Monday 27 March 2017

Mtandao wa Vijana Wanaoishi Na VVU Nchini Wahamasisha Watanznia Kupambana Na Kifua Kikuu

BBBBBBBBBBBBBBBMMMMMMMMMM
Na. Georgina Misama MAELEZO
Mtandao wa Vijana Wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (NYP+) kutoka Bagamoyo Mkoa wa Pwani, umetoa tamko la kuwataka vijana  na wananchi kwa ujumla kuongeza mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Kifua Kikuu katika kuadhimisha siku ya kifua kikuu Duniani.
Akiongea na Waandishi wa Habari katika kuadhimisha siku hiyo, Mwenyekiti wa NYP+ Bi. Mwanaharusi Mohamedi anasema kwamba Ugonjwa wa Kifua Kikuu ni hatari lakini unatibika ikiwa mgonjwa atazingatia tiba na masharti yake.
“Sisi Vijana tunaoishi na VVU tunawaomba watanzania wenzetu pamoja na wadau wote ambao wapo katika mapambano dhidi ya kifua kikuu, kufanya kila linalowezekana kuhakikisha tunautokomeza ugonjwa huu wa Kifua Kikuu” anasema Mwanaharusi.
Bi. Mwanaharusi aliongeza kuwa mtu anayeishi na VVU ni rahisi sana kupata maambukizi ya Kifua Kikuu kwasababu VVU vinapunguza kinga za mwili ambazo zingepambana na vijidudu vya maambukizi ya Kifua Kikuu.
Aidha, Vijana wa NYP+ wameipongeza Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kuweka mazingira mazuri na wezeshi katika kutekeleza mapambano hayo ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa dawa sahihi na ongezeko la vituo vya kutolea dawa hizo.
Akiongolea mikakati ya serikali katika kupambana na Kifua kikuu Bi. Zulfa Hamisi ambaye ni mjumbe wa NYP+ anawasihii wananchi wajitokeze kwa wingi kupima na kupatiwa tiba sahihi ya Kifua Kikuu kwani huduma hizo hutolewa sehemu nyingi na bila malipo ili taifa letu liweze kutokomeza kabisa Kifua Kikuu.
“Sisi vijana wa NYP+ tupo tayari kufanya uraghabishi na uhamasishaji pia kutoa elimu juu ya kupima na kupata tiba ya Kifua Kikuu katika vituo ambavyo serikali imeviweka kulingana na sera ya afya kitaifa”, anasema Bi. Zulfa.

Dunia huadhimisha Siku ya Kifua Kikuu  Machi 24, kila mwaka, ambapo kauli mbiu ya mwaka  2017 ni “Tuungane pamoja katika kutokomeza kifua kikuu” 

No comments:

Post a Comment