Wednesday, 13 May 2015
Mbaroni kwa ‘utapeli’ akijifanya mkuu CCP
JESHI la Polisi mkoani Kilimanjaro linamshikilia mkazi wa eneo la Mwakilyambiti, kijiji cha Hungumalwa, wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, Joseph Maliuta (27) kwa tuhuma za kujipatia Sh milioni 11 kwa wizi wa mtandao baada ya kujiita Mkuu wa Chuo cha Polisi Moshi (CCP), Matanga Mbushi.
Mtuhumiwa huyo alifanikiwa kuiba fedha hizo kupitia mitandao ya simu za mkononi baada ya kuwarubuni wakazi wa kijiji cha Hungumalwa kwamba angewasaidia kuwapa nafasi watoto wao kujiunga na chuo cha Polisi Moshi.
Kamanda wa Polisi wa Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani alisema tukio hilo lilitokea Mei 8 majira ya saa mchana katika kijiji hicho baada ya mtuhumiwa kusajili jina la mkuu wa chuo hicho katika simu yake kupitia huduma za kifedha.
Alisema mtuhumiwa alimfuata mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Ngeleja Shusha (42) na kumuuliza iwapo anahitaji kusaidia mtoto wake kuingia katika chuo cha Polisi Moshi, jambo ambalo mkazi huyo alikubali anahitaji msaada huo.
“Baada ya mazungumzo, Shusha ambaye ni mfanyabiashara, alisema ana watoto watatu wanaohitaji kuingia chuo cha Polisi ambapo wa kike ni mmoja na wa kiume wawili, ambapo alitakiwa kutangaza neema hiyo kwa wanakijiji wengine,” alisema.
Pamoja na Shusha lakini pia mtuhumiwa huyo alimtaka mkazi huyo kutafuta watu wengine wenye mahitaji kama yake ili waweze kusaidia watoto wao kujiunga na chuo cha Polisi kwa malipo ya Sh 250,000 kwa kila mtoto jambo ambalo lilitekelezwa na wanakijiji hao.
Alisema kutoka na udanganyifu huo, mkazi huyo alifanikiwa kukusanya kiasi cha Sh milioni 11 ambazo zote zilitumwa kwa mtuhumiwa ili aweze kutoa msaada waliohitaji.
Kamanda Ngonyani alisema baada ya Polisi kutapa taarifa za kufanyika kwa wizi huo iliweka mtego ambao ulisaidia kumnasa mtuhumiwa ambaye tayari amefikishwa mjini Moshi ili kufanyika kwa uchunguzi ili baadaye afikishwe mahakamani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment