Kutoka mezani kwangu Moses Joseph Machali, Tarehe: 21/11/2016
W
Napenda kuutaarifu umma wa Watanzania kupitia kwenu waandishi wa habari
kwamba ni jambo la ajabu na aibu kwa watu makini na wenye kuhitaji
mabadiliko ya kweli Kuacha kuunga Mkono juhudi zinazofanywa na serikali
ya awamu ya tano chini Uongozi wa Rais Dr. John Pombe Joseph Magufuli
bila kusahau utendaji makini wa Waziri Mkuu wake Mhe. Majaliwa Kasim
Majaliwa (Mb) pamoja na mawaziri mbalimbali wameonesha kutaka kufuata
mwenendo wa Rais Magufuli na Waziri Mkuu wake.
Mimi Moses Joseph Machali niliyefanya sana siasa za Upinzani hapa nchini
na niliyepiga kelele na kupinga siasa za kifisadi zilizoitawala nchi
hii; niliyepinga pia ufisadi uliokuwa umeitawala serikali huko nyuma kwa
nguvu na uwezo wangu wote nikishirikiana na wapinzani wenzangu,
ninaamua kujiunga na watu wanaonesha dhamira safi ya kuiendeleza nchi
yetu Tanzania. Watu wenye mwelekeo na dhamira ya kuijenga nchi yetu kwa
maendeleo enedelevu ni jamii ya akina Magufuli, Kasim Majaliwa, nk.
Mwaka mmoja wa Uongozi wa Rais Magufuli na baadhi ya wasaidizi wake
kupitia hatua mbalimbali zilizochukuliwa dhidi ya ufisadi uliokuwa
umeigubika nchi yetu, inatosha kabisa kwa mtu yeyote makini kufanya
uamuzi wa kumuunga mkono au kutokumuunga mkono Rais Magufuli.
Mimi nimechagua kumuunga Mkono Rais kwa vitendo, kwa sababu ninaposoma
Rekodi yangu ya enzi nikiwa Mbunge (Hansard) na kabla ya kuwa mbunge ni
kwamba nilipinga mnoo wizi na ufisadi wa kila aina; Nilipinga Matumizi
ya fedha serikalini yasiyo ya lazima na yasiyo na tija kwa taifa
(Rejeeni hotuba yangu ya Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi, nikiwa Waziri
Kivuli wa wizara hiyo ya mwaka 2014/2015 na 2015/2016), vilevile bila
kusahau hotuba zangu mbalimbali Bungeni na nje ya Bunge.
Kwa kushirikiana na wapinzania wenzangu enzi hizo tulishauri na kupinga
ufisadi wa kila aina, tuliitaka serikali kufanya mambo yenye tija kwa
taifa na sasa kila mwenye macho anaona hatua zinazochukuliwa na serikali
ya awamu ya tano. Miradi kama ya Ujenzi wa Reli, Ununuzi wa ndege mbili
na mipango ya kununua ndege zaidi kama namna ya kulifufua shirikia la
ATCL ni mambo tuliyoyahitaji kuyaona wapinzani; sasa yanafanyika. Wale
wenye dhamira ya dhati ya kuona nchi yetu ikipiga hatua, kamwe hatuwezi
kubeza mambo hayo bali kuyaunga mkono.
Wale tuliosema na kupiga kelele kwamba Serikali ni dhaifu ktk
kuwachukulia hatua watu mbalimbali wenye dhamana serikalini walioonekana
kufanya vibaya serikalini ktk nafasi zao, leo tunaona kumekuwepo na
kasi nzuri ktk kuwachukulia hatua watu hao. Hata hivyo leo hii upinzani
umepiteza mwelekeo kwa sababu unapingana na kile ulichokihubiri nchini.
Agenda ya kupinga ufisadi siyo ya upinzani tena bali ya JPM na CCM yake
au yao. Wapinzani wamegeuka kuwa watu wanaokataa yale waliyoyasimamia na
kuyahubiri huko nyuma. Hakika huo siyo uungwana bali aina mpya ya
ufisadi nchini na usaliti kwa agenda zao.
