Friday, 29 May 2015

BAJETI: Wabunge wamshukia Nyalandu

“Mheshimiwa Spika. Naomba Bunge lako tukufu likubali kupitisha makadirio ya matumizi ya jumla ya Sh81,964,541,000 kwa mwaka 2015/2016 kati ya fedha hizo, Sh74,255,391,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh7,709,150,000 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Fedha za matumizi ya kawaida zinajumuisha Sh45,235,955,000 za mishahara ya watumishi na Sh29,019,436,000 za matumizi mengineyo. Fedha za miradi ya maendeleo zinajumuisha Sh5,709,150,000 fedha za nje na Sh2,000,000,000 fedha za ndani.” Nyalandu 
  • Hotuba zote mbili, ya kamati na upinzani, zilieleza kushangazwa na kitendo cha waziri huyo kupinga watalii kulipa tozo mara moja kila wanapoingia katika Hifadhi ya Serengeti na Ziwa Manyara, badala yake kung’ang’ania walipe mara mbili, jambo ambalo ni kinyume na maelekezo ya Bunge.

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na Kambi ya Upinzani Bungeni jana waliungana kumbana Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu wakisema amelikosesha Taifa mabilioni ya shilingi.
Hotuba zote mbili, ya kamati na upinzani, zilieleza kushangazwa na kitendo cha waziri huyo kupinga watalii kulipa tozo mara moja kila wanapoingia katika Hifadhi ya Serengeti na Ziwa Manyara, badala yake kung’ang’ania walipe mara mbili, jambo ambalo ni kinyume na maelekezo ya Bunge.
Akisoma taarifa ya kamati kuhusu utekelezaji wa majukumu ya wizara hiyo, mwenyekiti wa kamati hiyo James Lembeli alisema, “Takwimu zinaonyesha kwamba tangu Julai 2014 hadi Machi 2015, hifadhi hizo mbili zilipoteza Sh1.4 bilioni kutokana na wizara kulazimisha tozo mara mbili. Kamati inahoji, kuna masilahi gani waziri kutetea mfumo ambao unaipotezea Serikali mapato?”
Alisema licha ya Bunge kuazimia Nyalandu atekeleze hukumu ya Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha iliyomtaka kutangaza katika gazeti la Serikali tozo mpya zitakazotumika katika hoteli ndani ya Hifadhi za Taifa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, hakuzingatia suala hilo.
“Kutokana na kuchelewa kuanza kutumika kwa tozo mpya kama ilivyoamriwa na Mahakama, Serikali imepoteza Sh3 bilioni hadi kufikia Machi 15, 2015. Kamati inamtaka waziri (Nyalandu) kulieleza Bunge nini kilimfanya akaidi kutekeleza hukumu iliyokuwa na masilahi kwa Taifa,” alisema Lembeli.
Msemaji wa Kambi ya Upinzani kuhusu wizara hiyo, Mchungaji Peter Msigwa alisema: “Fedha hizi Sh3 bilioni zingeweza kununulia madawati ya watoto wanaokaa chini, kununua vitanda vya wajawazito au kupunguza deni la (MSD) Bohari Kuu ya Dawa.”
Mchungaji Msigwa alisema ni aibu kwa Nyalandu ambaye ametangaza nia ya kugombea urais, kusimama na kusoma mafanikio ya wizara yake wakati amelisababishia Taifa hasara.
Katika hotuba yake, Msigwa pia aligusia ujangili wa wanyamapori na kuhoji sababu za Serikali kushikwa na kigugumizi cha kuteketeza tani 90 za shehena ya meno ya tembo yaliyohifadhiwa katika maghala baada ya kukamatwa kutoka kwa watu mbalimbali.
Msigwa pia aliibua sakata la kusafirishwa kwa wanyama hai kwenda Uarabuni akiitaka Serikali iweke hadharani majina ya watu waliohusika.
Mbunge huyo wa Iringa Mjini alisema ni wakati sasa kwa Serikali kuanika uozo huo hadharani kwa kuwa suala la kusafirishwa kwa wanyama haliko mahakamani tena kama ambavyo Serikali imekuwa ikijificha humo.
“Tunaomba majibu sasa, nani alibeba wanyama wale maana kesi haiko tena mahakamani kama ambavyo mmekuwa mkitueleza,” alisema Msigwa.
Alisema Watanzania wamechoka kudanganywa kwa maneno matamu ya kuwapumbaza, wanachotaka ni kujua jinsi rasilimali zao zinavyotumiwa vibaya.Katika hotuba yake Waziri Nyalandu aliomba kuidhinishiwa Sh81.9 bilioni kwa mwaka 2015/16, huku akieleza mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya utalii nchini na mapambano dhidi ya ujangili.
Mapema, wizara hiyo ilisema kwa kushirikiana na vyombo vya dola imeanza uchunguzi wa tukio la kupigwa risasi kwa mkazi wa Kijiji cha Bugeri, Fiay Hhawu (34), katika Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahamoud Mgimwa alisema uchunguzi huo unawashirikisha askari saba wa hifadhi hiyo ambao walikuwa katika lindo ili kubaini iwapo tukio hilo lilifanyika kwa makusudi.
“Wizara inakiri kupokea taarifa rasmi za kifo hicho na kuahidi kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini undani wa tukio hilo na wale wote watakaobainika kusababisha kifo hiki watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchini.
“Baada ya kupigwa risasi, askari walimchukua ndani ya gari kumuwahisha hospitali, lakini wanakijiji walifunga njia na hivyo kusababisha ugumu wa kupita kwenda hospitali,” alisema.
Mtu huyo alifariki akiwa njiani kupelekwa hospitali baada ya kuvuja damu nyingi.
Mgimwa alisema wizara yake imekuwa ikijitahidi kuweka mazingira mazuri kati yake na wanavijiji wanaozunguka hifadhi hizo na hivyo  wanachunguza tukio hilo kwa kina.
Majibu ya Nyalandu
Akijibu hoja hizo za kamati kwamba alikiuka maagizo ya Mahakama, Nyalandu alisema wizara yake ilitekeleza amri hiyo kwa kusaini tozo mpya kabla ya Machi kama ilivyoagizwa.
Alisema hakuna fedha zilizopotea kwa sababu Serikali iliendelea kukusanya tozo la hoteli kama kawaida tangu 2011 – 2014 wakati kesi ilipokuwa ikiendelea.
“Tutahakikisha kuwa tunapata fomula ya kukokotoa tozo katika hoteli zote zilizopo kwenye hifadhi zetu na zile zitakazojengwa siku zijazo. Nadhani hii itatusaidia kutenda haki kwa pande zote, mwekezaji na Serikali,” alisema.
Kuhusu tozo kwa watalii wanapoingia kwenye hifadhi, Nyalandu alisema Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) imekuwa na utaratibu wa kuwapa watalii saa 24 za kuwa ndani ya hifadhi. Alisema utaratibu huo uliwaruhusu kuingia na kutoka ndani ya muda huo.Kuhusu hoja ya meno ya tembo iliyotolewa na Mchungaji Msigwa, Waziri Nyalandu alisema: “Hatuna mpango wowote wa kuchoma shehena ya meno ya tembo iliyopo ghalani. Pia, Tanzania haitauza meno hayo kwa sababu tulisaini mkataba London (Uingereza) wa kutouza meno hayo.”
Akizungumzia hoja ya kusafirishwa kwa wanyama, Nyalandu alisema kulikuwa na kesi mahakamani ambako watu watano walikuwa wakituhumiwa. Alisema mtu mmoja alitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miaka 60 na wengine waliachiwa huru.

No comments:

Post a Comment