Tuesday, 1 March 2016

Wataalamu TPRI Wapelekwa Kilombero kufanya Uchunguzi

dk rutNa Dustan Kamala
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro imewapeleka wataalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Viuwatilifu ya Kitropiki (TPRI) wilayani Kilombero kufanya uchunguzi wa zao la mpunga linalosadikiwa kuharibiwa na dawa zilizomwagwa na Kampuni ya Kilombero Plantation (KPL) inayomiliki mashamba yanayopakana na mashamba ya wananchi.
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Idara ya Uchumi na Uzalishaji Mali Mkoa wa Morogoro Bw. Ernest Mkongo kuhusu uchunguzi unaoendelea kufanyika katika mashamba ya wananchi ili kutathmini athari zinazotokana na dawa hizo.
“Wataalamu kutoka TPRI wameshafanya uchunguzi wa awali na mpunga huo umeonekana kuwa na rangi ya njano isivyo kawaida, hivyo wamechukua sampuli za mpunga huo na kuzipeleka maabara kwa ajili ya uchunguzi zaidi ili kujua kama umeharibiwa na dawa za kuondoa magugu zilizomwagwa na Kampuni ya KPL” alisema Mkongo 
Aidha, Bw. Mkongo ameongeza kuwa, Taasisi ya TPRI ina wataalamu wa uhakika kwa hiyo anaamini watatoa majibu ya ukweli juu ya tatizo hilo.
TPRI ilianzishwa miaka ya 1940 ambapo kwa Tanzania ilirasimishwa rasmi katika Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Sheria Na. 18 ya mwaka 1979 kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa dawa zinazoathiri afya ya binadamu, wanyama na mazao.

Serikali yawapa motisha wachezaji wa Twiga Stars

TWI1
Baadhi ya wachezaji wa Timu ya Taifa ya mpira wa miguu wanawake “Twiga Stars” wakimsikiliza Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Annastazia James Wambura (hayupo pichani) alipowatembelea kambini kwao leo jijini Dar es Salaam.Twiga Stars inatarajiwa kucheza mechi na Timu ya Taifa wanawake ya Zimbabwe mchezo utakaochezwa tarehe 4 katika uwanjja wa Taifa.
Picha na WHUSM
TWI2
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Annastazia James Wambura akizungumza na wachezaji wa Timu ya Taifa ya mpira wa Miguu wanawake “Twiga Stars” alipowatembelea kambini kwa leo jijini Dar es Salaam. Katikati ni Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Makoye Nkenyenge na Mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa BMT Bi. Jeniffer Mmasi Shang’a (kulia).
TWI3
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Selestine Mwesiga akitoa shukura kwa Serikali kutokana na jitihada zake za kuitafutia wadhamini Timu ya Taifa ya Mpira wa miguu wanawake (Twiga Stars) wakati Naibu Waziri wa Habari, Utamduni, Sanaa na Michezo Mhe. Annastazia James Wambura(wapili kutoka kushoto) alipo watembelea wachezaji wa Timu hiyo leo jijini Dar es Salaam.Kutoka kulia ni Mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa BMT Bi. Jeniffer Mmasi Shang’a (kulia). Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Makoye Nkenyenge.
TWI4
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Annastazia James Wambura akisalimiana na Kocha wa Timu ya Taifa ya mpira wa Miguu wanawake “Twiga Stars” (Nasra Juma) alipowatembelea kambini kwao leo jijini Dar es Salaam. Katikati ni mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bi. Jeniffer Mmasi Shang’a.
TWI5
Mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bi. Jeniffer Mmasi Shang’a. akisalimiana na Kocha wa Timu ya Taifa ya mpira wa Miguu wanawake “Twiga Stars”  Bibi. Nasra Juma  wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Annastazia James Wambura (hayupo pichani) kambini kwao leo jijini Dar es Salaam.

Na: Chrispino Mpinge
Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imetoa motisha kwa wachezaji wa Timu ya Taifa ya mpira wa miguu wanawake(Twiga Stars) ikishinda katika mchezo wake dhidi ya Zimbabwe unatarajiwa kuchezwa siku ya Ijumaa tarehe 4 machi katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.

Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Annastazia James Wambula alipotembelea kambi ya Timu hiyo leo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na wachezaji wa Twiga Stars, Wambura amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa michezo wamekusanya shilingi milioni 15 ambazo zitatumika kama motisha kwa wachezaji hao.

Naibu Waziri huyo aliongeza kuwa iwapo timu hiyo itaibuka na ushindi katika mechi yake Dhidi ya Zimbabwe kila mchezaji atapata gawio la sh. Laki tatu kama mptisha na kuongeza kuwa itafanyika hivyo hivyo katika mchezo wa marudiano utakaochezwa nchini Zimbabwe.

Aidha alitumia fursa hiyo kuwaomba wadau wa michezo kuzidi kujitokeza na kuisaidi timu hiyo ikiwa ni pamoja na kuhudhuria kwa wingi katika mechi ya tarehe 4 machi dhidi ya Zimbabwe itakayochezwa katika uwanja wa Taifa.

Aliongeza kuwa msaada zaidi unahitajika ili kuiwezesha timu hiyo kukidhi mahitaji yake Muhimu,hivyo alitoa wito kwa wadau mbalimbali kutoa michango yao kupitia Twiga Specila Fund, Akaunti na: 20110001677 iliyoko NMB tawi la Bank House jijjini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TFF Selestine Mwesiga ameipongeza Serikali kwa jitihada Zake za kuhakikisha Twiga Stars inapata huduma muhimu ikiwemo motisha kwa wachezaji na benchi la ufundi.

Mwesiga pia amewapongeza wadau wote waliojitolea kusaidi timu hiyo ambapo amesema kujitokeza kwa wadau hao kunaongeza morali ya wachezaji.

Msaada huo wa shilingi milioni 15 umetolewa na wadau watatu ambapo mmoja aliyechangia sh. Milioni 3 aliomba jina lake lihifadhiwe, wengine ni Kampuni ya ASAS sh. Milioni 2 na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) sh. Milioni 10.

No comments:

Post a Comment