Wazir Mkuu Kassim Majaliwa
amezindua mradi wa maji safi na tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita
200,000 ambao utahudumia vijiji viwili vya Mkongotema na Magingo katika
kata ya Mkongotema, wilayani Songea, mkoani Ruvuma.
Akisoma taarifa ya mradi huo kwa
Waziri Mkuu jana (Alhamisi, Januari 5, 2017), Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Madaba, Bw. Shafi Mpenda alisema mradi huo ulioanza kujengwa mwaka
2013, umegharimu sh. bilioni 1.09.
“Hadi kukamilika kwake, mradi huu
umegharimu sh. 1,092,439,812 ambapo kati ya hizo sh. 1,069,647,312
zimetolewa na Serikali kuu na sh. 22,792,500 zimechangwa na wananchi,”
alisema.
Bw. Mpenda alisema mpaka sasa kaya
915 zenye watu 5,300 zinahudumiwa na mradi huo wenye vituo 57 vya
kutolea huduma za maji kwa jamii. Alisema lengo lao ni kufikisha vituo
71 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Akifafanua zaidi, Bw. Mpenda
alisema kukamilika kwa mradi huo kumesaidia kuwapunguzia wananchi
gharama za kununua maji ambapo pipa moja liligharimu sh. 3,000. “Pia
kutasaidia kupunguza adha ya kufuata maji umbali mrefu; kupunguza
magonjwa yanayotokana na mlipuko na kuwapa wananchi muda wa kutosha
kufanya shughuli nyingine za maendeleo,” alisema.
Akizungumza na wananchi
waliohudhuria uzinduzi wa mradi huo, Waziri Mkuu aliwapongeza wakazi hao
kuwa kukubali kuchangia ujenzi wa mradi huo kwani katika baadhi ya
maeneo miradi kama hiyo imekwama kukamilika kwa sababu wananchi
waligomea kuchangia.
Aliwataka wakazi wa vijiji hivyo
wasiharibu mazingira na watunze vyanzo vya maji ili mradi huo uweze kuwa
endelevu. “Mradi huu ni lazima tuutunze kwani hali ya hewa imebadilika
sana hivi sasa, sababu ni sisi wenyewe wananchi ambao tumekata miti sana
ili kupanua maeneo ya kilimo.”
“Changamoto inayotupata hivi sasa
ni kwama tumebakia kuwa na eneo kubwa la kilimo lakini mazao
yanayopatikana ni kidogo. Mtazamo wetu katika Serikali hivi sasa ni
kulima kwenye eneo dogo lakini mavuno yawe mengi,” alisema.
“Mtu asilime chochote karibu na
chanzo hiki ili tuweze kukitunza chanzo chetu. Na wenyeviti wa Serikali
za vijiji vyote viwili, wekeni utaratibu wa wananchi kwenda kupanda miti
ili eneo hili libaki kuwa na unyevunyevu kwa muda mrefu,” alisisitiza.
“Sera ya Serikali ni kuhakikisha
kuwa kila mwananchi anapata maji katika umbali usiozidi mita 400, na
hili tutaweza kulitimiza kama tu mtatunza vyanzo vya maji vilivyopo,”
alisema.
Alitumia fursa hiyo kuwaomba
wakazi wa vijiji hivyo watunze akiba ya chakula walichonachi kwa sababu
hali ya hewa imebadilika na hakuna anayejua mvua itaanza kunyesha lini.
“Hatujui mvua itakuja lini na kwa kiasi gani; mara zitakapoanza kunyesha
kila mmoja katika familia ahakikishe analima mazao mbadala kama kunde,
maharage na mihogo ambayo yanastahimili ukame,” alisema.
Waziri Mkuu pia alikagua utoaji huduma kwenye kituo cha afya cha madaba na ujenzi wa kituo cha kupozea umeme cha Madaba.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
IJUMAA, JANUARI 6, 2017.
No comments:
Post a Comment