Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiwasilisha bungeni hotuba ya mwelekeo na malengo ya makadirio ya matumizi ya ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2015/2016, bungeni Dodoma jana.
Dodoma. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana
aliwasilisha Bajeti ya lala salama ya ofisi yake na taasisi zake kwa
mwaka 2015/16, huku akieleza mafanikio katika sekta mbalimbali
yaliyofikiwa na Serikali ya Awamu ya Nne tangu ilipoingia madarakani
mwaka 2005.
Bajeti hiyo iliwasilishwa katika mkutano wa 20 wa
Bunge la 10 ambao ndiyo wa mwisho kwa Serikali ya Awamu ya Nne kabla ya
Bunge kuvunjwa kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Akitumia saa 2.30 kusoma hotuba hiyo ya kurasa
105, Pinda alisema katika mwaka 2015/16, ofisi yake imepanga kutumia
Sh5.8 trilioni ambazo matumizi yake yatafafanuliwa katika bajeti za
wizara zilizopo chini ya ofisi yake.
Pinda alitumia fursa hiyo kuzungumzia pamoja na
mambo mengine, mafanikio katika usafirishaji wa reli, bila kugusia
harufu ya ufisadi katika ununuzi wa mabehewa katika Kampuni ya Reli
Tanzania (TRL) uliosababisha vigogo wake watano kusimamishwa kazi.
Mafanikio ya Serikali
Pinda alisema tangu 2005 hadi 2014, Serikali
imeweka mazingira wezeshi ya uwekezaji, kwamba Kituo cha Uwekezaji
Tanzania (TIC) kimesajili miradi 7,159 yenye thamani ya Dola za Marekani
74,274 milioni na kutoa ajira 869,635.
Alisema katika kipindi cha miaka 10, Serikali
iliwawezesha wananchi kubaini fursa za kiuchumi kupitia mpango wa
uwezeshaji wananchi kiuchumi na kuongeza ajira ulioanzishwa mwaka 2006,
kutoa mikopo ya masharti nafuu ya Sh50 bilioni iliyotolewa kwa
wajasiriamali 74,790.
“Katika mwaka 2015/16, Serikali itaendelea
kuwahamasisha wananchi kuanzisha na kujiunga na vikundi vya uzalishaji
mali, vyama vya kuweka akiba na kukopa ili waweze kukopesheka,” alisema.
Kuhusu ajira, alisema vijana walioajiriwa katika sekta ya umma ni
188,087 na walioajiriwa katika sekta binafsi ni milioni moja wakati
vijana milioni 15 wamejiajiri katika shughuli za kilimo, mifugo, uvuvi
na biashara ndogondogo.
Alisema viwanda vya kusindika maziwa vimeongezeka kutoka 22 mwaka 2005 hadi 74 mwaka huu.
Kuhusu uchumi, Waziri Mkuu alisema umekua kutoka
asilimia 4.7 mwaka 2006 hadi asilimia saba mwaka 2014 na hivyo kuongeza
pato la Mtanzania kutoka Sh360,865 mwaka 2005 hadi Sh1.7 milioni mwaka
2014.
“Uzalishaji wa mazao ya uvuvi umeongezeka kutoka
tani 341,109 mwaka 2006 hadi tani 375,158 mwaka 2015. Tani 43,354 za
mazao ya uvuvi na tani 42,100 za samaki hai wa mapambo ziliuzwa nje ya
nchi na kuliingizia Taifa Sh7.5 bilioni. Viwanda vya kuchakata samaki
vimeongezeka kutoka 25 hadi 48,” alisema Pinda. Pia, alizungumzia pia
sekta ya utalii akisema idadi ya watalii nchini imeongezeka kutoka
1,095,884 mwaka 2013 hadi 1,102,026 na kuongeza mapato ya utalii kutoka
Dola za Marekani 1,853 milioni hadi Dola 1,983 milioni.
Pinda alisema thamani ya madini yaliyozalishwa nchini na kuuzwa
nje iliongezeka kutoka Dola 655.5 mwaka 2005 hadi Dola milioni 1,794
mwaka 2014, huku sekta ya viwanda ikikua kwa wastani wa asilimia 7.7.
Barabara
“Serikali ya awamu ya nne imekamilisha ujenzi wa
barabara zenye urefu wa kilomita 1,226 na kilomita 1,305 za barabara kuu
zimejengwa kwa kiwango cha lami na kilomita 960 kufanyiwa ukarabati.
Kilomita 393 za barabara za mikoa zimejengwa kwa kiwango cha lami,”
alisema.
Alisema katika mwaka ujao wa fedha, Serikali
itaanza ujenzi wa Bandari ya Mbegani - Bagamoyo itakayokuwa kubwa Afrika
Mashariki na Kati sambamba na kujenga, kupanua na kukarabati viwanja
vya ndege.
Kuhusu umeme, alisema Serikali imeimarisha
miundombinu ya uzalishaji wa umeme nchini kwa kiwango kikubwa na
kuongeza uzalishaji kutoka megawati 891 mwaka 2005 hadi 1,226 Machi 2015
na kwamba watumiaji wa umeme wameongezeka kutoka asilimia 13 hadi 36.
Pia, aligusia mafanikio yaliyopatikana katika
elimu, ikiwamo ujenzi wa maabara, kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi
wanaojiunga vyuo vikuu na kuboresha sekta ya afya chini ya Mpango wa
Maendeleo ya Afya ya Msingi wa mwaka 2007 hadi 2017.
Wanawake katika uongozi
Pinda alisema: “Katika kipindi cha miaka 10 ya
uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne, idadi ya mawaziri wanawake
imeongezeka kutoka sita kati ya mawaziri 25 mwaka 2005 hadi kufikia 10
kati ya mawaziri 30 mwaka 2015.”
“Wakuu wa mikoa wameongezeka kutoka wawili kati
ya 21 mwaka 2005 hadi saba kati ya wakuu wa mikoa 25 mwaka 2015. Wakuu
wa wilaya wameongezeka kutoka 20 kati ya wakuu wa wilaya 104 mwaka 2005
hadi wakuu wa wilaya 46 kati ya 133 mwaka 2015.
Alisema majaji wanawake wameongezeka kutoka wanane
kati ya 50 mwaka 2005 hadi kufikia 24 kati ya majaji 67 mwaka 2015 na
wabunge wanawake wametoka 62 kati ya 288 mwaka 2005 hadi kufikia 127
kati ya 357 mwaka 2015.
Mauaji ya albino
Akizungumzia mauaji ya albino, Pinda aliwataka
viongozi wa dini kuendelea kuhubiri na kuelimisha jamii kuondokana na
imani potofu za kishirikina kwa kuamini kuwa kupata kiungo cha albino ni
kutajirika. “Mpaka sasa watuhumiwa 181 wamekamatwa na kuhojiwa tangu
mwaka 2006 na 2015. Kati yao 133 wamefikishwa mahakamani na kufunguliwa
kesi za mauaji na 46 kwa makosa ya kujeruhi na 13 wamehukumiwa kunyongwa
hadi kufa,” alisema Pinda.
Ajali za barabarani
Pinda alisema kuanzia Julai 2014 hadi Machi mwaka
huu, kulikuwa na matukio 8,072 ya ajali za barabarani ambayo
yalisababisha vifo vya watu 2,883 na kuwa jeshi la polisi na vyombo
vingine vya dola vinafanya utafiti wa kina kuhusu ajali hizo.
No comments:
Post a Comment