Madini mapya yamegunduliwa nchini Tanzania, katika eneo lenye madini ya kipekee la Manyara, na kupewa jina Merelaniite.
Jina hilo limetokana na eneo ambalo madini hayo yalipatikana, Merelani
(Mererani) katika milima ya Lelatema katika wilaya ya Simanjiro katika
eneo la Manyara.
Eneo hilo linafahamika sana kwa madini ya Tanzanite.
Madini hayo yaligunduliwa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha
Kiteknolojia cha Michigan cha Marekani, makavazi ya historia asilia ya
London, chuo kikuu cha Di Firenze cha Italia na makavazi ya historia
asilia ya Smithsonian ya Washington.
Wataalamu sita waliofanya uchunguzi, kwenye makala iliyochapishwa kwenye
jarida la Minerals (Madini) wanasema madini hayo yana vipande
vinavyofanana na sharubu vya rangi ya kijivu vya urefu wa milimita moja
hivi, ingawa kuna baadhi vyenye urefu wa hadi mililita 12.
Kipenyo cha vipande hivyo ni mikrometa kadha.
Madini hayo yanakaribiana na madini ya zoisite (aina ya tanzanite),
prehnite, stilbite, chabazite, tremolite, diopside, quartz, calcite,
graphite, alabandite na wurtzite.
"Madini haya mapya yametambuliwa na taasisi inayoyapa majina madini, IMA
CNMNC (2016-042), na kupewa jina linalotokana na eneo yalipogunduliwa
kwa heshima ya wachimba migodi wa eneo hilo wa zamani, wanaoishi na
wanaofanya kazi," makala ya wataalamu hayo inasema.
"Wilaya ya Merelani imekuwa maarufu tangu mwishoni mwa miaka ya 1960
kutokana na aina ya madini ya thamani ya rangi ya samawati kwa jina
zoisite yafahamikayo kama tanzanite, lakini ni eneo muhimu sana kwa
wanaotafuta madini ya kipekee na ni eneo la kusisimua sana kutafuta
madini mapya," John Jaszczak, mwanafizikia katika Chuo Kikuu cha
Kiteknolojia cha Michigan, na aliyeongoza katika kuandika makala kuhusu
ugunduzi wa madini hayo anasema.
Madini hayo yalitambuliwa mara ya kwanza mwaka 2012 na Simon Harrison na
Michael Wise, bila wataalamu hao kuyafahamu vyema, pale walipogundua
vitu vilivyoonekana kama nyaya ndogo zilizokuwa zimedunga na kuingia
ndani ya vipande vya madini ya chabazite.
Baadaye uchunguzi zaidi ulifanywa na ikagunduliwa kwamba yalikuwa madini tofauti.
Mshirikishe mwenzako Unavyoweza kumshirikisha mwenzako
No comments:
Post a Comment