Thursday, 3 November 2016

Uzalishaji kutumia nishati ya jua ni moja ya malengo ya kampuni ya TBL Group kutunza mazingira

vi1
Gavin Van Wjik
vi2
Sehemu ya mitambo ya Panel za Umeme wa Jua katika kiwanda cha TBL Mbeya


 
Mapema mwezi uliopita kampuni ya TBL Group imeanza kufanya uzalishaji kwa kutumia nishati ya umeme wa jua katika kiwanda cha bia cha  Mbeya.Mwandishi wetu Maalum amefanya mahojiano na Mkurugenzi wa Ufundi wa kampuni hiyo Gavin Van Wjik, kujua kwa nini kampuni imeamua kutumia teknolojia hiyo.
 
Unaweza kutueleza kwa nini kampuni ya TBL Group imeanza kufanya uzalishaji kwa kutumia umeme wa nishati ya  jua (Solar Power)?
 
Moja ya  dhamira yetu  na ndoto yetu  kubwa ni  kuwa kampuni bora inayotengeneza bia na vinywaji vinginevyo katika dunia maridhawa.Ili kutimiza dhamira na ndoto hii tumekuwa tukilipa kipaumbele mkubwa suala la utunzaji wa mazingira,ikiwemo kuhamasisha jamii kuwa na unywaji wa kistaarabu bila kusahau kuwekeza kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili jamii tunapofanyia biashara zetu.Teknolojia hii mpya ya kuvuna umeme wa jua kwa ajili ya uzalishaji ni moja ya mkakati wetu wa kupunguza athari za uchafuzi wa mazingira kutokana na mchakato wa uzalishaji viwandani.
 
Je mbali na utunzaji wa mazingira teknolojia hii ina umuhimu hani kwa kampuni?
 
Teknolojia hii japo ni ngeni katika ukanda wetu wa bara la Afrika tayari inatumiwa na viwanda vikiwemo vya utengenezaji bia kwenye nchi zilizoendelea katika sekta ya viwanda na imeonekana kupunguza gharama za uzalishaji kwa kiasi kikubwa .
 
Tuna Imani wazalishaji wengi katika sekta ya viwanda watafuata nyayo zetu na kuanza kutumia teknolojia hii pia matarajio yetu ni kuona inapunguza gharama za uzalishaji .
 
Kwa nini mmechagua teknolojia hii kwa kutumia mitambo iliyotengenezwa nchini Ujerumani?
 
Tumefanya utafiti na kugundua ni teknolojia bora na siku zote tunaamini katika ubora!
 
Kampuni imejifunza kitu gani katika mchakato mzima wa kuanza kutumia teknolojia hii?
 
Kikubwa tulichojifunza ni kuwa tumefanya uamuzi sahihi wa kuileta nchini na katika muda mwafaka,tukiwa kama kampuni kubwa inayoongoza katika sekta ya viwanda nchini tuna wajibu wa kuwa mfano kwa viwanda vingine ili viweza kujifunza kutoka kwetu.Wakati huu ambapo serikali inahimiza kuingia kwenye taifa la viwanda ni muhimu kufanya mabadiliko ili kufanikisha lengo  hilo kwa vitendo.
 
Je ni mabadiliko gani mmeanza kuyaona tangu mmeanza kutumia teknolojia hii?
Ni mapema mno kufanya tathmini kwa kuwa ndio tumemaliza awamu ya kwanza ya kufunga Panel za kuvuna umeme zinazoweza kuzalisha KiloWatt 138 ambazo kwa sasa zinao uwezo  wa kukidhi mahitaji ya matumizi ya umeme wa kiwanda kwa asilimia zaidi ya 30%.
Mwakani tutaongeza mitambo mingine ambapo kazi hiyo ikikamilika itawezesha kiwanda kuendeshwa kwa kutumia zaidi umeme wa jua kuliko  kwa kuwa mkoani Mbeya hali ya hewa ni nzuri na kuna vipindi vya jua kwa muda mrefu katika mwaka kuweza kupata nishati ya jua ya kutosha.
Teknolojia hii haitaishia katika kiwanda cha Mbeya tu bali itatumika katika viwanda vingine vya kampuni ambapo itaendelea kusambazwa kwa awamu mbalimbali hatua kwa hatua.
Mbali na teknolojia hii tutaendelea kuleta teknolojia nyingine bora zenye kuondoa uharibifu wa mazingira ikiwemo kupunguza gharama za uzalishaji na kwenda sambamba na mataifa yaliyoendelea katika sekta ya viwanda.

No comments:

Post a Comment