Tuesday, 29 November 2016

Watumishi wa TAKUKURU Waliotumbuliwa tangu Mwaka jana Kwa Kukiuka Agizo la Rais Warejeshwa Kazini

Watumishi waandamizi wanne wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) waliosimamishwa kazi baada ya kusafiri nje ya nchi kinyume na agizo la Rais John Magufuli, wamerejeshwa kazini baada ya takriban mwaka mmoja kupita.
Msemaji wa Takukuru, Mussa Misalaba aliwataja watumishi hao kuwa ni Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma, Mary Mosha na Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Ekwabi Mujungu ambao wamerejeshwa baada ya shauri lao kusikilizwa na ofisi husika.
“Shauri lao lilishughulikiwa na Ofisi ya Rais kutokana na vyeo vyao, wamerejeshwa ofisini na kuanza kazi Novemba 14,” alisema.



Misalaba alisema watumishi wengine waliorejeshwa kazini ni aliyekuwa Msemaji wa Takukuru, Doreen Kapwani na Katibu Muhtasi wa mkurugenzi mkuu, Rukia Nikitas shauri lao lilisikilizwa na mamlaka ya taasisi hiyo na hatua za kinidhamu zilichukuliwa ikiwamo kuhamishwa vitengo.
Watumishi hao walidaiwa kuondoka nchini Novemba 23 mwaka jana, kabla ya kupewa majibu ya vibali walivyoomba baada ya kuandika barua Ikulu kuhusu safari hiyo.
Rais Magufuli alitangaza kufuta safari za nje ya nchi kwa maofisa wa Serikali Novemba 7, 2015 na kutoa mwongozo kwamba safari zitakazoruhusiwa ni zile zenye ruhusa ya Ikulu.
Kusimamishwa kwao kazi kulitangazwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alipozungumza na waandishi wa habari Desemba 16 mwaka jana.
Takukuru iliiandikia Ikulu barua ya kuomba kibali kwa ajili ya safari hiyo, lakini kabla ya kujibiwa, wafanyakazi hao waliamua kusafiri.

No comments:

Post a Comment