Na Mwandishi Wetu
WACHEZAJI nembo ya Tanzania
Kimataifa wanatarajia kuzindua mashindano ya kuwania kombe la Diwani wa
Kata ya Tabata, Patrick Assenga (Chadema) yanayotarajia kuanza
(Kesho-Jumamosi) mwishoni mwa wiki kwenye uwanja wa Shule ya msingi
Tabata.
Akizungumza jana kwenye hafla ya
kukabidhi vifaa kwa timu shiriki za mashindano hayo, Assenga alisema
wachezaji wanaotarajia kuwa sehemu ya uzinduzi wa mashindano hayo ni
pamopja na Jellah Mtagwa, Peter Tino, Dua Said, Moses Mkandawile na
wengineo waliowahi kuitangaza nchi nje ya mipaka yake.
“Tumepanga wachezaji wa zamani
watacheza kwa dakika chache katika uzinduzi wa mashindano hayo na
baadaye tutawakabidhi zawadi maalum kwa lengo la kuthamini mchango wao
katika soka la Tanzania,” alisema Assenga.
Assenga alisema katika mashindano
yake yanayotarajia kushirikisha timu 16 za mitaa nane iliyoko katika
kata hiyo, ameguswa na wachezaji waliowahi kutamba katika soka la
Tanzania ambao hawathaminiwi kama mashujaa waliofanya makubwa katika
nchi hii.
Assenga alisema uandaaji wa
mashindano hayo ni ahadi aliyowahi kuitoa wakati wa kampeni za kuwania
uongozi huo kwamba atajikita zaidi kwenye kusaidia vijana hasa katika
upande wa michezo na maendeleo mengine yanayowahusu vijana.
Diwani huyo alisema pamoja na
kuwa na lengo la kuwasaidia vijana pia kuwapa thamani waliokuwa
wachezaji waliowahi kuitangaza Tanzania katika nchi nyingine kama
Nigeria, Liberia na kwingineko.
Aidha Diwani huyo alisema
mashindano hayo yatakuwa yakifanyika kila mwaka hadi atakapomaliza
uongozi wake katika Kata hiyo ambako katika uzinduzi huo, Meya wa Ilala
Charles Kuyeko anatarajia kuwa mgeni rasmi.
“Nimepanga pia kabla ya kuanza
mashindano, Jumamosi nitashirikiana na na wananchi wa Tabata kufanya
usafi kwa kushirikiana na wananchi wa Kata hiyo, hivyo nawaomba wakazi
wa Tabata kujitokeza kufanya usafi katika maeneo yao,” alisema Assenga.
Mwenyekiti wa Kamati ya
maandalizi ya mashindano hayo, Rogers Peter alisema wamejipanga vilivyo
kufanikisha mashindano hayo ambayo yanabeba taswira ya Tanzania kwa
sababu wamekumbuka wachezaji wa zamani na kuwalinganisha na vijana wa
sasa lengo likiwa ni kutoa elimu kwa vijana na kuwatengenezea fursa
zaidi kwa ajira.
Hata hivyo, Peter alitumia fursa
hiyo kumuomba Diwani kutupia macho fursa nyingine za mchezo kkwa upande
wa soka la ufukweni na wanawake akiwa na dhamira ya kutaka Tabata kuwa
kisima cha vipajia nchini.
Naye Mkuu wa Nidhamu wa
mashindano hayo, aliyekuwa golikipa wa Simba, Moses Mkandawile alisema
katika historia ya Tabata haijawahi kutokea kiongozi mwenye maono kama
Assenga ambaye ameguswa zaidi na vijana ambao mara nyingi wanashinda
vijiweni.
No comments:
Post a Comment