Monday 2 February 2015

Ebola ‘yaua’ soko la utalii Arusha



Arusha. Imeelezwa kuwa idadi ya watalii mkoani hapa imepungua kwa sababu mbalimbali zikiwamo tishio la ebola na ugaidi.
Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (Tato), Willy Chambulo alisema hayo hivi karibuni na kuongeza kuwa hali hiyo imesababisha hoteli za kitalii na nyingine kupunguza wafanyakazi.
Chambulo aliiomba Serikali kusaidia sekta hiyo kwa kueleza kuwa ebola haijangia Tanzania ili kuondoa wasiwasi kwa baadhi ya watalii ili waendelee kuja nchini na kuongeza pato la Taifa.
“Hata hoteli zangu sita nimezifunga na wenzangu ambao hawajafunga nao watafunga tu, kwa sababu ya kukosa watalii wanaoogopa ebola ambayo kwetu haipo,” alisema Chambulo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alisema ebola na tuhuma za ugaidi vimetikisa sekta ya utalii.
Alisema kila mwaka Tanzania imekuwa ikipokea watalii 250,000 wanaopitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta Kenya, lakini hivi sasa idadi hiyo imepungua.
Waziri Nyalandu alisema mwaka 2015 umepokewa vibaya katika sekta ya utalii kutokana na sakata hilo.
Alisema baadhi ya mataifa yanadhani ebola imeingia Afrika nzima.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Kitalii Tanzania ya Leopard, Zuhel Fazal alisema athari za ebola na ugaidi zimesababisha kampuni yake kupunguza mishahara ya wafanyakazi kwa asilimia 25.
Fazal alisema biashara ya utalii katika kampuni hiyo imepungua kwa asilimia 45.
Pia alisema ili kukabiliana na hali hiyo, wamepunguza pia marupurupu mengine kwa wafanyakazi kama vile kuwalipia kodi za nyumba.
Fazal aliiomba Serikali ishirikiane na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuondoa uvumi huo ili watalii warejee nchini kama awali.

No comments:

Post a Comment