisi wa Scotland.
John McGowan – afisa mwandamizi wa uchunguzi wa NCA, alisema: “Upekuzi wa meli ulikuwa mrefu na unaosababisha maumivu, na uliofanywa na watu wenye utalaamu mkubwa wa kufanya kazi kwenye mazingira magumu.
“Matokeo yake ni ugunduzi huu mkubwa – unaoaminika kuwa mkubwa kuwahi kutokea kwenye rekodi nchini Uingereza na ambao unaweza kuwa na thamani ya mamilioni ya fedha.”
Hata hivyo, rekodi za mtandao wa shughuli za baharini unaonyesha kuwa katikati ya Februari, meli hiyo ilikuwa Uturuki na wiki mbili zilizopita ilianza safari kutoka visiwa vya Tenerife nchini Hispania na ilipokamatwa ilikuwa inaelekea Hamburg, mji wa pili kwa ukubwa nchini Ujerumani ikitazamiwa kufika jana usiku.
Meli hiyo imekutwa na watu tisa wenye umri kati ya miaka 26 na 63 wote raia wa Uturuki na wameshitakiwa kwa kukutwa na dawa za kulevya. Washitakiwa wote hawakusema lolote waliposomewa mashtaka yao. Washitakiwa hao ni Mustafa Ceviz, 54, Ibrahim Dag, 47, Mumin Sahin, 45, Muhammet Seckin, 26, Umit Colakel, 38, Kayacan Dalgakiran, 63 na Emin Ozmen, 50, wote wanatoka jiji la Istanbul. Wengine ni Abdulkadir Cirik, 31, anayetoka Mersin na Mustafa Guven, 47, kutoka Yozgat, nchini Uturuki. Walifikishwa mahakamani Jumatatu.
Balozi wa Tanzania azungumza
Akizungumza na gazeti hili, balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Peter Kallaghe alisema nao wamezisoma taarifa hizo kwenye vyombo vya habari, lakini licha ya kutokuwa taarifa rasmi kwao waliifanyia kazi kwa kuwasiliana na mamlaka husika nchini.
Alisema ni kweli meli hiyo ina usajili wa Tanzania, lakini taarifa walizozipata toka mamlaka husika zinaonyesha mkataba wa usajili wa meli hiyo ulimalizika mwaka jana, lakini wamiliki wa meli ama kwa ujanja au kwa sababu wanazozijua waliendelea kutumia usajili huo.
Balozi Kallaghe alisema pamoja na kwamba suala hilo tayari liko mahakamani, wao wanaendelea na uchunguzi kuweza kubaini ukweli kuhusu meli hiyo kuendelea kutumia usajili wa Tanzania.
Nzowa anena
Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Kuzuia Dawa za kulevya , Kamanda Godfrey Nzowa alikiri kuwapo na tukio hilo na usajili wa meli hiyo kuwa Tanzania, lakini alisema hakuna Mtanzania yoyote aliyekamatwa zaidi ya Waturuki tisa.
Aliongeza kuwa, wao kama kitengo cha kupambana na kuzuia dawa hizo wameshaanza taratibu za uchunguzi wakishikiana na Shirika la Polisi la Kimataifa (intepol) ili kubaini ukweli wa tukio hilo ambalo halijawahi kutokea nchini humo.
Hili ni tukio la pili kubwa la Tanzania kuchafuliwa kimataifa kwa meli kukamatwa na dawa za kulevya ambapo Septemba 2013 meli ya mizigo ya Gold Star iliyosajiliwa nchini ilikamatwa ikiwa na tani 30 za dawa za kulevya aina ya bangi zenye thamani ya Pauni za Uingereza 50 milioni (Sh125 bilioni).
Meli hiyo ya mizigo ilikamatwa jirani na Kisiwa cha Sicilia katika Bahari ya Mediterranian nchini Italia wakati ikielekea Uturuki. Maofisa wa polisi nchini humo walidai kuwa watuhumiwa tisa waliokamatwa ni raia wa Misri na Syria.
Tukio hilo limetokea miezi miwili baada ya Watanzania wawili kukamatwa na dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 150 na thamani ya Sh6 bilioni kwenye Uwanja wa Oliver Tambo, Afrika Kusini.
Siku za karibuni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema kwenye hotuba yake ya kuahirisha Mkutano wa 12 wa Bunge kuwa kumekuwa na changamoto ya uharakishaji wa mashauri ya dawa za kulevya, hali inayoifanya Serikali kufikia hatua ya kufikiria kuwa na mahakama maalumu.
“Nina imani tukijipanga vizuri inawezekana. Iko hoja kwamba, labda tutafika mahala tufikirie kuwepo na mahakama maalumu ya dawa za kulevya ambayo itakuwa na kazi moja tu ya kusimamia mashauri yanayohusu dawa za kulevya,” alisema.
Waziri Pinda alisema kati ya mwaka 2010 hadi Julai, 2013, mashauri 368 yanayohusu dawa za kulevya yalipelekwa mahakamani, kati ya hayo, 91 yalimalizika kwa watuhumiwa kufungwa na wengine kutozwa faini.

No comments:

Post a Comment