Thursday, 10 March 2016

Serikali ya kifalme ya Norway kusaidia Ukusanyaji wa Kodi Nchini


kij1
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje kutoka Serikali ya Kifalme ya Norway Mhe. Tone Skogen akifafanua jambo wakati Wa ufunguzi wa mapango wa ukusanyaji kodi nchini kushoto ni Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji.
Na  Kalonga Kasati
Serikali ya Kifalme ya Norway imetoa kiasi cha Dolla za kimarekani shilingi Milion 5 kwa Serikali ya Tanzania kwa kuwaunga mko no Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Serikali ya awamu ya tano katika jitihada zake katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato nchini.
Makubaliano hayo ya ufunguzi wa kuchangia mapato yamefanyika leo jijini Dar es salaam kati ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje kutoka Serikali ya Kifalme ya Norway Mhe. Tone Skogen pamoja na Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt Ashatu Kijaji.
Akizungumza katika ufunguzi huo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje kutoka Serikali ya Kifalme ya Norway Mhe. Tone Skogen amesema kuwa lengo la mpango huo ni kuimarisha na kuongeza kodi ya mapato ya ndani kwa  kuhakikisha kwamba mianya ya wakwepaji kodi inazuiwa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt Ashatu Kijaji amesema kuwa Serikali imeendelea kuimarisha na kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa ulipaji kodi bila kushurutishwa ili kuondokana bajeti  tegemezi kutoka nje.
“Lengo la kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa  ulipaji kodi bila kushurutishwa na kuzuia mianya Yote ya ukwepaji kulipa kodi  ni kuondokana na utegemezi wa bajeti na kuanza kujitegemea hivyo hatuwezi kufika huko bila kuimarisha ukusanyaji wa  mapato nchini” alisisitiza Naibu Waziri huyo.
Naye Kaimu Kamishna Mkuu TRA Bw. Alphayo Kidata ameishukuru Serikali ya Kifalme ya Norway kwa kuimarisha Uwezo wa wataalamu nchini kwa kuwawezesha  mbinu mbalimbali za kukagua mahesabu katika makampuni makubwa nchini.
Awali Serikali ya Kifalme ya Norway ilitoa zaidi ya Dola za kimarekani million 3 katika mpango huo wa kuimarisha Ukusanyaji wa mapato nchini.

No comments:

Post a Comment