Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisobwa.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni, limetumia mabomu ya machozi
kuwatawanya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), wanaoishi
katika hosteli za Mabibo ambao walikuwa wakiandamana kudai fedha zao za
kujikimu.
Walichukua hatua hiyo kutokana na kucheleweshewa mikopo na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya juu (HELSB).
Tukio hilo lilitokea usiku walipoandamana kudai wawekewe fedha kwenye akaunti zao ambazo zimecheleweshwa kwa wiki 11.
Wanafunzi hao waliondoka Mabibo saa 4:00 usiku kwa maandamano
kuelekea UDSM ili kuwashirikisha wenzao kushinikiza uongozi kufatilia
madai yao ndipo walipokutana na Polisi waliolazimika kutumia mabomu ya
machozi kuwatawanya baada ya kushindwa kutii amri ya kusitisha
maandamano.
Katika purukushani hizo zilizodumu dumu kwa saa tatu, Polisi
walitumia mabomu mengi kuwatawanya wanafunzi hao huku wanafunzi watatu
wakikamatwa na wengine watatu wakijeruhiwa.
Licha ya kudhibitiwa na Jeshi hilo, jana wanafunzi hao waliendelea na mgomo wa kutoingia darasani mpaka watakapolipwa fedha zao.
Rais wa Serikali ya wanafunzi (Daruso) Irene Ishengoma, alisema
maandamano hayo yalitokea baada ya wanafunzi kutangaziwa kuwa
watakopeshwa Sh. 20,000 na chuo kwa ajili ya kujikimu wakati wakisubiria
malipo yao.
“Baada ya kusubiria kwa muda mrefu, uongozi wa chuo ulituahidi
kutukopesha Sh. 20,000 kwa wanafunzi 7,000 ambao wanaidai HESLB tangu
Mei 8, mwaka huu, walipaswa kutuwekea fedha zetu,” alisema.
Alisema baada ya tamko hilo kutoka Serikali ya wanafunzi,
wanafunzi hao waligoma kupokea fedha hizo kwani kiwango hicho ni
kidogo.
Ishengoma alisema baada ya mvutano huo walikubaliana kutoingia darasani mpaka watakapolipwa madai yao.
Aliongeza kuwa walipozungumza na uongozi wa chuo waliahidiwa kuwa fedha hizo zitawekwa leo, hivyo walejee madarasani.
Alisema wanafunzi hawakukubaliana na taarifa hizo kwani wao waliachokuwa wakitaka ni HESLB kuwalipa fedha zao.
“Kwanini tulipwe Sh. 20,000 wakati tunaidai bodi Sh. 450,000?” Hii
haikubaliki kwani hivi sasa maisha yamepanda na wanafunzi wengi wanaishi
kuwa kukopa,” alisema.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Rwekaza Mukandala, alisema
amekutana na uongozi wa Daruso kujadiliana namna ya kutatua tatizo hilo.
Alisema wamekubaliana kuwa wanafunzi wote wangelipwa fedha zao zote jana kwani fedha hizo zimeshafika HESLB.
Alisema walilazimika kuwakopesha Sh. 20,000 wakiamini fedha zao zitalipwa ndani ya muda mrefu.
“Leo (jana) fedha zitawekwa katika akaunti za wanafunzi ambazo walikuwa wakidai,” alisema.
Aliongeza kuwa bado chuo kinafanya tathmini ya uharibifu uliotokea
wakati wa maandamano ya wanafunzi hao kwani inasemekana walivunja
milango, madirisha na kupasua baadhi ya vioo vya magari.
“Kuna taarifa kuwa kuna wanafunzi watatu ambao waliumia katika
tukio hilo, lakini hivi sasa wanaendelea vizuri baada ya kupatiwa
matibabu na kuruhusiwa,” alisema.
Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB,
Cosmas Mwaisobwa, alisema wanajitahidi kushughulikia madai ya wanafunzi
wa vyuo vyote ambavyo vinanufaika na fedha za Bodi hiyo.
“Hatuwezi kusema ni lini au saa ngapi tutakuwa tumewaingizia fedha
hizo kwani hatulipi kwa chuo kimoja bali ni vyuo vyote ambavyo
vinanufaika na HESLB,” alisema.
No comments:
Post a Comment