Tuesday, 1 March 2016

Kuziona Twiga Stars na Zimbabwe 2000

Kiingilio cha chini cha mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika kwa Wanawake kati ya timu ya Taifa ya Tanzania ya Wanawake ‘Taifa Stars’ dhidi ya timu ya taifa ya wanawake Zimbambwe kitakua shilingi elfu mbili tu.

Mchezo huo namba 3, unatarajiwa kuchezwa siku ya Ijumaa saa 10 kamili jioni katika uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, huku kiingilio cha juu kikiwa shilingi elfu tatu kwa jukwaa kuuu.
Waamuzi wa mchezo huo ni Lidya Tafesse, akisaidiwa na Yehuzewdubizua Yehuw, Tsige Sisay, Woinshetkassaye Abera kutoka nchini Ethiopia, huku Kamisaa wa mchezo huo Geneviev Kanjika akitoka Congo DR wote wanatarajiwa kuwasili siku ya Alhamisi mchana kwa shirika la ndege la Kenya (KQ).
Wakati huo huo kikosi cha Twiga Stars kimeendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo huo wa siku ya Ijumaa, huku kocha mkuu wa timu hiyo Nasra Juma akisema vijana wake wote wapo katika hali nzuri na tayari kuwakabili Wazimbambwe.
Aidha Kocha Nasra amewaomba wadau wa mpira wa miguu nchini na watanzania wote kwa ujumla, kujitokeza uwanjani siku ya Ijumaa kuja kuwapa sapoti katika mchezo huo, ambapo watakua wakiwakilisha na kupeperusha bendera ya Tanzania.

JAFO AMUAGIZA MKURUGENZI WA KISARAWE KUMTAFUTIA KAZI NYINGINE MENJEJA WA MAMLAKA YA BODI YA MAJI

Jafo-30Jan2016
Na Tabu Mullah
 NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Utumishi na Utawala bora,  Seleman Jafo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kisarawe kumtafutia kazi nyingine meneja wa Mamlaka ya Bodi ya Maji Kisarawe Listern Materu kutokana na kushindwa kutatua kero ya maji kwa muda mrefu.

 Jafo ambae pia ni mbunge wa jimbo la Kisarawe alisema, hawawezi kuendelea kukaa na watumishi ambao hawaguswi na matatizo ya wananchi.
 Alitoa agizo hilo juzi mjini Kisarawe, kwenye mkutano aliouandaa kwa ajili ya kuwashukuru wananchi kwa kumpa ridhaa ya kuendelea kuongoza jimbo hilo, na kusikiliza kero zinazowakabili wananchi hao.

 Naibu Waziri huyo alimtaka Materu kuachia nafasi ya Meneja ili apangiwe kazi nyingine kwani ameshindwa kutatua changamoto ya maji katika mji wa Kisarawe.
 “Mkurugenzi mtafutie kazi nyingine katika ofisi yako, hatuwezi kuwa na watu ambao hawaguswi na matatizo ya watu tafuta atakayekaimu nafasi yake katika kipindi hiki.
 Hatufanyi mambo ya kuchekeana, na hatuwezi kuibadilisha  Kisarawe yetu kama tutaendelea kuwavumili watumishi wanaochangia kudumaza maendeleo”alisema Jafo.
 Inadaiwa kuwa, Materu amekua meneja wa Mamlaka hiyo kwa zaidi ya miaka kumi lakini hakuna njia mbadala iliyobuniwa na mamlaka hiyo kuondoa tatizo la maji kukosekana mara kwa mara.
 Mji huo wa Kisarawe una chanzo cha maji cha kimani ambacho kinatoa lita 16000 kwa saa na chanzo kingine cha minaki kinachotoa zaid ya lita 10,000 kwa saa hali ambayo ni dhahiri kusingekuwepo na tatizo la  maji.

 Wananchi waliohudhuria katika mkutano huo walifurahishwa na kitendo kilichofanywa na mbunge wao huku wakiendelea kumuomba ahamie katika idara ya ardhi.

 Mwajuma Yusuph, Salehe Ally na Said Issa walisema kitendo cha kuondolewa Meneja huyo kitaleta mabadiliko kwani baadhi ya watumishi wanafanya kazi kwa mazoea bila kujali adha inayowapata wananchi.

Profesa MAYUNGA HABIBU NKUNYA ateuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC)


maxresdefaultWaziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa kwa Mamlaka aliyopewa amemteua Profesa MAYUNGA HABIBU NKUNYA kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) kuanzia Februari 17, 2016.

Uteuzi huo ni wa miaka mitatu kuanzia tarehe 17 Februari, 2016 hadi 16 Februari, 2019.
Kabla ya uteuzi huo Profesa Nkunya alikuwa ni Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Programu ya Mapitio ya Mfumo wa Taifa wa Ubunifu (National Innovation System Review Programme).

Uteuzi huo unafuatia kumalizika kwa muda wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo.  
Taarifa hii imetolewa na,
Eng. Joseph M. Nyamhanga
KATIBU MKUU (UJENZI),
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
01 Machi, 2016

No comments:

Post a Comment