Wednesday, 30 November 2016

Rungwe amtaka Profesa Lipumba awaombe radhi wana-CUF, Watanzania

. Wakati pande mbili zinazosigana ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) zikiendelea kulumbana, Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe amemtaka Profesa Ibrahimu Lipumba kuwaomba radhi Watanzania.
Rungwe ambaye alikuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, alitoa ushauri huo alipofanya mahojiano na gazeti hili jijini hapa. Akiuzungumzia mgogoro uliomo ndani ya chama hicho alisema busara inahitajika kurekebisha kasoro zilizojitokeza.
“(Profesa) Lipumba anatakiwa akubali kuwa alifanya maamuzi kwa pupa na alitumia zaidi uprofesa badala ya busara. Anatakiwa awaombe radhi wafuasi wa chama hicho na Watanzania kwa ujumla kwa uamuzi wake wa awali,” alisema Rungwe.
Agosti mwaka jana, Profesa Lipumba alimuandikia barua katibu mkuu wa chama hicho akimjulisha juu ya azma yake ya kujiondoa kwenye uenyekiti. Wakati akifanya hivyo, taifa lilikuwa likijiandaa kwa uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais.
Mwaka mmoja baada ya kuandika barua hiyo, Profesa Lipumba aliandika nyingine na kutengua uamuzi huo. Alitaka kurudi kwenye nafasi yake ya uenyekiti ili aendelee kukitumikia chama hicho.
Hatua hiyo ilileta mvutano miongoni mwa wanachama, viongozi na baraza la wadhamini ambao waligawanyika pande mbili, moja ikitaka mwenyekiti huyo arudi kwenye nafasi yake huku wengine wakipinga.
Mvutano huo ulikolea baada ya Mkutano Mkuu wa CUF kujadili na kupitisha barua yake yake ya kujiuzulu. Baadaye, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliingilia kati mgogoro huo na kutangaza kumtambua mwenyekiti huyo na sasa mgogoro huo upo Mahakama Kuu.
Wakati anajiondoa kwenye majukumu ya kila siku ya chama hicho na kubaki kuwa mwanachama wa kawaida, Profesa Lipumba alieleza kutoridhishwa kwake na uamuzi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao alikuwa mwenyekiti mwenza kumkaribisha Edward Lowassa kuwa mgombea urais .
Kwa kuzingatia hayo yote, Rungwe alisema kwa mtu yeyote anayefuatilia mwenendo wa chama hicho na upinzani kwa ujumla, ataona kilichofanywa hakikuwa sahihi, hivyo ni muhimu wa mhusika kuwa muungwana kwa kuomba msamaha.
“CUF ilivurugika kwa muda huo lakini upinzani kwa ujumla umeimarika,” alisema mwenyekiti huyo wa Chaumma.

No comments:

Post a Comment