Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene.
Kampuni hiyo imesema serikali imepata hasara ya Sh. bilioni 6.0
katika kipindi cha siku nne, ambacho kampuni hiyo ilisitishwa kutoa
huduma ya kuuza umeme. Kampuni hiyo ilisema huuza umeme kwa asilimia 75.
Aidha, kampuni hiyo imesema haijapata notisi toka serikalini ya kusitishwa kwa mkataba wake na Tanesco.
Juzi waziri Simbachewene alitangaza kusitisha mkataba na kampuni
hiyo kwa kushindwa kutoa huduma bora ya mfumo wa Luku kutokana na
mitambo yao kutokukidhi vigezo na kusababisha usumbufu kwa wateja.
NIPASHE Jumamosi ilifanya mahojiano na Meneja Ukuzaji Biashara na
Masoko kutoka Kampuni ya Selcom, Juma Mgoli, ambaye alisema ameshangazwa
na taarifa ya waziri kudai kampuni yake haina vigezo wakati imekuwa
ikiuza umeme wa Tanesco kwa asilimia 75.
Alisema wameshindwa kuelewa ni vigezo gani vilivyotumiwa na waziri
kusitisha mkataba, wakati kampuni yake imekuwa ikiuza umeme wa Sh.
bilioni 1.0 hadi bilioni 2.0 kwa siku.
Aliongeza kuwa inapokaribia mwisho wa mwezi mauzo hufika hadi Sh. bilioni 4.0 kwa siku.
Alisema kutokana na mauzo hayo, inaonyesha dhahiri kuwa kampuni yao
inafanya vizuri sokoni na kwamba tatizo la mtandao halipo upande wao
bali lipo kwa Tanesco.
Alisema Tanesco ina mashine za Electronic Vending Getway (EVG)
ambazo uwezo wake ni mdogo katika kuhudumia wateja, hivyo kusababisha
ukosefu wa mtandao. “Mfano mzuri nadhani unaona tangu tumeacha kutoa
hiyo huduma kuna foleni kubwa kwenye vituo vinavyouza umeme sasa,
tutaambiwaje hatufanyi vizuri sokoni,” alihoji.
Aliongeza kuwa Selcom imejiunganisha kwenye benki 34 kwa ajili ya kutoa huduma hiyo.
Alisema toka kampuni yake ilipozuiwa kuuza umeme katika kipindi
cha siku nne, Tanesco imepata hasara ya Sh. bilioni 6.0 na serikali
imepoteza mapato ya kodi ya zaidi ya Sh. bilioni 1.0.
Hata hivyo, alisema suala hilo linahusu masuala ya kisheria na
kwamba wameshawasiliana na wanasheria wao kuangalia kama kuna ukiukwaji
wowote wa mkataba huo ili sheria ichukue mkondo wake.
Alisema waziri hana mamlaka ya kuvunja mkataba kienyeji kwani uvunjaji wa mkataba una utaratibu wake.
Usitishwaji wa huduma hiyo, ulianza tangu mwanzo wa wiki hii ambapo
juzi baadhi ya wateja walikuwa wakitumia ujumbe mfupi kwenye simu zao
za mkononi unaosema: "Ndugu mteja huduma ya Luku haipatikani kwa sasa
kutokana na shida iliyopo upande wa washirika wetu, tafadhali tembelea
wakala wa Tanesco kununua umeme wako".
Hata hivyo, jana wakati gazeti hili likielekea mtamboni ujumbe
mwingine kupitia simu za mkononi ulitumwa ukieleza: "Ndugu mteja sasa
unaweza kununua umeme wako wa Tigopesa kwa kupiga namba *150* 01#
NIPASHE ilishuhudia vituo vingi vinavyouza umeme wa Luku vikiwa na foleni ya wateja wanaotaka huduma hiyo.
Baadhi ya wateja walikuwa wakiilalamikia Tanesco kuifungia kampuni
iliyokuwa ikitoa huduma hiyo kwa njia ya mtandao na kusababisha usumbufu
mkubwa.
No comments:
Post a Comment