Ivo Mapunda ambaye ni golikipa wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania na
vilabu vikongwe nchini vya Simba na Yanga ameamua kurejesha uwezo wake
uwanjani kwa kuwajenga vijana wadogo kwa kwa ajili ya siku za baadaye
baada ya kuanzisha kituo chake cha kuibua vipaji maeneo ya
Kitunda-Mwanagati.
Mapunda ambaye kwa sasa hachezi mechi za kiushindani tangu alipoachwa na
Azam FC baada ya mkataba wake wa muda mfupi kumalizika amekuwa nyumbani
tangu kuanza kwa msimu huu wa VPL 2016-17.
Golikipa huyo aliyepata kucheza soka la kulipwa kwenye vilabu vya
Ethiopia na Kenya kabla ya kurejea tena Tanzania amesema, lengo la
kuanzisha kituo hicho ni kusaidia vijana ambao hawana kazi za kufanya na
huenda ikawa ni fursa kwao kupata ajira kupitia vipaji vyao.
“Nimeandaa ufunguzi wa kituo changu cha michezo kitakuwa kinaitwa Ivo
Mapunda Sports Center, ni kituo ambacho kitakuwa kinachukua vijana
wadogo kuanzia miaka 5 hadi 18 na hii nimeifanya ili kujaribu kuibua
vipaji kwa watoto wadogo kwasababu sasahivi limekuwa tatizo kwa vijana
kupata ajira na sehemu za kucheza,” anasema golikipa huyo wa zamani wa
Taifa Stars aliyepata kuvitumikia vilabu vya Simba na Yanga kwa nyakati
tofauti.
“Kwa eneo ambalo nakaa mimi nimeona kuna vijana wengi ambao hawana
shughuli za kufanya sasa nimeamua nifungue hiki kituo kuwapa fursa ya
kuonesha vipaji vyao. Tayari nimeshapata eneo kutoka serikali za mitaa
na natarajia kufanya ufunguzi rasmi Novemba 26 mwaka huu siku ya
Jumamosi ijayo,” alifafanua Mapunda ambaye amesema kituo kitakuwa
Kitunda-Mwanagati.
“Utaratibu wa namna ya kujiunga utafahamika siku hiyohiyo ya ufunguzi pamoja na mambo mengine mengi.”
Tangu Ivo alipomaliza mkataba wake na Azam hajatangaza kustaafu soka la
ushindani lakini huenda aliamua kustaafu kucheza soka bila kutangaza.
No comments:
Post a Comment