Sunday, 27 November 2016

Brela Yatoa Somo Kwa Vijana Kuhusu Ujasiriamali, Biashara

 Naibu Msajili wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni(BRELA)(Sheria za Biashara), Bw.Andrew Mkapa akiwasilisha mada kwenye semena elekezi juu ya ujasiriamali na urasimishaji biashara kwa vijana wa jijini Dar es Salaam. semina hiyo imeandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kwa lengo la kuwaelimisha vijana juu ya ujasiriamali ili waweze kuachana na dhana ya kuajiriwa na kufikiria kujiajiri zaidi kutokana na fursa zilizopo katika maeneo yao.

Washiriki wa semina ya ujasiriamali wakifatilia kwa makini mada inayowasilishwa na Naibu Msajili wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni(BRELA)(Sheria za Biashara), Bw.Andrew Mkapa (hayupo pichani) juu ya umuhimu wa kurasimisha biashara zao ili waweze kupata fursa ya kufanya kazi na kutambulika na Serikali. Semina hiyo imeandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni yenye lengo la kuwaelimisha vijana juu ya ujasiriamali ili waweze kuachana na dhana ya kuajiriwa na kufikiria kujiajiri zaidi kutokana na fursa zilizopo katika maeneo yao.
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umetoa wito  kwa vijana nchini kutumia fursa mbalimbali  za mafunzo ya ujasiriamali na biashara ili kujingea uwezo  wa kujiamini pale wanapoamua kujihusisha na biashara.

 Naibu Msajili  wa Wakala (Sheria za Biashara), Bw.Andrew Mkapa amesema mafunzo ya ujasiriamali na biashara ni nguzo muhimu kwa vijana hasa wanapokuwa na malengo ya kujiajiri kwani mafunzo hutoa mwongozo.  “Ni Muhimu  sana  nawashauri vijana  nchini kujitokeza kwenye mafunzo ya ujasiriamali na biashara muweze kujijengea uwezo na kujua umuhimu kurasimisha biashara zao ili  kutambulike na mamlaka husika,” Bw. Mkapa alitoa wito huo mwishoni mwa wiki  mara baada ya kutoa mada kwenye semina ya ujasiriamali kwa vijana iliyoandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Hapi kwa lengo la kuwajengea uwezo vijana wa kujiajiri.

 Bw. Mkapa alisema, Vijana waondokane na dhan ya kusubiri kuajiliwa pindi wanapomaliza shule  badala yake wajikite  zaidi kwenye kujiajiri wenyewe kwenye biashara na shughuli nyingine za kijamii.  “BRELA imeamua kujikita zaidi katika kutoa elimu ya mafunzo ya kurasimisha biashara kwa vijana ili  kuwahamasisha wapate ufahamu wa jinsi gani wanaweza kuanzisha makampuni na majina ya biashara ili waweze kutambulika kisheria,” alisisitiza.
 Bw. Mkapa ambaye pia alitoa mada iliyowasisimua zaidi vijana, alimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Kindoni, Bw.Hapi kwa jitihada za kuwakutanisha vijana pamoja na kutoa mafuzo ya ujasiriamali na biashara. “Kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu na Msajili wa  Makampuni, nachukua fursa kumpongeza mkuu wa wilaya, wawezeshaji na washiriki wote kwenye mafunzo haya,” alisema na kuongeza kuwa BRELA  ipo tayari muda wote kutoa elimu  jinsi ya ya kusajili makampuni, jinsi ya kusajili majina ya biashara na faida zake.
Haya mafunzo yana maana na yatawasaidia sana vijana pindi watakapoanza kuunganishwa na fursa mbalimbali zinazotolewa kama vile ya mikopo kwani tayari watakuwa na uwelewa mkubwa wa kuzitumia fursa.  “sio tuu kwa vijana hawa waliohudhuria leo hapa lakini ni kwa watu wote kwa ujumla nchi nzima ni muhimu katika karne hii ya sasa kufanya biashara zilizo rasmi,” alisisitiza Mkapa
Mshiriki wa mafunzo, Bw. Medson Moshi ni miongoni mwa vijana waliohudhuria semina hiyo na aliwataka na kuwahimiza vijana wengine kuchangamkia fursa kama hizo na kuachana na mtazamo wa kusubiri  kulipwa fedha ili kuweza kudhuria semina za mafunzo kama hiyo.  “mimi nitoe tu mwito kwa vijana wezangu siyo mpaka upewe fedha ndio uje kwenye mafunzo kama haya, ni vizuri kuangalia elimu kwanza na fedha itakuja baada ya miundombinu  kwanza” alisema, Bw. Moshi.
Semina hiyo  ambayo iliandaliwa  Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kwa lengo la kuwabadilisha kifikra na mtazamo  vijana  kuachana na dhana ya  kupenda kuajiriwa tu ni vizuri wakaanza  kufikiria kujiajiri zaidi kutokana na fursa zilizopo katika maeneo yao.

No comments:

Post a Comment