Usalama wa Wanawake kufuatia Mabadiliko ya Tabia Nchi
Ukatili dhidi ya wanawake ni
uvunjaji mkubwa wa haki za msingi za binadamu na tishio kwa mamilioni ya
wasichana na wanawake duniani kote. Takribani mwanamke mmoja kati ya
wanawake watatu duniani amekuwa akipigwa, kulazimishwa kufanya ngono, au
kunyanyaswa vinginevyo katika maisha yake. Jamii nzima imeathiriwa na
ukatili ambao unaweza kuwa wa kimwili, kingono (unyanyasaji,
kulazimishwa au kubaguliwa) na kisaikolojia (kunyanyaswa kwa maneno au
kwa hisia, kama vile kuonewa au kutengwa).
Katika siku hii ya Kimataifa ya
Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake, UNESCO inaangazia mabadiliko ya
tabia nchi na uhaba wa rasilimali kama sababu za kuchochea ukatili dhidi
ya wanawake – nyumbani, mitaani, wakati wa majanga asilia
yanayosababishwa na tabia nchi.
Mabadiliko ya tabia nchi
yanazidisha tishio – yanaweza kuongeza uhamaji na kukosa makazi kwa watu
na kuchangia katika kutokuzalishwa kwa mazao au mafuriko, kuongeza
msukumo nyumbani na katika utafutaji wa riziki. Utafiti unaonyesha
kwamba wanawake wanawajibika kwa asilimia 65 ya uzalishaji wa chakula
katika kaya huko Asia, kwa asilimia 75 katika nchi za Kusini mwa Jangwa
la Sahara na kwa asilimia 45 huko Amerika ya Kusini. Mara nyingi, ni
wajibu wa kiutamaduni wa wanawake unaowaweka katika hatari kubwa dhidi
ya madhara ya mabadiliko ya tabia nchi – na kwa hiyo kujikuta wakiwa
katika mazingira yenye uwezekano wa kufanyiwa ukatili wanavyotembea
maili nyingi kila siku kutafuta chakula, maji na kuni au baada ya kukosa
makazi au kupata umasikini kutokana na majanga. Kukosa njia za
kujitafutia riziki na umasikini kunaweza pia kusababisha ukatili
nyumbani kutokana na msukumo wa kiuchumi, pamoja na kuendelea kwa muda
mrefu kwa mienendo ya ukeketaji wa wanawake na ndoa za utotoni.
UNESCO inashiriki kikamilifu
katika kuimarisha ujasiri wa kukabili mabadiliko ya tabia nchi,
ujumuishaji wa mkabala wa kijinsia katika utendaji wake wote. Kwa
kutumia ushirikiano na mipango ya kibunifu, UNESCO inaendeleza fikra
inayodai kuwa wanawake na wasichana ni muhimu katika kukabiliana na
mabadiliko ya tabia nchi, hasa, kwa mfano, mipango ya kusimamia maji na
utayari wa kukabiliana na majanga.
Tunafahamu kwamba uzalishaji wa
gesi ukaa unaiathiri sayari ya dunia. Tunapaswa pia tutambue kwamba
mabadiliko ya tabia nchi yanaathiri maisha ya wasichana na wanawake
duniani kote. Tunapokuwa tupo tayari kuanza kutekeleza Mkataba wa Tabia
Nchi wa Paris na kujiandaa kwa ajili ya mafanikio ya COP22 huko
Marrekech, tusiisahau nusu ya idadi ya watu wetu na uwezo wao mkubwa
wanaouwakilisha. Wanawake lazima wawe katika kiini cha utatuzi wote wa
mabadiliko ya tabia nchi.
No comments:
Post a Comment