Wednesday, 6 May 2015

Timu ya kushughulikia mikataba ya gesi yatajwa.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
 
Katibu  Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue (pichani),  amezindua timu ya wataalamu 25 ambao wamechaguliwa kwa ajili ya kuwakilisha serikali katika mazungumzo yote ya mikataba na kampuni za gesi asilia.
Lengo la kuundwa kwa timu hiyo ni kuleta mikataba yenye manufaa makubwa kijamii na kiuchumi kwa ajili ya Watanzania na Taifa kwa ujumla.
Timu hiyo ambayo lengo lake pia ni kutatua masuala ya uchumi endelevu wa gesi inajumuisha wataalamu kutoka ofisi na taasisi mbalimbali kama Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Fedha, Wizara ya Kazi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na TANESCO.
 
Nyingine ni  TPDC, Tume ya Mipango, STAMICO, Ofisi ya Waziri Mkuu, Benki Kuu, TRA, Wizara ya Viwanda na Biashara, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, TAMISEMI na NEMC.
 
Akizindua timu hiyo, Balozi Sefue alisema kwamba mpango huo utawawezesha kuwapatia wataalam wa kufanya mazungumzo yenye ueledi na mafanikio kwa Taifa. 
 
  Pia aliishauri timu hiyo kujitolea kujifunza, kuelewa, kufikiria kimkakati, kusimamia, kutafiti, kuchunguza na muhimu zaidi kufanya mazungumzo vizuri kwa niaba ya serikali kwa ajili ya maslahi ya Tanzania kwa sasa na hata baadaye.
 
“Kufanya mazungumzo ya mikataba ya mafuta na gesi asilia na kampuni za kimataifa ya mafuta ni changamoto kubwa kwa serikali za nchi zilizobarikiwa na rasilimali nyingi kutoka Afrika, changamoto ambayo lazima itatuliwe,” alisema.
 
Balozi Sefue alisema kampuni za kimataifa za mafuta zina uwezo mkubwa wa kuleta wataalamu wao waliobobea katika fani za uhandisi, kiuchumi na kisheria kutoka duniani kote na wenye uzoefu wa muda mrefu.
 
 “Tayari ugunduzi wa futi za ujazo trilioni 50 za gesi asilia zinaweza na inapaswa kuleta chachu ya kufanya mageuzi ya kiuchumi katika nchi yetu ili iweze kuwa nchi endelevu yenye kipato cha kati katika miaka ya hivi karibuni. Lakini ili hii ifanyike, tunapaswa kuiga yale mazuri, kutokurudia makosa ambayo nchi zingine wamekwisha yafanya huko nyuma na pia inatubidi tufanye mazungumzo mazuri ili kupata mikataba bora,”

No comments:

Post a Comment