Baada ya kudumu Ikulu kwa takribani siku 127 zikiwamo 67 tangu aongezewe
muda wa mwaka moja akiwa na Serikali ya Awamu ya Tano, Balozi Ombeni
Sefue ameshukuru heshima aliyopewa na Rais John Magufuli kwa muda wote
aliomsaidia kutekeleza majukumu yake ya ukatibu mkuu kiongozi na kueleza
kuwa Serikali ya sasa ni ya mabadiliko.
Wakati Sefue akiondoka,
mhandisi John Kijazi amepokea kijiti cha ukuu wa utumishi serikalini na
kuahidi kuwa atafuatilia mazingira ya watumishi wote pamoja na mazingira
yao, ili kurekebisha panapohitajika kwa lengo la kuongeza uwajibikaji
na tija kwa wananchi.
Akizungumza muda mfupi baada ya kuapishwa
kwa mrithi wake, licha ya kumshukuru Rais, Balozi Sefue aliwataka
watendaji wote serikalini kumpa ushirikiano wa kutosha Balozi Kijazi ili
kuleta ufanisi kwenye huduma za umma.
“Namshukuru Rais kwa
kuniamini kwa kipindi chote nilichodumu naye. Ni heshima kubwa
kuwatumikia Watanzania pamoja naye. Nitampa ushirikiano wowote
atakaouhitaji katibu mkuu kiongozi mpya kwenye utekelezaji wa majukumu
yake,” alisema Sefue.
Rais Magufuli, ameahidi na mara zote
amekuwa akisisitiza adhma yake ya kutumbua majipu kwa watumishi wote
ambao hawaendani na kasi yake.
Tangu taarifa za mabadilio hayo
zilipotangazwa jana, kumekuwepo na tetesi nyingi kuwa huenda Sefue naye
ni jipu lilikuwepo ikulu, suala ambalo halikupata maelezo ya kutosha
kutoka kwa balozi huyo.
Alipoulizwa juu ya tetesi hizo alijibu kwa ufupi: “Hii ni Serikali ya mabadiliko.”
Kwa
upande wake Kijazi, alisema atafanya kazi kwa kuzingatia vipaumbele vya
Rais huku akimshauri namna sahihi za kuboresha mazingira ya utumishi
serikalini.
Akieleza juu ya majukumu yake mapya, alionyesha
kuyatambua ipasavyo na kubainisha kuwa atashirikiana na Baraza la
Mawaziri kwenye vikao vyao, bila kusahau kuzifuatilia wizara husika na
kuona endapo kila kitu kinaenda kama inavyotakiwa.
“Nitakutana
na mawaziri kwenye vikao vyao nitakavyoviandaa. Nitawasiliana na
kuwafuatilia watendaji wa wizara husika juu ya masuala yatakayokuwa
yamejitokeza ndani ya maeneo yao ya uwajibikaji. Kila mmoja atimize
wajibu wake ili Taifa lisonge mbele,” alisema Kijazi.
Ili kuitendea haki
hadhi ya utumishi wa umma, Kijazi ameahidi kuhakikisha kila kitu
kinasimamiwa kwa ukaribu huku akitoa msisitizo kwenye vipaumbele vya
Rais.
“Kwenye suala la mapato na rushwa, nitafuatilia kwa nguvu ili
kuongeza uwajibikaji kwa watumishi wa Serikali,” alisisitiza Kijazi.
Balozi
Kijazi aliteuliwa juzi kushika nafasi inayoachwa na Balozi Sefue. Kabla
ya uteuzi huo, Kijazi alikuwa mwakilishi wa Tanzania kwa nchi za India,
Singapore, Sri Lanka, Bangladesh na Nepal huku makazi yake yakiwa
jijini New Delhi, India kuanzia mwaka 2007.
Katika wadhifa huo,
alikuwa mkuu wa mabalozi wote wanaowakilisha Tanzania nje ya nchi pamoja
na mkuu wa mabalozi wa Afrika nchini India.
Kabla hajateuliwa kuwa
mwakilishi wa nchi, Kijazi amekuwa mtumishi serikalini kwa nafasi
mbalimbali ikiwamo Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi kuanzia mwaka 2002 mpaka
2006.
Kabla ya hapo alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Miundombinu kati ya mwaka 1996 hadi 2002.
Ndani
ya Wizara ya Ujenzi, kabla hajawa katibu mkuu, alikuwa mhandisi
mwandamizi wa ujenzi wa barabara kisha kupandishwa cheo na kuwa
mkurugenzi wa barabara za mikoa.
Kumbukumbu za taaluma yake
zinaonyesha kuwa alipata Sha hada yake ya kwanza ya Sayansi ya Uhandisi
wa Umma mwaka 1982 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na baadaye
Shahada ya Uzamili katika Uhandisi wa Barabara kutoka Chuo Kikuu cha
Birmingham, Uingereza mwaka 1992.
Jana wakati anaapishwa, saa
4:15 asubuhi, Kijazi alikuwa sambamba na mke wake, Fransiscar Kijazi na
kwa pamoja wamejaliwa watoto watatu, David, Emmanuel na Richard.
Kwa
heshima ya familia hiyo, baada ya kukamilisha protokali, Rais Magufuli
alipiga picha ya pamoja na familia ya mteule huyo mpya atakayehudumu
ikulu kuanzia sasa.
Hata hivyo kwa mara ya mwisho, Sefue
aliendelea na kazi yake mpaka jana Asubuhi na ndiye aliyemkabidhi Kijazi
kitabu kitakatifu cha Biblia, Katiba na kiapo cha uongozi ambacho
alisaini.
No comments:
Post a Comment