Kama kweli sisi tumeokuwa wapinzani na tulioonesha kupinga kwa nguvu
zote ufisadi ulioiumiza nchi hii tulimaanisha yale tuliyoyahubiri na
kuwaaminisha watu basi tunao wajibu wa kuacha tabia ya kuwa vigeugeu kwa
mambo tuliyoyaamini na kuyahubiri. Kutofanya hivyo basi ni mwendelezo
wa ufisadi kwa maslahi binafsi.
Ni nani asiyeona kwamba serikali ya awamu ya tano inafanyia kazi mambo
mengi tuliyoyapigia kelele? Au tunajifanya kutokukubali ukweli unaoishi
kwa ule msingi wa upinzani wa Tanzania kwamba Tukimuunga mkono Mtawala
kamwe hatutapata kuaminiwa na wapiga kura nchini na hivyo tupinge tu
hata kama ni ukweli? Nadhani kinachofanyika ni mwendelezo wa kupinga
hata mazuri ili kutafuta fursa ya wapinzani kukubalika kisiasa zaidi
hata kwa njia na mbinu haramu kama kawaida ya siasa zilizo zoeleka hapa
nchini kwa miaka mingi.
Taifa hili haliwezi kuendelea kwa kuwa na siasa za kutokukubaliana na
ukweli unaoishi. Kama dhamira ya kila mtanzania ikiwemo wapinzani ni
kuona nchi ina move basi hatuhitaji kuwa watu wa kupingapinga hata
yaliyo mema bali kuyaunga mkono yale yaliyo mema bila kujali yanafanywa
na nani bali msingi mzuri unapaswa kuwa ukweli kwa kila jambo.
Serikali ya awamu ya tano imeonesha njia ktk mambo mengi na inastahili
kuungwa mkono. Safari ni hatua na ninaamini kwamba hata yale
yanayoonekana kutokufanyiwa kazi ndani ya mwaka mmoja uliopita na ambayo
yalishindikana huko nyuma, bado yanaweza kuja kufanyiwa kazi huko
mbeleni. Serikali ya JPM imejitahidi sana tukilinganisha na huko tuliko
toka. Uongozi huu unafanana sana na ule wa akina Hayati EDAWARD MORINGE
SOKOINE chini ya hayati Baba wa Taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere.
Daima ninaamini ktk yale ninayoyaamini pasipo kufungwa na ukada bali
kuangalia ukweli ni upi. Hata kelele wanazopiga baadhi ya watu kwamba
maisha yamekuwa magumu kwa sababu ya Magufuli ni propaganda tu kwa
sababu hakuna uhusiano wa maisha magumu na suala la KUDHIBITI wapiga
dili wa fedha na mali za umma bali tukubali kwamba wapiga dili waliozoea
kupiga dili na kuziingiza fedha walizopiga ktk mzunguko kwamba siyo
jambo la msingi ktk kujenga uchumi imara.
Uchumi imara hauwezi kujengwa kwa kuruhusu ubadhirifu wa fedha na mali
za umma au hata za mtu mmoja mmoja. Kinachoonekana hivi sasa ni kama
nchi inasukwa upya na hivyo tuwaunge mkono viongozi wa serikali ya awamu
ya tano kwa mema wanayoyafanya na kuwashauri kurekebisha ktk yale
ambayo hayajakaa vizuri. Tuachane na siasa nyepesi za kutaka kuona
kwamba mazuri ni yale yanayofanywa na wapinzani huku mambo hayohayo
yakifanywa na CCM yaonekane hayafai na kutajwa kuwa ni ya hovyo. CCM ya
JPM siyo ile ya 2015 kurudi nyuma kidogo. Hii ni tofauti na ninaiunga
mkono.
Hivyo basi leo Tarehe 21/11/2016 ninatangaza rasmi kwamba ninajiunga na
timu JPM kwa maslahi ya taifa kwa kuwa sioni sababu ya kupingana na yale
niliyoyapigania na itakuwa ni sawa na mtu kupigana na kivuli chake
mwenyewe. Kwaherini Upinzani nimeamua kuanza siasa mpya za masuala yale
niliyoyaamini na ninayoyaamini. Imani ni Matendo Na Matendo ni imani.
Piga vita ufisadi kwa imani na Matendo.
Moses Joseph Machali
X-mbunge, Kasulu Mjini 2010-2015,
No comments:
Post a Comment