Wednesday, 13 May 2015

Anusurika kuuawa kwa kukataa kuidhinisha fedha

KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Endiamtu mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, amenusurika kufa kwa kushambuliwa kwa kupigwa ngumi na Mwenyekiti wake baada ya kutoidhinisha matumizi ya Sh milioni moja.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu huyo wa CCM wa Kata Salimu Mohamed Kombo alisema alipigwa na kupoteza fahamu na Mwenyekiti wake Issa Katuga aliyekuwa Diwani wa Mirerani mwaka 2000 hadi 2005.
 Kombo alisema tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki ambapo alipigwa sehemu mbalimbali za mwili, wakiwa kwenye ofisi ya CCM Kata ya Endiamtu baada ya Katuga kumtuhumu kutoidhinisha fedha ili zilipe madeni.
Alisema Mwenyekiti huyo alipendekeza fedha za mgao wa uwanja wa CCM Endiamtu, ambazo zinatokana na mnara wa Kampuni ya Airtel zitolewe ndipo wajumbe wakagoma kuziidhinisha naye akachukia na kumpa kipigo kikali.
“Mwenyekiti wangu baada ya kuona hivyo akaniita ofisini jioni na kuniuliza ndipo akaanza kunipiga vichwa, ngumi, sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo usoni, kichwani, na kunichana puani na mdomoni,” alisema Kombo.
Alisema baada ya kupigwa alipoteza fahamu na alipozinduka alibaini amepoteza fedha taslimu Sh 100,000 na simu ya mkononi aina ya Tekno ndipo akaenda Polisi kutoa taarifa na kisha akatibiwa kwenye Kituo cha Afya Mirerani.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi Christopher Fuime, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa walimshikilia Katuga kwa mahojiano kuhusiana na tukio hilo.
“Bado tunaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na mara baada ya kukamilika tunatarajia kumfikisha mahakamani wakati wowote ila Kombo alijeruhiwa kwa kuumizwa sehemu tofauti,” alisema Kamanda Fuime.
Kwa upande wake, Katuga alikanusha vikali kumpiga Kombo na kudai kuwa hawezi kumpiga Katibu wake japokuwa wamekuwa na mitazamo tofauti katika uongozi wao, inayotokana na kambi za kisiasa katika uchaguzi.
“Mara nyingi tumekuwa tunapingana kwenye vikao na Katibu wangu, lakini siwezi kumpiga nadhani maadui wangu wa kisiasa wamemchochea anituhumu hivyo japokuwa nasikia atafikisha suala hili mahakamani,” alisema Katuga.

No comments:

Post a Comment