Bado hakuna mwafaka kuhusu hatima ya Katiba Mpya, baada ya
kuahirishwa kwa upigaji Kura ya Maoni iliyopaswa ifanyike Aprili 30
mwaka huu.
Wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na baadhi
ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakisema Kura ya Maoni itafanyika
wakati wowote mwaka huu baada ya kukamilika uandikishaji wapigakura kwa
Mfumo wa Biometric Voters’ Registration (BVR), wanaharakati na viongozi
wa vyama vya upinzani, wanaamini kuwa kuahirishwa kwa Kura ya Maoni,
kungetoa fursa ya mchakato huo kurudi kwenye Bunge la Katiba.
Wapinzani hao wanasema hili litasaidia kuondoa
tofauti zilizojitokeza wakati wa Bunge la Katiba ambako kundi hilo
lilisusa na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Hata hivyo, wapo wanaoamini pia kuwa kuahirishwa
kwa Kura ya Maoni, ndiyo mwisho wa Mchakato wa Katiba Mpya, hasa baada
ya rais aliyeanzisha mchakato huo kumaliza muda wake baada ya uchaguzi
mkuu.
Nec iliahirisha Kura ya Maoni iliyopaswa kufanyika
Aprili 30 mwaka huu kutokana na kulegalega kwa shughuli ya kuandikisha
wapigakura kwa BVR na baada ya tamko hilo giza likagubika hatima ya
mchakato mzima.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 na
mabadiliko yake yaliyofanyika mwaka 2012 na Sheria ya Kura ya Maoni ya
mwaka 2013, ziko kimya juu ya nini kinafuata baada ya kuahirishwa kwa
Kura ya Maoni.
Sheria hizo zimeeleza tu namna Mchakato wa
Mabadiliko ya Katiba unavyopaswa kuendeshwa kuanzia siku ulipotangazwa
hadi kupatikana kwa Katiba Mpya. Pia sheria zimeeleza nini kitafuata
kama kura ya NDIYO haitafika zaidi ya 50 kutoka pande zote za Muungano.
Kifungu cha 35(3) cha Sheria ya Kura ya Maoni na
Kifungu cha 36(3) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba vinasema kama kura
za ndiyo hazifiki zaidi ya nusu ya wapigakura wote Bara na Zanzibar,
Tume ya Uchaguzi Nec, na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, kwa makubaliano
maalumu na baada ya tangazo la Serikali, watachagua njia nyingine ndani
ya siku 30 tangu kutangazwa kwa matokeo hayo.
Ikifikia hapo mchakato wa upigaji Kura ya Maoni
utaanza upya. Sheria zote zimempa Rais mamlaka ya kuitisha tena Bunge la
Katiba kubadili vipengele vilivyokataliwa wakati wa upigaji kura.
Kifungu cha 35(5) cha Sheria ya Kura ya Maoni
pamoa ja na Kifungu cha 36(5) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,
vinasema, kama kura za HAPANA zitakuwa nyingi ikilinganishwa na kura ya
NDIYO, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,
itaendelea kutumika.
Vyama vya upinzani kupitia Umoja wao wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), wamekuwa wakitaka Kura ya Maoni iahirishwe ili kukaa
na kutafuta kwanza mwafaka katika baadhi ya mambo ikiwamo Muundo wa
Muungano.
Mwenyekiti mwenza wa Ukawa Ibrahim Lipumba,
amesema siyo sahihi kuendelea na mchakato wa Kura ya Maoni, kabla ya
kupitia upya maeneo yaliyoleta mpasuko kwenye Mchakato wa Katiba.
“Sisi tuligomea mchakato huo, pamoja na mambo mengine kutaka
Serikali iuahirishe ili tumalize kwanza uchaguzi mkuu, halafu ndipo
turudi kwenye Kura ya Maoni,” anasema Lipumba.
Kwa upande wake Mratibu wa Mtandano wa Kutetea
Haki za Watetezi wa Haki za Binadamu (THRD), Onesmo Olengurumwa anataka
Kura ya Maoni isifanyike mwaka huu kwa sababu ya mazingira ya kisiasa
yaliyopo.
“Serikali isijisikie kwamba imeshindwa katika
hili. Nec iachwe ifanye kazi yake na mimi naamini kuwa kwa sasa
kipaumbele cha kwanza cha Nec ni Uchaguzi Mkuu na siyo Kura ya Maoni,”
anasema na kuendelea;
“Tunahitaji mwafaka wa kitaifa kuhusu suala la
Katiba na tunaweza kufikia hatua hiyo kama wanasiasa wataamua kuwa na
akili za kuaminiana bila kuwazia namna ya kutetea nafasi zao za
kisiasa.”
Olengurumwa ambaye pia ni mwanasheria,
amependekeza mabadiliko katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Sheria
ya Kura ya Maoni ili kuwa na namna nyingine ya kushughulikia suala hilo.
“Watu wamekuwa wakilalamika kuhusu sheria hizo.
Kwanza sheria zenyewe zimevunjwa mara kadhaa sasa tuzibadili kabisa ili
tuwe na mjadala wenye afya kuhusu Katiba Mpya,” anasema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk Benson
Bana, anasema wapinzani na chama tawala CCM, wana tofauti kubwa katika
suala la Mchakato wa Mabadiko ya Katiba.
Kwa mujibu wa Dk Bana, kuahirisha tu Kura ya
Maoni, hakumaanishi kumaliza tofauti zilizopo. Bado kuna haja ya kukaa
meza moja na kujadili tofauti hizo kwa faida ya taifa, anasema.
Dk Bana anasema haoni tatizo kama Kura ya Maoni
itafanyika baada ya uchaguzi, na kwamba hofu kwamba tusipoifanya sasa
huenda isifanyike tena haina msingi.
“Katiba Mpya siyo urithi wa Rais, bali Rais ndiye anayepatikana kwa Katiba.
Hivyo Rais ajaye anaweza kuendeleza pale tulipofikia lakini hawezi kubadili wala kuusitisha mchakato wote,” anasema.
Mbunge wa Nzega, Hamis Kigwangala anasema anaona
kuna umuhimu wa wadau kukaa meza moja na kujadili tofauti zinazoonekana
kwenye Mchakato wa Katiba, ikiwamo suala la kuwa na Tume huru ya
Uchaguzi, mgombea binafsi na kupinga matokeo ya rais mahakamani.“Tunahitaji mambo haya kabla ya Uchaguzi Mkuu. Wapinzani wamekuwa
wakiyapigia kelele kwa muda mrefu sasa. Naamini tukitekeleza hayo,
Wapinzani hawatakuwa na cha kusema kama CCM itashinda,” anasema.
No comments:
Post a Comment