Lowassa: Ni safari ya matumaini
Makamba: Safari ya ushindi imeanza
Makamba: Safari ya ushindi imeanza
Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, wakiwa kwenye kikao cha Kamati Kuu.
Waliofutiwa adhabu ni mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na
Frederick Sumaye, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira,
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, aliwaambia
waandishi wa habari jana, mara baada ya kikao hicho kumalizika na
kufikia uamuzi huo.
"Adhabu hiyo kwa sasa imemalizika na wanachama hao wameruhusiwa kuendelea na shughuli zao katika chama," alisema Nape.
Hata hivyo, CC imewataka wanachama hao na watu wengine wenye nia ya
kugombea urais kupitia CCM kuzisoma, kuziheshimu na kuzizingatia kanuni
za maadili ya chama na kanuni zingine zinazoongoza mchakato huo ili
wasikumbwe na adhabu ya kuzivunja kanuni hizo.
Alisema Kamati Kuu ilipokea na kutafakari taarifa ya Kamati ya
Usalama na Maadili ambayo ilipitia adhabu waliyopewa wanachama hao
waliokiuka kanuni za maadili iliyodumu kwa kipindi kisichopungua miezi
12 na kupewa onyo kali.
Adhabu yao ilianza tangu Februari 18, mwaka jana na ilitarajiwa
kumalizika Februa 18, mwaka huu. Hata hivyo, Februari 28, mwaka huu
Kamati hiyo ilikutana na kusema adhabu bado inaendelea.
Maamuzi ya kamati hiyo, yamekuja baada ya kutafakari taarifa ya Kamati ya Maadili iliyokutana mapema jana.
KIKAO CHA DHARURA
Kabla ya maamuzi ya Kamati Kuu, kilifanyika kikao cha dharura
ambacho kiliwahusisha vigogo wa juu wa chama hicho, hatua iliyofanya
kikao cha CCM kuahirishwa hadi jioni jana.
Taarifa zilizozifikia gazeti hili zilieleza kuwa kikao hicho
kilihudhuriwa na Mwenyekiti, Rais Kikwete, Katibu Mkuu, Abdulahaman
Kinana, Makamu Mwenyekiti Bara, Phillip Mangula na Makamu Mwenyekiti,
Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein,
Chanzo chetu cha habari kilifahamisha kuwa Mwenyekiti, alikuwa
anasisitiza kufutwa kwa adhabu hiyo ili wapate nafasi ya kugombea, huku
mjumbe mwingine aking’ang’ania isifutwe.
Hata hivyo, Nape alipoulizwa kuhusiana na kikao hicho alisema
hakukuwa na kikao chochote zaidi ya cha maadili kilichofanyika na
wajumbe kutawanyika.
Aidha, alisema wale wote wanaotaka kugombea, yaani waliokuwa kwenye
adhabu na wengine watakojiingiza katika kampeni mapema na kukiuka miiko
na maadili ya chama, taarifa za kukiukwa kwao zitatumika kwenye mchujo
wa nafasi walizoziomba hasa kwenye urais.
"Taarifa hizo zitapima na kuangalia kwa sifa, nafasi walizoziomba
kama wanafaa au hawafai katika kupata uteuzi wa nafasi wanayoiomba,
sehemu hii ni ya muhimu sana," alisema.
Hata hivyo, alisema watu wanaangalia vikao hivyo vya CCM na wana
presha za makambi hivyo vitu vinavyoenea kwenye mtandao na mtaani ni vya
uongo kwani Kamati Kuu haijatoa onyo kali kwa wanachama hao.
"Hakuna barua wala onyo kali zaidi ya haya niliyozungumza,"alisema.
Awali akitoa taarifa kwa mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya
Kikwete, Katibu Mkuu wa CCM, Abdurahaman Kinana, alisema wajumbe
waliohudhuria ni 30 kati ya 32 waliotakiwa kuwepo.
Wajumbe ambao hawakuwepo ni Makamu wa Rais, Mohammed Gharib Bilal ambaye yupo China.
LOWASSA
Kufuatia maamuzi hayo Lowassa alisema uadilifu wake ndani ya chama
umemfanya afutiwe adhabu hiyo na kwamba yaliyotokea ni sehemu ya safari
yake ya matumaini.
Akiongea kwa niaba ya Waziri Mkuu aliyejiuzulu na Mbunge wa
Monduli, Msemaji wake, Aboubakar Liongo, alisema “Lowassa anaendelea
na vikao na yaliyojitokeza kuhusiana na adhabu aliyopewa ni sehemu ya
safari ya matumaini,” alisema.
Aidha, alisema Lowassa anajiandaa kutangaza nia wiki ijayo, jijini Arusha.
MAKAMBA
Kwa upande wake , Makamba alisema amefurahia kufutiwa adhabu hiyo na sasa safari ya ushindi inaanza.
SUMAYE
Alisema walikuwa na adhabu ya mwaka mmoja na iliisha mwezi Februari, walichokuwa wanasubiri ni vikao vya maamuzi kuketi.
Alisema sasa wako huru na watatekeleza matakwa ya chama katika kugombea uchaguzi mkuu.
MEMBE
Alipopigiwa simu kuzungumzia kufutiwa adhabu hiyo alijibu kwa kifupi “No comment” (sina cha kuzungumza)
No comments:
Post a Comment