Beki wa Yanga, Vincent Bossou, ametamka hadharani licha ya kukubali
kipigo cha mabai 2-1 kutoka kwa Mbeya City lakini hatamsahau mwamuzi wa
kati wa mchezo huo, Rajab Mrope kutokana na maamuzi yake kuwa tata.
Yanga ilipata kipigo hicho kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya katika
mchezo wa Ligi Kuu Bara, juzi, ambapo beki huyo raia wa Togo anasema
hajawahi kuona maamuzi kadhaa yaliyofanywa na refa huyo.
“Tumefungwa na tunakubali matokeo lakini sitasahau alichokifanya refa,
alikuwa na makosa mengi na maamuzi tata kibao ambayo yametugharimu kwa
kiasi kikubwa.
“Sidhani kama marefa wa namna hii wataweza kulikomboa soka la Tanzania
ambalo linataka kupiga hatua kutoka hapa lilipo kwa sababu hawajiamini
na hata kuchezesha kwenyewe inakuwa shida na hata kusimamia maamuzi
yao,” alisema Bossou.
Katika mchezo huo, mwamuzi alikubali bao la pili la Mbeya City lakini
baada ya kuzongwa na wachezaji wa Yanga waliodai haikuwa sahihi kwa kuwa
faulo iliyopigwa ilitekelezwa bila ruhusa ya mwamuzi, refa huyo
akaamuru faulo irudiwe, Mbeya City nao wakamzonga wakilalamika,
akabadili maamuzi tena na kukubali kuwa ni bao na mpira uwekwe kati.
No comments:
Post a Comment