Sunday, 13 December 2015

RUSHWA NI ADUI WA HAKI KWA WANYONGE


10-8-2008 1-30-26 PM_0125 - Copy 
 Picha kwa Hisani Ya Maktaba

Kwanza kabisa Nianze Makala haya kwa kumshukuru Mungu kwa kutupa uhai, Hakika Anatupendelea Sisi sote tunaovuta Hewa yake Sasa.

Baada ya kusema hayo Nikumbushe tu kwamba Mwanzoni mwa utawala wake Rais Benjamin Mkapa aliunda tume ya kuchunguza Rushwa Nchini Na akamteua Jaji Joseph Sinde Warioba kuiongoza.

Kama kawaida yake, Jaji Warioba na Timu yake Wakafanya kazi Nzuri Mno, lakini Kama Mazoea, Matokeo Yake Yamebaki ni Karatasi kufichwa Makabatini Bila kufanyiwa kazi.

Tume ile iliyokuwa ikichunguza Mianya ya Rushwa Serikalini ilibainisha kila kitu na ikataja Idara za Serikali Zilizokubuhu kwa Rushwa.

Nasikitika kusema kwamba yaliyobainishwa Yalikodolewa macho tu Bila kufanyiwa kazi na Rais Wa Wakati huo na Matokeo yake Uzalendo Ukaisha Kwani wananchi Walikuwa Wakiona Wanaofaidi keki ya Taifa ni Wachache.

Rushwa sasa imekithiri na ufisadi umezidi kuongezeka serikalini kwa kiasi kisicho na Mfano, Nadhani Mpaka Baadhi ya Watendaji wakaona kuwa Rushwa ni Mtindo wa Maisha na siyo adui wa Haki kama alivyokuwa Akisema Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Niliandika sana kuhusu uzalendo katika nchi hii, Nikihimiza kila Mtanzania asikie uchungu mtu Mmoja akiiba mali za umma na kuwataka wananchi Kujitahidi kufanya kazi kwa Bidii ili kujenga nchi Na kujiletea Maendeleo.

Inawezekana kuna watu walikuwa wakinidhihaki kwa kukemea ufisadi lakini naamini kwamba sasa Wanajua kwa nini nilikuwa Nashauri Watu Wakemee Ufisadi na Rushwa.

Ujio katika utawala wa nchi wa Rais John Magufuli Unaweza kutuonesha ni vipi Watawala Wetu Wanafikiri juu ya Ufisadi na Bidhaa Zitokanazo na Ufisadi.

Katika hatua iliyowashangaza Wengi, Rais Magufuli Ameweza kuokoa Mabilioni ya Shilingi Ambazo Zilikwisha potelea Mifukoni Mwa Wachache kutokana na vitu hivyo viwili, Rushwa Na Ufisadi.

Katika kipindi kifupi cha Uongozi wake Rais Mpya Nchini, jamii imegundua kuwa kuna Baadhi ya Watendaji Hawana Huruma na Walalahoi na Wanajijali Wenyewe na familia zao.

Rushwa na ufisadi ni kitu kibaya Sana katika Nchi Na Huwa Najiuliza ni Ujasiri gani Unaowafanya Wakuu wa Serikali Waiibie Serikali yao Wenyewe Mabilioni ya Shilingi?

Niliwahi Kujiuliza huko nyuma kuwa iweje serikali Ishindwe kupaka Rangi Nyumba zake na watumishi Wanaoishi katika Nyumba hizo Wanajenga kila Mwaka na kujinunulia Magari ya Kifahari Wakati Pengine hawana hata Biashara Wanayoifanya?

Waliokuwa wanafanya Hayo Walikuwa Wanajua kuwa Wananchi Wanawaona lakini Wakawa Hawajali na kusema Watafanya nini?

Lakini kwa wale tunaotaka kufikiri Angalau kidogo, Watakubaliana nami kwamba Rais Magufuli ni mtu Ambaye yupo bega kwa bega na Watanzania Wanaotaka maendeleo ya kweli katika nchi yetu.

Hotuba zote alizozitoa kwa Taifa baada ya kushika Madaraka Zinaleta Matumaini kwamba huko Tuendako, Hakuna Mtanzania atakayekufa katika Hospitali za serikali kwa kukosa Dawa ya Vidonge Vya malaria na Moyo wa Uzalendo Utaongezeka.

 Inawezekana ikiwa kila Mmoja Wetu atahakikisha Anakuwa Askari wa kulinda Mali za Umma.

Kila Mtu afanye kazi kwa Bidii, kizalendo kwa lengo Moja tu kwamba Nchi yetu ipige Hatua Mbele Kuelekea kwenye Maendeleo.

Wakati Umefika wa kuwa Bega kwa Bega na Rais Magufuli. Kila Mmoja Wetu akiwa na Moyo wa Uzalendo Naamini Hatatoa Rushwa na hatafanya Ufisadi.
Makala Haya Yameandaliwa na Kalonga Kasati Wa Fofammedia.blogspot.com

No comments:

Post a Comment