TAHADHARI KUHUSU UGONJWA WA KIMETA NA MAGONJWA MENGINE YATOKANAYO NA WANYAMA
Wizara
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inapenda kutoa
taarifa kwa jamii kuchukua tahadhari ya magonjwa yanayoenezwa kutoka kwa
wanyama kwenda kwa binadamu. Magonjwa hayo ni kama kimeta, homa ya
malale, tauni, homa ya bonde la ufa, kichaa cha mbwa, mafua makali ya
ndege n.k.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na timu ya Mkoa na Wilaya ilifanya uchunguzi na kubaini kuwa watu 23 waliugua na walihusika moja kwa moja katika uchinjaji au upishi wa nyama za ng’ombe wagonjwa au waliokufa waligundulika kuwa na dalili za ugonjwa wa Kimeta.
Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na:
Timu ya wataalamu wa afya kutoka ngazi ya Taifa walikwenda kushirikiana na timu ya mkoa na wilaya husika katika uchunguzi na udhibiti wa ugonjwa
Ufuatiliaji wa waliokula nyama ya ng’ombe waliougua au kufa ulifanyika ambapo wote wamepata dawa za kinga, jumla ya watu 904 walihusishwa na kula nyama za ng’ombe waliokwishakufa (Wilaya ya Siha= 836, na Wilaya ya Moshi Vijijini=68)
Elimu ya afya kwa jamii jinsi ya kujikinga na ugonjwa huu
Kunyunyuzia dawa ya kuua bakteria wanaoeneza ugonjwa katika maeneo ya kufugia au kuchinjia wanyama
Kutoa elimu na kufanya ufuatiliaji wa mabucha yote ya nyama ambayo yanahusika na uuzaji wa nyama za ng’ombe waliokufa
Elimu kuhusu umuhimu wa chanjo kwa Mifug
Namna ya kuzuia Kimeta
Ugonjwa wa Kimeta unasababishwa na aina ya bakteria aitwaye Bacillus anthracis ambaye anashambulia wanyama mwitu, wafugwao pamoja na binadamu. Ugonjwa huo unaambukizwa kutoka mnyama kwenda kwa binadamu au kutoka binadamu mmoja kwenda mwingine au kwa njia ya:
kugusa nyama, damu na majimaji kutoka kwa mnyama au mwilini mwa mtu aliyeambukizwa ugonjwa huo
kula nyama ya mnyama aliye mgonjwa hasa ambayo haijaiva vizuri
Kuvuta vumbi kutoka lenye vimelea vilivyotoka kwa mnyama mgonjwa
Wizara inatoa rai kwa jamii kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huu ambazo ni pamoja na:
Epuka kula nyama inayotokana na mnyama aliye mgonjwa au aliyekufa
Tumia nyama iliyothibitishwa na mtaalamu wa mifugo
Toa taarifa kwa wataalamu wa mifugo kuhusu wanyama wagonjwa au vifo vya wanyama
Epuka kugusa nyama, damu na majimaji kutoka kwa mnyama au mwilini mwa mtu aliyeambukizwa ugonjwa huo bila vifaa kinga
Epuka kula nayama ambayo haijaiva vizuri
Toa chanjo kwa wanyama wafugwao
Hitimisho
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto itaendelea kushirikiana na sekta ya mifugo na nyingine ili kuimarisha mikakati ya kudhibiti magojwa ya nayoenezwa kutoka kwa mifugo kwenda kwa binadamu kama magonjwa ya kimeta, homa ya malale, tauni, homa ya bonde la ufa, kiachaa cha mbwa, mafua makali ya ndege n.k. Jamii inaaswa kuzingatia maagizo yanayotolewa na wataalamu wa afya pamoja na wa mifugo ili kujikinga na magonjwa hayo na mara waonapo dalili za magongwa hayo watoe taarifa mapema.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
04 Machi, 2016
No comments:
Post a Comment