Yanga imeonyesha haitaki kusubiri mambo yaende yasivyo baada ya kuona
mkataba wa mshambuliaji wake nyota Amissi Tambwe unakwenda ukingoni,
kwani tayari imeanza kumuandalia mkataba mpya ili imalizane naye,
mapemaa.
Mrundi huyo aliyetua Jangwani Desemba 15, 2014 akitokea Simba, amebakiza
miezi sita kabla ya kumaliza mkataba wake na Yanga. Kwa mujibu wa
kanuni za Fifa, anaruhusiwa kuanza mazungumzo na timu nyingine.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alisema ni vigumu kumuachia
mshambuliaji huyo aondoke kwenye timu hiyo na badala yake watamuongezea
mkataba mwingine wakati wowote.
Sanga alihoji itawezekana vipi kumuachia mshambuliaji mwenye uwezo
mkubwa wa kufunga mabao! Hivyo hizo timu zinazopiga hesabu za kumsajili
nyota huyo, zifute ndoto hizo.
Aliongeza kuwa, uongozi huo umepanga kukaa naye meza moja kwa ajili ya
kuujadili mkataba mpya katika kuhakikisha anabaki kuendelea kuichezea
Yanga kwa misimu mingine miwili.
"Ujue tutaonekana watu wa ajabu kumuachia Tambwe aondoke kwenye timu
yetu, utamuachaje mshambuliaji anayeifungia timu mabao? Haitoshi ana
rekodi nzuri ya kuwa mfungaji bora mara mbili kwenye misimu tofauti
kwenye ligi kuu.
"Hivyo, Wanayanga wala wasiogopeshwe na vitisho kutoka kwa wapinzani
wao, Tambwe atabaki kuichezea Yanga kwenye misimu mingine ijayo ya ligi
kuu, ninaamini kila mtu anajua uwezo wake wa kufunga mabao.
“Tumepanga kukutana hivi karibuni kwa ajili ya kuujadili mkataba mpya na
kikubwa ni dau la usajili na malipo ya mshahara ambao tumepanga
kumboreshea ili tumshawishi abaki Yanga,” alisema Sanga.
No comments:
Post a Comment