Hii ni baada ya beki Paschal Serge Wawa kumaliza mkataba na klabu hiyo na kutoongezwa tena mwingine.
Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez anaonekana kutomkubali beki huyo.
Labda ni kwa sababu tangu atue kwenye klabu hiyo hajamuona akicheza.
Kwa muda mrefu sasa, beki huyo aliyejizolea sifa nchini na kuwa kipenzi cha mashabiki wengi wa soka nchini amekuwa majeruhi.
Sina uhakika sana endapo kocha huyo angekuja wakati Wawa akiwa uwanjani na kushuhudia shughuli yake angefanya uamuzi huo.
Wawa raia wa Ivory Coast, amerejea kwenye klabu yake ya zamani, El Merreikh ya Sudan.
Amesaini mkataba wa miaka miwili. Wao hawana wasiwasi na uwezo wa beki
huyo kwa sababu wanamfahamu na ndiko alikotoka kabla ya Azam kumtia
machoni na kumchukua.
Mjadala uliokuwapo kwa wadau wengi wa soka ni kwamba timu hiyo imekosea
kumuacha beki kisiki na mwenye uwezo wa hali ya juu kama huyo kuondoka.
Wengine hawaamini kama mabeki wa kati waliokuwapo kwenye kikosi cha Azam wanafikia uwezo wa Wawa.
Mwishoni wanamaliza kusema kuwa Azam imepoteza kifaa na kuongeza kuwa ipo siku isiyo na jina watakuja kumkumbuka.
Azam bila Wawa tayari imesharuhusu mabao 14 mpaka sasa, wakati msimu wa
2014/15 alipocheza mechi karibu zote, Azam iliruhusu nyavu zake
kutikiswa mara 18 tu kwa msimu mzima.
Msimu uliopita Azam iliruhusu mabao 23, na sababu kubwa beki huyo hakucheza mechi zote kutokana na kuanza kuwa majeruhi.
Wawa ni mchezaji pekee ambaye mashabiki wa timu hasimu za Simba na Yanga
wote walikuwa wanamkubali na pia wangependa hata timu zao ziwe na beki
kama huyo.
Kabla ya kuondoka, Wawa alieleza namna majeraha yake yalivyokuwa yakimnyima raha.
“Nilipopata majeraha haya nilikuwa nafikiria ndio basi sitaweza kucheza
soka, nilikuwa nafikiria natakiwa kufanyiwa upasuaji na nilikuwa na hofu
kubwa ya kukaa mwaka mmoja nje ya dimba bila kucheza,” alisema na
kuongeza.
“Lakini pia mara baada ya kupata majeraha haya, niliweza kupumzika kwa
muda wa takriban miezi miwili kabla ya kwenda Afrika Kusini na kisha
daktari aliuchunguza mguu wangu na kuniambia kuwa nina matatizo katika
goti," anasema.
Hata hivyo, alifurahi alipoambiwa kuwa tatizo lake halihitaji upasuaji.
“Namshukuru sana Mungu kwani jambo la kwanza nililofanya wiki moja kabla
ya kwenda huko nilimwomba Mungu nisikutane na upasuaji,” anasema
mchezaji huyo ambaye mashabiki walimpachika majina ya 'Guu la Chuma',
'Roho ya Paka' na 'Mwili wa Simba'.
Hakupata tatizo la upasuaji, lakini alikuja kukutana na kadhia ya kuachwa kwenye kikosi chake.
Sifa zake
Pamoja na kucheza ligi, lakini alijizolea sifa zaidi na majina mengi kwenye michuano ya Kombe la Kagame mwaka 2015.
Jacob Mulee, kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Kenya ambaye alikuwa
akichambua michezo mbalimbali kwenye kituo kimoja cha michezo TV moja ya
Afrika Kusini, alisikika akisema kama Wawa asingekuwa mchezaji basi
angekuwa mwanajeshi.
Muda wote awapo uwanjani Wawa ameonekana kuwa ni mchezaji anayejituma
dakika zote za mchezo, anatumia nguvu pale inapohitajika, lakini
vilevile anatumia akili nyingi pale anapolazimika kufanya hivyo hasa
anapokuwa anamkaba mchezaji ndani ya eneo lake la hatari.
Anapokutana na mshambuliaji asiyeweza kupambana inakuwa ni kazi rahisi kwake kuondoka na mpira kirahisi.
Wawa amekuwa tofauti na mabeki wengi wa Tanzania, Afrika Mashariki na
Kati na hii inatokana na uzoefu na kujitambua kuwa yeye ni mchezaji wa
kimataifa. Ni mara chache sana amefanya faulo pale anapomkabili mpinzani
wake na hiyo imemsaidia kuepuka kadi zisizo za lazima kwake.
Ndiyo maana pamoja na mabavu aliyokuwa nayo, alipata kadi moja tu ya njano kwenye michuano hiyo.
Alikotokea
Alizaliwa Januari 1, 1986 Bingerville, Ivory Coast. Wawa alianza kucheza
mpira mwaka 2003 kwenye Academy ya ASEC Mimosas ambayo imezalisha
wachezaji wengi wa kiafrika wenye majina makubwa barani Ulaya na duniani
kwa ujumla.
Alienda kufanya majaribio kwenye klabu ya FC Lorient ya nchini Ufaransa,
lakini mwaka 2010 alijiunga na miamba ya soka ya Sudan timu ya
Al-Merrikh kwa mkataba wa miaka mitatu. Na Novemba 2014 alijiunga na
timu ya Azam FC ya jijini Dar es Salaam.
Kwenye michuano ya Kagame ameonyesha kweli yeye ni beki bora baada ya
kuwazuia washambuliaji walioonekana kuwa hatari kama Michael Olunga wa
Gor Mahia, Donald Ngoma wa Yanga, na wengineo.
Alitangazwa mchezaji bora wa mechi mara tatu kwenye michuano ya Kagame
na kuiongoza safu ya ulinzi ya Azam kumaliza michuano hiyo ikiwa
haijafungwa bao hata moja tangu hatua ya makundi hadi fainali, ilipotwaa
ubingwa kwa kuichapa Gor Mahia mabao 2-0.
No comments:
Post a Comment