TIMU ya taifa ya wanawake ya Tanzania, Twiga Stars inashuka dimbani
mjini Younde leo kumenyana na wenyeji, Cameroon katika mchezo wa
kirafiki wa kimataifa.
Twiga Stars ilioondoka Dar es Salaam juzi na kikosi cha wachezaji 17 na
viongozi sita kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ) ikipitia
Nairobi, Kenya.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alisema
jana kwamba Twiga Stars wapo huko kwa mwaliko wa wenyeji wao, Cameroon
ambao ni waandaaji wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake
mwaka 2016.
Lucas alisema Cameroon ambao wameamua kuipa heshima Tanzania na kuona
kuwa timu hiyo ina ubora na kwamba inafaa kuipimana ubavu kabla ya
kuanza kwa fainali hizo Novemba 19, mwaka huu.
Twiga Stars ambayo sehemu kubwa ya kikosi hicho kinaundwa na wachezaji
wa timu ya taifa ya Wanawake ya Tanzania Bara yaani Kilimanjaro Queens
ina rekodi nzuri ya kuwa kinara wa viwango vya ubora kwa nchi za Afrika
Mashariki na kati lakini zaidi ni mabinga wapya wa ukanda huo – ubingwa
uliopatikana Septemba, mwaka huu huko Uganda.
Rekodi hizo zimesukuma Shirikisho la Mpira wa Miguu la Cameroon
(FECAFOOT) – nyumbani kwa Rais wa CAF, Issa Hayatou kuikubali Twiga
Stars na hivyo kuomba kucheza nayo mwishoni mwa wiki hii. Twiga Stars
iko chini chini ya Makocha Sebastian Nkoma na Wasaidizi wake Edna Lema
na El Uterry Mohrery.
Kikosi cha Twiga Stars wamo makipa, Fatma Omari na Najiat Abbas; mabeki
ni Wema Richard, Sophia Mwasikili, Anastasia Katunzi, Maimuna Hamisi,
Fatuma Issa, Happiness Mwaipaja na Mary Masatu wakati viungo ni Donisia
Minja, Stumai Abdallah, Amina Ally, Anna Mwaisura na Fadila Kigarawa
ilhali washambuliaji ni Fatuma Swalehe, Asha Rashid na Mwanahamisi
Omari.
No comments:
Post a Comment