Waendesha mashtaka kutoka Uswizi ambao wamekuwa wakifanya uchunguzi wa
tuhuma za ufisadi wametwaa magari 11 ya kifahari yaliyomilikiwa na mwana
wa kiongozi wa Equatorial Guinea.
Teodorin Obiang Nguema, mwana wa rais wa taifa hilo ambaye pia ni makamu wa rais, anatuhumiwa kulangua na kutakasa pesa.
Hajazungumzia tuhuma hizo kufikia sasa.
Maafisa wa Uswizi wametwaa jumla ya magari 11. Miongoni mwa magari hayo
ni gari la Porsche la thamani ya zaidi ya $830,000 (£667,000) na Bugatti
Veyron linalouzwa $2m (£1.7m).
Anatarajiwa kufika kortini Ufaransa kujibu mashtaka sawa na hayo mwaka ujao.
Waendesha mashtaka Geneva wanasema alinyakua utajiri wa mafuta wa taifa
hilo na kuutumia kununua vitu vya anasa, vikiwemo ndege ya kibinafsi na
kumbukumbu ya Michael Jackson.
Equatorial Guinea, taifa ndogo katika pwani ya Afrika, liligundua mafuta mwaka 1995.
Rais wake, Teodoro Obiang Nguema, ndiye aliyeongoza muda mrefu zaidi Afrika tangu atwae madaraka mwaka 1979.
Bw Obiang, 47, aliteuliwa kuwa makamu wa rais na babake mwezi Juni.
Anatarajiwa kufika Ufaransa kujibu mashtaka ya ufisadi na ubadhirifu wa
pesa za umma. Amepinga madai hayo katika mahakama ya UN na kuna
uwezekano kwamba hatafika mbele ya majaji Ufaransa.
No comments:
Post a Comment