Timu ya soka ya Yanga.
Akizungumza na NIPASHE juzi jioni kabla ya kuondoka nchini kuelekea Sousse, nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro', alisema watashuka uwanjani kwanza wakihitaji ushindi na hatimaye kusonga mbele kwenye mashindano hayo na pia kila mmoja akitaka kuimarisha ajira yake hasa kuelekea kipindi cha usajili wa mwishoni mwa msimu.
Cannavaro alisema timu inaposhiriki mashindano ya kimataifa, ndiyo
nafasi pekee kwa wachezaji kujitangaza na hatimaye kupata mikataba mipya
ndani ya klabu au nje ya nchi endapo watawavutia mawakala watakaokuwa
wanaifuatilia mechi hiyo ya marudiano.
Beki huyo wa kati alisema wamechoka kuitwa 'wasindikizaji' wa timu
za Waarabu kwenye mashindano hayo ya kimataifa na mwaka huu wamejipanga
kuhakikisha wanapata ushindi ugenini.
"Tunajua kuwa mechi haitakuwa rahisi, lakini mkumbuke na sisi si
wasindikizaji, tumefanya mazoezi kama wao wanavyofanya, kwa uwanjani
tuko tayari kwa mchezo, kama kuna mengine nje ya uwanja hatuwezi
kuyasemea," alisema beki huyo.
Aliongeza kuwa soka la sasa limebadilika na hakuna timu
inayojiamini kwa asilimia zote kuwa itasonga mbele, hadi dakika 90 za
uwanjani zitakapomalizika hivyo wanawaomba wanachama na mashabiki wa
timu yao kuwaombea dua ili waendelee kuwapa furaha kama walivyofanikiwa
kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Naye Mrisho Ngasa alisema amejipanga kuonyesha kiwango cha juu
katika mchezo huo wa Jumamosi kwa sababu ni 'daraja' lingine la
kuelekea kwenye soka la kulipwa nje ya nchi.
Ngasa alieleza kuwa bado ana ndoto za kucheza soka nje ya Tanzania
hivyo mechi za kimataifa ndizo huamua nini hatma yake kwenye kupata
mikataba kutoka katika timu zinazomfuatilia.
"Ndio wakati wa kujitafutia maslahi, tunaenda vitani kwa kutaka
timu yetu isonge mbele lakini kila nafasi ya mchezaji inajambo lake,
nitajipigania ili niweze kujitengenezea maisha mazuri," aliongeza Ngasa
ambaye ameshacheza timu zote tatu kubwa kwenye Ligi Kuu Bara ambazo ni
Azam, Simba na Yanga anayoitumikia kwa kipindi cha pili sasa.
Kuhusiana na yeye kuichezea Yanga wakati hana mkataba na timu hiyo,
Ngasa alisema anaamini atafanya maamuzi ya wapi anaelekea kabla ya
mechi ya mwisho ya msimu huu ambayo mabingwa hao wapya watafunga pazia
kwa kuikabili Ndanda FC kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani
Mtwara.
Mshambuliaji anayeongoza kwenye safu ya ushambuliaji msimu huu,
Simon Msuva, alisema anatarajia kuifanyia 'makubwa' zaidi timu yake
katika mechi hiyo ya kimataifa kama ilivyo kwenye ligi ya nyumbani.
Msuva alisema anajua mechi hiyo ya Jumamosi itakuwa ngumu na yenye ushindani lakini hawahofii wapinzani wao.
"Mungu ni mkubwa, hakuna kisichowezekana, tunaenda Tunisia kupambana," alisema kwa kifupi Msuva.
Katika mechi ya kwanza iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini
Dar es Salaam wiki mbili zilizopita, Yanga na Etoile du Sahel zilitoka
sare ya bao 1-1 hivyo wawakilishi hao pekee wa Tanzania waliobakia
katika michuano ya kimataifa wanahitaji ushindi wowote au sare ya
kuanzia mabao 2-2 ili wasonge mbele.
Yanga imefika hatua hiyo ya 16 bora baada ya kuwaondoa BDF XI ya Botswana na Platinum FC ya Zimbabwe.
Endapo itafanikiwa kuitoa Etoile du Sahel, itasubiri kupangiwa moja
ya timu itakayotolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na
ikiitoa, itakuwa imefuzu kucheza nane bora hatua ambayo huchezwa kwa
mtindo wa ligi.
No comments:
Post a Comment