Na Beatrice Lyimo-MAELEZO-Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi wa kikosi cha
usalama Barabarani Mohammed Mpinga ametoa wito kwa madereva wote ikiwemo
madereva wa Serikali na Mashirika ya Umma kuzingatia sheria za Usalama
Barabarani.
Kamanda Mpinga ameyasema hayo leo
jijini Dar es salaam wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari kuhusu uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya “Abiria paza sauti”
inayotarajiwa kuzinduliwa tarehe 28 Novemba, mwaka huu.
Kamanda Mpinga alisema kumekuwa
tabia ya baadhi ya madereva hususani wa Serikali na mashirika ya umma ya
kutofuata sheria za usalama barabarani kwa kuendesha magari kwa
mwendokasi, na kuwaonya kuwa sheria ni msumeno na inapaswa kufuatwa na
kila mtu.
“Kumekuwa na madereva hasa wa
magari madogo kusafiri kwenda maeneo mbalimbali ya nchi huku wakiwa
hawana uzoefu wa kuendesha umbali mrefu na hivyo kupelekea uvunjifu wa
sheria za barabarani kwa kuendesha kwa mwendokasi na kusababisha ajali”
alifafanua Kamanda Mpinga.
Akifafanua zaidi Kamanda alisema
uzoefu unaonyesha kuwa katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka
kumekuwa na ongezeko kubwa la magari barabarani, na hivyo kuwataka
wananchi kuzingatia sheria za barabarani ili kuweza kupunguza ajali za
barabarani.
Kwa upande wake Kaimu Mtendaji
Mkuu wa Taasisi ya Mabalozi wa Usalama Barabarani, Jackson Kalikumtima
alisema lengo la kampeni ya Paza Sauti ni kuhamasisha ushiriki kamilifu
wa wananchi katika kukabiliana na ajali kwa kuchukua hatua stahiki bila
ya uwepo wa askari.
Pia alisema kuwa kampeni hiyo
imelenga kubadili tabia na mtazamo wa madereva kuhusu usalama barabarani
ili waendeshe kwa kuzingatia sheria bila shuruti na kubadili mtazamo wa
wananchi kuhusu usalama barabarani ili watambue kuwa usalama barabarani
ni jukumu la kila mmoja.
Naye Mwanasheria wa Kikosi cha
Usalama Barabarani nchini, (ASP), Deus Sokoni alisema mkakati wa
kupunguza ajali barabarani katika kampeni hiyo umelenga katika kutoa
elimu kwa jamii ili kuona suala la usalama barabarani ni jukumu la kila
mmoja na si jukumu la Polisi pekee.
“hakuna asiyetumia barabara
duniani, hatutaki ajali tunataka kuishi salama, hivyo kila abiria
anawajibu wa kutunza na kutii sheria za barabarani “ aliongeza
Mwanasheria huyo.
Mwenyekiti wa Chama cha
Kutetea Abiria Taifa (CHAKUA), Hassan Mhanjama aliwataka abiria wote
nchini hususani wanaotajaria kusafiri mwishoni mwa mwaka kuwasiliana na
Mamlaka ya Usafirishaji SUMATRA pindi watakapopandishiwa nauli mbali na
taratibu zilizopo.
No comments:
Post a Comment