Saturday, 23 May 2015

Yanga kujifua Zanzibar Kagame

Kikosi cha Yanga
Mabingwa mara tano wa Kombe la Kagame, Yanga wanataraji kuweka  kambi Zanzibar ya maandalizi ya michuano hiyo ya klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati itakayofanyika nchini Julai.
 
Wachezaji wa Yanga kwa sasa wapo mapumzikoni baada ya kutwaa ubingwa wa 25 wa ligi kuu ya Bara na kumalizika kwa msimu Mei 9.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini jana, mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Jerry Muro alisema maandalizi ya kambi hiyo yamekamilika.
Yanga itakuwa ikiwania kutwaa ubingwa mwingine wa Kombe la Kagame nyumbani kama inavyopewa nafasi kubwa, na kuwafikia watani wa jadi Simba kama klabu zilizobeba kombe hilo mara nyingi zaidi.
Tangu kuanza kwa michuano hiyo mwaka 1974, timu zifuatazo zimetwaa ubingwa mara nyingi zaidi: 6 - Simba (Bara), 5 - AFC Leopards (Kenya) na Yanga (Bara), 3 - Tusker (Kenya) na Gor Mahia (Kenya).
 
Wakati El Mereikh (Sudan), SC Villa (Uganda), Kenya Breweries na APR (Rwanda) zimeshinda mara mbili, Vital'O (Burundi), Rayon Sports, Attraco (Rwanda) na Uganda Police zimewahi kuwa mabingwa mara moja kila moja.
El Mereikh ndiyo mabingwa watetezi wa michuano hiyo baada ya kuwafunga wenyeji APR jijini Kigali katikati ya mwaka jana.
 
Wachezaji wote wamepewa taarifa kwa ajili ya kambi hiyo ya Zanzibar, alisema Muro bila kutaja tarehe ya kuanza.
 
Alisema uongozi umejipanga mapema kutokana na kuelekeza macho yake katika michuano hiyo ambayo "ina changamoto kubwa kwa klabu shiriki."
Wakati huo huo, mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Jerry Muro alisema hatma ya wachezaji Jerry Tegete na Hussein Javu ambaye amemaliza mkataba lipo mikononi mwa kamati ya usajili, ambayo imepokea ripoti ya usajili ya kocha na inaijadili.
 
Alisema chochote kitakachoamuliwa na kamati kuhusu wachezaji hao kitawekwa hadharani lakini kwa sasa wachezaji hao bado ni wa Yanga.
Muro alisema wanataka kuibadilisha Yanga ili mwakani iwe ya kimataifa zaidi kutokana na usajili wake.
 
Lengo la mwakani ni kufika mbali katika Ligi ya Klabu Bingwa Afrika na taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment