Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (kushoto) akichangia bungeni mjadala wa kupitisha bajeti ya Ofisi ya Rais , Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Utawara Bora na Uhusianao na Uratibu kwa mwaka wa fedha 2015/2016, mjini Dodoma jana.
Dodoma. Mjadala wa bajeti mwaka 2015/16
umegeuka mwiba mchungu kwa Ofisi ya Rais baada ya mawaziri watatu
waliopo katika ofisi hiyo kubanwa na wabunge wa upinzani hasa wale
wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wakisema “njaa imeanzia
Ikulu na Ofisi ya Rais inayosimamia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru) haina utashi wa kupambana na rushwa.”
Mawaziri hao jana walitakiwa kueleza sababu za
ofisi hiyo kushindwa kutokomeza rushwa, mikakati ya Serikali kuiwezesha
Takukuru na kuipa meno ya kuwashtaki moja kwa moja watuhumiwa wa rushwa.
Kambi hiyo imeilipua Taasisi ya Wanawake na
Maendeleo (Wama) inayoongozwa na mke wa Rais, mama Salma Kikwete
wakitaka ifutwe kwa maelezo kuwa imekiuka sheria za nchi.
Katika mjadala huo, Mbunge wa Muhambwe
(NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali aliibua malumbano makali kati yake na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika na
Mwenyekiti wa Bunge, Lediana Mng’ong’o, baada ya kudai kuwa Ikulu na
Serikali ya Awamu ya Nne imeshindwa kupambana na rushwa licha ya kuwa
chini ya Rais.
Alivyochafua hali ya hewa
Katika mjadala huo, Mkosamali alihoji; “kama
Takukuru, Mkurabita na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (Tasaf) ziko
chini ya Ofisi ya Rais na bado zinalia njaa, kwa nini watumishi wa umma
kama wauguzi na walimu wawe chini ya ofisi hii badala ya kuwa katika
Ofisi ya Waziri Mkuu au Tamisemi?
“Yaani njaa imeanzia Ikulu. Tumeiweka Takukuru
Ikulu tukidhani kuwa Rais ataweza kupambana na rushwa, sasa ukiona
taasisi hiyo imefeli tambua kuwa Rais hana utashi wa kisiasa wa
kupambana na rushwa
“Watu wanajua Takukuru ikiwatuhumu katika kesi
kubwa zitafutwa. Taasisi hii kufeli kufanya kazi maana yake ni kuwa
Serikali imefeli katika miaka yote minane, hata Rais hakuwa na nia ya
kupambana na rushwa,” alisema na kusisitiza jinsi Bunge la Katiba
lilivyoshindwa kuipa meno Takukuru kupitia Katiba Inayopendekezwa.
Alihoji, “Tasaf wameomba Sh18 bilioni mwaka jana
na mpaka sasa wamepewa Sh3 bilioni na sasa hivi mnaomba tena mabilioni
ya shilingi. Hivi mnataka wakurugenzi wa Tasaf na wafanyakazi
wawachukuliaje?”
Alihoji taasisi zilizopo chini ya Ofisi ya Rais
kutopewa fedha za bajeti kama ilivyoidhinishwa mwaka jana na kusema
kitendo cha mwaka huu wizara tatu za Ofisi ya Rais kuja na bajeti
nyingine wakiomba mabilioni ya fedha ni fedheha.
“Kama taasisi zilizopo Ikulu zina njaa, hivi
nyinyi huko katika halmashauri si ndiyo mtakufa! Rais ambaye taasisi
hizi zipo ofisini kwake anashindwa kuzihudumia atawakumbuka watu wa
Kibondo? Hii Serikali imechoka kabisa na imechakaa,” alisema.
Kauli hiyo ilimnyanyua Mkuchika na kuomba kutoa
taarifa, jambo ambalo lilipingwa na Mkosamali akidai kuwa awali aliomba
kutoa taarifa kwa mwenyekiti na kunyimwa.
“Mwenyekiti usiendeshe Bunge namna hii, nieleze umetumia kanuni
gani ya kunizuia nisitoe taarifa na kumruhusu Mkuchika. Umetumia kifungu
kipi, kwani huyu (Mkuchika) si mbunge kama mimi,” alihoji Mkosamali na
kujibiwa na Mng’ong’o kuwa Mkuchika ni waziri.
Huku akiwa amesimama, Mkosamali aliendelea kuzungumza licha ya kuzimiwa kipaza sauti.
Katika taarifa yake Mkuchika alisoma Kanuni ya ya
Bunge 64 (d) inayosema; Hatatumia jina la Rais kwa dhihaka katika
mjadala au kwa madhumuni ya kutaka kulishawishi Bunge kuamua jambo
lolote kwa namna fulani.
“Mkosamali wakati anachangia ameeleza Rais hana
nia ya kupambana na rushwa. Namtaka afute kauli hiyo kwa sababu
amekwenda kinyume na kanuni za majadiliano. Ila mchana nikimjibu
nitamweleza alichokifanya Rais katika kupambana na rushwa,” alisema
Mkuchika.
