Tuesday, 15 March 2016

Serikali Kudhibiti Uagizaji Sukari:Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

JILWaziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kudhibiti uagizaji wa sukari kutoka nje ili kulinda soko la ndani.

Ametoa kauli hiyo jana (Jumatatu, Machi 14, 2016) wakati akizungumza na uongozi wa kiwanda Cha sukari cha Kagera pamoja na uongozi wa mkoa wa Kagera alipotembelea kiwanda hicho Ambapo alisema wamezuia sukari kutoka nje ili kuhakikisha sukari inaisha katika maghala yao.
Akiwa katika siku ya pili ya ziara yake mkoani Kagera, Waziri Mkuu ameviagiza viwanda kuzalisha sukari nchini vizalishe sukari ya kutosha ili kukidhi mahitaji ya soko.

Alisema mahitaji halisi ya sukari hapa nchini ni tani 420,000 huku uwezo wa viwanda vya ndani ni kuzalisha tani 300,000 hivyo alitoa wito kwa viwanda hivyo kuongeza uzalishaji.
“Tunahitaji viwanda vya ndani vizalishe sukari ya kutosha na mahitaji yawe yamefikiwa kama Tulivyokubaliana, lengo ni kuzuia uagizaji wa sukari kutoka nje ambao ukiendelea utavivuruga viwanda vya ndani,” alisema.

Pia alivitaka viwanda hivyo viwe vimefikia malengo ya kuzalisha sukari ya kutosha katika kipindi Cha kuanzia miaka mitatu hadi minne kama walivyokubaliana katika kikao cha wadau wa sukari nchini kilichofanyika hivi karibuni.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliupongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika mashamba ya miwa, ununuzi wa mitambo pamoja na kuajiri idadi kubwa ya watumishi ambao ni Watanzania.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa kiwanda hicho, Bw. Ash Rana alisema kwa sasa wanazalisha tani 60,000 za sukari na kwamba wana lengo la kuzalisha tani 120,000 katika kipindi cha miaka minne ijayo.
Alisema uzalishaji wa sukari kiwandani hapo umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka ambapo mwaka wa fedha wa 2011/2012 walizalisha tani 35,362 na mwaka 2015/2016 wamezalisha tani 60,000.

Ofisa huyo aliiomba Serikali ipunguze riba ya mikopo ya kwenye uwekezaji wa sekta ya kilimo ambapo kwa sasa wanatozwa asilimia 20 kiwango ambacho alisema ni kikubwa sana.
Alisema wana mipango ya kukiboresha na kukipanua zaidi kiwanda hicho na hivi sasa wako katika hatua za mwisho za kupata mkopo wa Dola za Marekani milioni 68 ambao kati ya hizo, dola milioni 10 zitapelewa katika uboreshaji wa umwagiliaji na zilizobaki katika kuimarisha miundombinu ya kiwanda hicho.
IMETOLEWA NA: OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, MACHI 15, 2016.

No comments:

Post a Comment