Emma Morano ndiye binadamu mzee zaidi aliye hai
Binadamu pekee aliye hai, ambaye inatambuliwa kwamba alizaliwa katika
karne ya kumi na tisa, leo anasherehekea sikukuu yake ya 117 tangu
kuzaliwa kwake.Emma Morano, alizaliwa katika jimbo la Piedmont karibu na mji wa Milan, Italia tarehe 29 Novemba, 1899.
Wakati huo, kampuni ya magari ya Fiat ilikuwa tu ndiyo imeanzishwa. Klabu ya soka ya Milan nayo ilikuwa imeanzishwa wiki chache awali.
Ameshuhudia wafalme watatu wa Italia wakitawazwa na kuondoka, alizaliwa wakati wa utawala wa Mfalme Umberto wa Kwanza.
Aidha, katika maisha yake, kumekuwepo na Baba Watakatifu kumi na mmoja.
Isitoshe, alishuhudia Vita Vikuu vya Kwanza na vya Pili vya Dunia.
Mwaka huu, alitambuliwa kuwa mwanamke mkongwe zaidi aliye hai baada ya kifo cha Mmarekani Susannah Mushatt Jones mwezi Mei. Ndiye pia binadamu pekee aliye hai ambaye alizaliwa miaka 1800.
Bi Morano anasema sana amekuwa na maisha marefu kutokana na jeni.
Mamake aliishi hadi miaka 91. Dadake wengi pia walifariki wakiwa na umri mkubwa.
Anasema kwa kiwango fulani, lishe yake imechangia. Anasema amekuwa akila mayai matatu - mawili yakiwa mabichi, kila siku kwa zaidi ya miaka 90.
Alianza hayo alipokuwa mwanamke kijana, baada ya madaktari kugundua alikuwa na ugonjwa wa anaemia, ambapo mgonjwa hupungukiwa na seli nyekundu za damu au haemoglobini, muda mfupi baada ya Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia.
Siku hizi amepunguza na hula mayai mawili pekee, na biskuti kadha.
Hilo linaenda kinyume kabisa na ushauri wa sasa wa madaktari kuhusu jinsi ya kuishi maisha marefu na yenye afya, daktari wake wa miaka 27 Carlo Bava ameambia AFP.
"Emma hula mboga chache sana, na hali matunda sana. Nilipokutana naye alikuwa anakla mayai matatu kila siku, mawili mabichi kila asubuhi na moja la kupikwa mchana saa sita na kisha anakula kuku chakula cha jioni."
Licha ya haya, Carla anasema, mwanamke huyo anaonekana kuwa na "maisha tele".
'Nioe au nikuue'
Jambo jingine ambalo Bi Morano anasema huenda limechangia maisha yake marefu, ni hatua yake ya kumfukuza mumewe mwaka 1938 baada ya mtoto wake wa kiume kufariki akiwa na miezi sita pekee.
Ndoa yao ilikuwa inaendelea vyema kwa mujibu wa Bi Morano.
Alikuwa amempenda mvulana aliyeuawa wakati wa Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na hakutaka kumuoa mtu mwingine.
Lakini aliambia gazeti la La Stampa, alipokuwa na miaka 112, kwamba hakuna na namna nyingine ya kufanya ila kuoa mtu mwingine.
"Aliniambia: 'Ukiwa na bahati utanioa, la sivyo nitakuua'. Nilikuwa na miaka 26. Niliolewa."
Baadaye, ndoa yao ilianza kuvurugika na akamfukuza mumewe ingawa hawakuvunja ndoa yao hadi mwaka 1978 mumewe alipofariki.
Bi Morano alifanya kazi hadi alipotimu miaka 75 na aliamua kutooa tena.
"Sitaki kudhibitiwa na yeyote," aliambia gazeti la New York Times.
Ili kusherehekea siku hii muhimu, wakazi wa eneo la Pallanza karibu na Ziwa Maggiore, ambapo amekuwa akiishi, wanaandaa maonyesho ya mitindo yakiangazia karne tatu katika historia.
Profesa wa masuala ya msambojeni George Church ambaye hufanya kazi katika chuo cha matibabu cha Harvard pamoja na kundi lake la watafiti ambao wamekuwa wakifanya utafiti kuhusu umri wa kuishi, ameambia BBC kwamba binadamu wataendelea kuongeza muda wa kuishi.
"Nafikiri tutashuhudia ongezeko kubwa la muda wa kuishi katika miaka michache iliyopita kutokana na teknolojia, na pia utafiti unaofanyiwa watu wa kipekee kama vile Emma."
Emma bado yuko buheri wa afya.
Hata hivyo, hajaondoka nyumba yake ya vyumba viwili kwa miaka 20.
Carlo anahisi shinikizo kuhusu majukumu ya kumtunza mwanamke huyo mkongwe, ambapo anasema ni kama kuutunza Mnara wa Pisa.
"Ile siku utaanguka, kuna mtu atalaumiwa," aliambia AFP. "Emma atakapofariki, mimi ndiye nitakayewajibishwa."
Mtu aliyeishi muda mrefu zaidi duniani kwa mujibu wa Guinness alikuwa Mfaransa Jeanne Calment, aliyeishi miaka 122 na siku 164. Alifariki Agosti 1997.
No comments:
Post a Comment