Kukutana kwa timu hizo kunatokana na Simba kushinda 2-0 dhidi ya
Jang’ombe Boys jana jioni katika mchezo wa mwisho wa Kundi A Kombe la
Mapinduzi Uwanja wa Amaan.
Matokeo hayo yanaifanya Simba imalize kileleni mwa Kundi A kwa pointi
zake 10, ikifuatiwa na Jang’ombe Boys, Taifa Jang’ombe zenye pointi sita
kila moja na URA yenye pointi nne.
Hata hivyo, Taifa Jang'ombe na URA jana usiku zilicheza mechi yao ya
mwisho ambayo itaamua timu itakayokutana na Azam nusu fainali.
Ikumbukwe Yanga imeshika nafasi ya pili Kundi B nyuma ya Azam
walioongoza kutokana na mabao ya kufunga na kufungwa baada ya kufungana
kwa pointi saba kila timu.
Katika mchezo wa jana, mabao yote ya Simba yalifungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Laudit Mavugo, moja kila kipindi.
Mavugo aliyesajiliwa Simba msimu huu kutoka Vital’O ya kwao Burundi,
alifunga bao la kwanza dakika ya 11 kwa shuti baada ya kuukuta mpira
uliorudi kufuatia kugonga nguzo ya lango kutokana na shuti la winga
Shiza Kichuya aliyepokea pasi nzuri ya mshambuliaji mzawa Juma Luizio,
Mavugo akafunga bao la pili dakika ya 53 kwa shuti kali tena baada ya
kupokea pasi ya Kichuya pembeni kulia na kumkokota beki wa Jang’ombe
hadi kwenye 18 kabla ya kufunga.
Bao hilo likawafanya Jang’ombe Boys kupoteana na kuwapa fursa Simba
walio chini ya kocha Mcameroon Joseph Omog kutawala zaidi mchezo.
Kilichofuatia ni kasi ya mashmbulizi mfululizo langoni mwa Jang’ombe
Boys na kosa kosa za mabao ya wazi hadi filimbi ya mwisho. Baada ya
mchezo huo, Mavugo akachaguliwa kuwa mchezaji bora.
Nahodha wa Simba, Mkude alisema wamefurahi kwa ushindi huo na kuongoza
Kundi A na kwamba kuelekea mchezo wa nusu fainali dhidi ya mahasimu wao,
Yanga hawana wasiwasi.
“Sisi tumejiandaa vizuri, ni matumaini yetu na wao wamejiandaa vizuri,
mchezo wa mpira wa miguu ni maandalizi, baada ya maandalizi tutakutana
tutacheza, utakuwa mchezo mzuri, kipimo kizuri kwetu na kwao, dakika 90
zitaamua,” alisema.
Kikosi cha Simba kilikuwa; Peter Manyika, Janvier Besala Bokongu/Vincent Costa dk.78, Mohammed Hussein ‘Thabalala’, Abdi
Banda, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shiza Kichuya/Hijja Ugando dk.71,
Muzamil Yassin/James Kotei dk.46, Pastory Athanas, Laudit Mavugo/Jamal
Mnyate dk.55 na Juma Luizio/Moses Kitundu dk.63.
Jang’ombe Boy: Hashim Ruga, Shomary Ismail, Muharami Issa, Ibrahim
Said/Abubakar Ali dk.72, Ali Badru, Yakoub Omar, Abdi Kassim, Khamis
Makame, Hafidh Juma, Juma Ali/Ali Suleiman dk.67 na Abdulsamad Ali.
No comments:
Post a Comment