Wednesday, 9 December 2015

WALIOKWEPA KODI TRA WALIPA BIL 8.6

WALIOKWEPA KODI TRA WALIPA BIL 8.6

 Na Kalonga Kasati
MAMLAKA ya Mapato nchini (TRA), imekusanya sh. bilioni 8.6 kutoka kwa kampuni zilizokwepa kulipa kodi tangu Rais Dkt. Magufuli atoe siku saba za wahusika kuzilipa kodi hizo kuanzia Desemba 3, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam , Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dkt. Philip Mpango, alisema fedha hizo zimekusanywa baada ya Rais Dkt. Magufuli kuwataka wafanyabiashara waliokwepa kodi walipe wenyewe ndani ya siku hizo.

Alisema baadhi ya kampuni zilizolipa kodi hizo ni Said Salim Bakhresa ambaye alilipa sh. bilioni 2, Tifo Global Trading Co.Ltd sh. milioni 310, IPS, Roofing Co.Ltd sh. milioni 800, Red East Building Co.Ltd sh. milioni 100, Zing Enterprises sh. milioni 325 na Sapato N Kyando sh. milioni 50.

"Hadi sasa TRA imekusanya sh. bilioni 8 na baada ya siku saba kuisha Desemba 11, mwaka huu, tutachukua hatua kwa kampuni zote ambazo zimeshindwa kulipa kodi nje ya muda uliotolewa na Rais," alisema.
Aliongeza kuwa, TRA hawatalala hadi kieleweke ikihakikisha kodi stahiki inakusanywa na kuwataka wafanyabiashara wote ambao ni waadilifu waendelee na biashara zao.

Dkt. Mpango alisema TRA na vyombo vingine vya dola vimeendelea kuchukua hatua dhidi ya watumishi wote ambao mwenendo wao unatia shaka, kuwasimamisha kazi, kuwachunguza, kuwapandisha kizimbani.

"Mtumishi mwingine mmoja ambaye ni Naibu Kamishna wa Forodha TRA, Patrick Mgoya, naye amesimamishwa kazi kuanzia jana, hadi kufikia Desemba 15, mwaka huu, kila mfanyakazi TRA awe ametaja mali anazomiliki kihalali na muda huo ukipita vyombo husika vitamchunguza," alisema Dkt. Mpango.

Aliwataka watumishi wote wa TRA kufanyakazi kwa kufuata sheria na kuongeza kuwa, Serikali inathamini mchango wa wafanyabiashara wote hasa waadilifu wanaolipa kodi kwa wakati ili kukuza uchumi wa nchi na itaendelea kuboresha mazingira ya wafanyabiashara nchini.

"Hakuna dhambi kwa Mtanzania kumiliki mali lakini azipate kihalali kwani TRA tunayoanza kuijenga tunataka iwe rafiki wa wafanyabiashara wanaolipa kodi.

Kwa upande wake, Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Lusekelo Mwaseba alisema mfanyabiashara yeyote ambaye alipitisha makontena au mizigo katika bandari yoyote au Kituo cha Forodha mipakani bila kulipa ushuru anatakiwa kulipa ndani ya muda wa msamaha uliotolewa na Rais Dkt. Magufuli.

TRA imewataka Watanzania wote kuwasiliana na Ofisi ya Makao Makuu na kutoa taarifa zinazohusu ukwepaji wa kodi, watumishi wasio waadilifu ambao hutoa lugha mbaya kwa wateja.

No comments:

Post a Comment