Taarifa hiyo ilikataliwa na Mkosamali akisema:
“Nitafutaje wakati ndiyo hali halisi. Juzi, Katibu Mkuu Kiongozi (Balozi
Ombeni) Sefue kawasafisha wala rushwa. Kesi kubwa zote mmezifuta na
suala la kuiongezea meno Takukuru lililokuwa katika rasimu ya (Jaji
Joseph) Warioba mmeshindwa kuliweka katika Katiba Inayopendekezwa.”
Licha ya kutakiwa na Mng’ong’o kufuta kauli ya
‘Rais kashindwa kupambana na rushwa’, Mkosamali alisisitiza, “Nimesema
Takukuru wakituhumu kesi 4,000 wanashinda kesi 40 hadi 50, sasa huo ni
uongo, kweli wana nia ya kupambana na rushwa?”
Wabunge wasisitiza
Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Karagwe (CCM),
Gosbert Blandes alisema Sheria ya Kupambana na Rushwa inatakiwa
kubadilishwa ili kuiwezesha Takukuru kumshtaki moja kwa moja mtuhumiwa
wa rushwa, badala ya kumchunguza tu na kupeleka faili kwa DPP.
Mbunge wa Tarime (CCM), Nyambari Nyangwine
alisema: “Takukuru inatakiwa ipewe fedha kwa wakati na watumishi wa
kutosha ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Tunatakiwa tuwe na
sheria kali ili watakaokamatwa kwa rushwa wanyongwe au kupigwa risasi
kabisa.”
Aliongeza, “Viongozi wote wanatakiwa kuchunguzwa
kwa sababu wanapata maendeleo ndani ya muda mfupi tangu kuwa viongozi,
iweje ndani ya mwaka tu mtu awe na nyumba ya ghorofa na magari?”
Mbunge wa Manyoni Mashariki (CCM), John Chiligati
alisema: “Rushwa imekithiri kwa kiasi kikubwa ninaitaka Serikali ieleze
kwa nini haichunguzi mali za viongozi. Wapo viongozi wanaotumia ofisi za
umma kwa masilahi yao binafsi kwani ndani ya muda mfupi wanakuwa
matajiri wa kutupwa.”
Wama yalipuliwa
“Vibali vya ajira mpya 58,483 kati ya 68,138 vilivyoidhinishwa katika bajeti ya 2014/2015 vilitolewa,” alisema.
Alisema mwaka 2015/2016 Serikali inatarajia
kuajiri watumishi wapya 71,496 na kipaumbele kitakuwa katika sekta za
elimu, afya, kilimo na mifugo.
Majibu
Akijibu hoja za wabunge hao, Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya alimshutumu mmoja wa
kiongozi wa upinzani kwa kushindwa kuwa mzalendo.
Alisema kiongozi huyo akiwa Marekani, alieleza kuwa Tanzania imekuwa ikikiuka haki za binadamu kwa kuwapiga wapinzani.
Alisema kiongozi huyo alipigiwa makofi bila
kufahamu waliokuwa wakifanya hivyo walikuwa wakimshangaa kwa kitendo
chake cha kutokuwa mzalendo kwa nchi yake.
Alisema kiongozi huyo alifika mbali na kusema kuwa
wataleta wanasheria na kuipeleka Serikali katika Mahakama ya Kimataifa
ya Makosa ya Jinai ya The Hague.
“Huwezi kumkuta Mmarekani akiisemea vibaya nchi
yake na hii ni kwa nchi yoyote duniani. Mimi niliposikia nilishangaa
kwelikweli,” alisema.
Aliwaomba wabunge wa upinzani kumpa heshima yake Rais na kuacha kumzungumza kama wanavyomzungumzia mbunge mwingine.
“Huwezi kumzungumzia Rais kama unavyomzungumzia
Mbunge wa Rungwe. Mimi mnaweza kuzungumza hata mkitaka kunitukana sawa,
lakini mnapomzunguzia Rais lazima tuseme,” alisema.
Profesa Mwandosya alitumia fursa hiyo kuaga
akisema hatagombea tena ubunge katika Uchaguzi Mkuu... “Miaka 15
niliyopita bila kupingwa inatosha labda unaweza kuwa ndiyo mwanzo wa
kulitumikia Taifa katika ngazi nyingine,” alisema.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto,
Sophia Simba alisema ni shirika lisilo la kiserikali moja tu la Sisi kwa
Sisi lililofutiwa usajili kutokana na kujihusisha na ushoga.
Kuhusu Wama alisema imesajiliwa na Brela na inaendeshwa kwa kufuata taratibu za kisheria.
Katika majibu yake, Mkuchika alisema hakuna
mkutano wowote ulioitwa na Ikulu kwa ajili ya kuwasafisha mawaziri na
viongozi waliohusika na sakata la Tegeta Escrow wala Operesheni
Tokomeza.
Juu ya Rais Kikwete kutokuwa na dhamira ya
kupambana na rushwa, alisema Rais, Serikali na chama kupitia ilani yake
ya uchaguzi wana dhamira ya dhati ya kupambana na tatizo hilo.
Alitaja mambo yanayoonyesha kuwa Serikali ina
dhamira ya dhati kuwa ni pamoja na kujenga makao makuu ya Takukuru,
kujenga ofisi saba za chombo hicho na kuongeza raslimali watu.
No comments:
Post a Comment